Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwanini kuna Mayele na Inonga Ligi Kuu Bara?

Inonga Mayele M Kwanini kuna Mayele na Inonga Ligi Kuu Bara?

Mon, 6 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika mchezo wa soka kuna mambo mengi ya kuzingatia ili timu ifanye vizuri hususan katika ngazi ya klabu, ambapo ndani yake yanahitajika maandalizi mazuri, uwepo wa benchi la ufundi bora na kubwa zaidi ni wachezaji wenye ubora mkubwa kwenye timu husika.

Katika kuzingatia hilo klabu nyingi zenye misuli imara kiuchumi zimekuwa zikifanya usajili mbalimbali ilimradi kuhakikisha kipengele cha wachezaji bora wanakuwa nao ili kupata mafanikio.

Katika kupata wachezaji bora kuna mambo mengi ya kuzingatia na hili linabaki kwenye kipengele cha jicho la wataalamu (skauti) ambao wanalinganisha wachezaji, timu na ligi na mazingira yake.

Ndio maana kwenye soka la Afrika timu nyingi zinazingatia mazingira ya kimaisha na taifa husika la wachezaji hususan kwenye kipengele cha utamaduni. Tukianzia hapa utamaduni unaanza kwenye lugha ambayo mchezaji anazungumza.

Kwanini? klabu nyingi za Afrika zenye utaratibu bora wa skauti na kuzingatia wataalamu wa eneo hilo huwa hawakurupuki kwenye kuchagua wachezaji, bali huwa wanazingatia mengi ili wachezaji wafanye vyema.

Mfano klabu zilizopiga hatua kubwa zaidi kwenye soka Afrika ni zile za Afrika Kaskazini ambazo huwa zinazungumza Kiarabu na Kifaransa isipokuwa Libya ambako ina Kitaliano pia.

Katika muktadha wa kuzingatia zaidi utamaduni wa kuchagua wachezaji hujikita katika lugha na mazingira yake. Ndio maana leo ni rahisi kuona wachezaji wengi wanaotokea mataifa yanayozungumza Kifaransa wakienda Kaskazini mwa Afrika.

Ndio maana Ben Malango Ngita na Luamba Ngoma Fabrice walikutana Raja Casablanca, kama ilivyo kwa Francy Kazadi na Mohamed Ouatara walikutana Wydad, haikushangaza kuona Prince Ibara akiwa USM Alger. Guy Mbenza kuwepo WAC na hata Yannick Bangala kwenda FAR Rabat.

Hao ni wachache kati ya wengi zaidi ambao utamaduni wao umetosha kuwapa maisha huko, Al Ahly na Aliou Dieng wa Mali, Zamalek na Kabongo Kasongo tangu wakati wa Mac Mboua na maisha yanaendelea.

Esperance De Tunis Dume iliyobeba mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa na viungo wawili bora, Frank Kom wa Cameroon na Fausine Coulibaly wa Ivory Coast, 2018 walicheza dhidi ya Al Ahly ya Salif Coulibaly wa Mali.

Hapo ni baadhi tu, lakini kuna kundi kubwa la wachezaji wanaoshindwa kutamba katika ligi nyingine kutokana na kutoshabihiana na utamaduni au mazingira.

Kwa miaka mingi wachezaji wengi kutoka Nigeria wamekuwa na wakati ngumu Tanzania mfano Emeh Izechukwu, Obi Obina, Abasalim Chidiebele mpaka kizazi cha kina Nelson Okwa na Victor Akpan bado wanahangaika kupata ubora wao.

Kwa sasa upepo wa skauti na kiwango bora kwa wachezaji wengi wa kigeni wanaocheza Tanzania ni wale wanaotoka DR Congo na hii ni tangu wakati wa Mayaula Mayoni, Shaaban Nonda - Yanga kuna nyota kama Fiston Mayele, Yannick Bangala na wengine ambao wamekuwa bora kwenye kikosi huku Simba walikuwa na Deo Kanda na sasa Inonga na ujio wa Jean Baleke umeanza na mguu mzuri.

Kwanini wanafanya vizuri? Sababu ni zile mbili kwanza sababu za mazingira ambapo ya DR Congo na Tanzania hayajaachana sana kwenye maeneo mengi na pili ni utamaduni ambalo ndilo kubwa zaidi - kwa maana ya lugha. Wapo wachezaji wanazungumza Kireno ambao soko lao sio kubwa sana kutokana na hali kutoendana nao hususan kwenye mazingira ya maisha na utamaduni wa lugha.

Ndio maana ni ngumu kwa wachezaji wa Angola, Msumbiji, Cape Verde, Guinea ya Ikweta, SaoTome and Principe kuwaona wanacheza katika mataifa mengine ya Afrika na kwao ni rahisi kwenda Ureno kuliko kubaki Afrika. Kwenye tathmini nzuri kwa klabu zetu juu ya skauti kwa sasa ni rahisi kuskauti kwa kuzingatia mazingira na utamaduni wa nchi husika ili kupata kilicho bora kwenye kikosi cha klabu.

Sio wachezaji wote wanaozungumza Kifaransa watafanikiwa Afrika Kaskazini. Sio wachezaji wote wanaotokea DR Congo watafanya vizuri Tanzania. Kuna mambo mengine ndani yake. Kuna kiwango cha uimarikaji wa mchezaji, yaani ‘improvement limit’ ambapo anaweza kuwa bora lakini akashindwa kuwa bora akihamia timu yenye uhitaji mkubwa zaidi wa kiwango chake na asiupate, au falsafa na mifumo ya kiufundishaji inaweza kumnyima fursa mchezaji kuonyesha ubora wake.

Columnist: Mwanaspoti