Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwani Simba wamekutwa na ugonjwa gani?

SIMBA KIKOSI KJ.jfif Kikosi cha Simba

Mon, 12 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ukiniuliza kama Simba wako sawasawa, nitasema hapana. Nawaona kama wagonjwa. Sidhani kaka wako sawa kiafya. Ni kama mtu mwenye Malaria iliyopanda kichwani. Ni kama mtu mwenye Degedege kali!

Miaka minne iliyopita, kila timu nchini kwetu pengine ingetamani kuwa kama Simba. Utulivu wa hali ya juu kwenye uongozi. Utulivu wa hali ya juu kwenye kiwango cha timu uwanjani. Simba haikufika robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa bahati mbaya.

Simba haikutwaa Ubingwa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu Bara kwa bahati mbaya. Timu ilikuwa timamu kiroho na kimwili, timu haikuwa na Malaria kali, timu hakuwa na Degedege. Nini kimewakuta Simba? Sina majibu.

Kama mwenzangu umebahatika kujua chochote, usisite kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Sidhani kama Simba iko timamu kimwili na kiakili msimu huu.

Sidhani kama kuna timu yoyote inataka kuwa kama Simba ya msimu huu, sidhani kama kuna timu inataka kuwa na viongozi kama wa Simba wa msimu huu. Sidhani. Sidhani kabisa!

Hadi kucheza mechi ya kwanza na Nyasa Big Bullets, tayari Simba imeshatumia makocha wanne msimu huu. Walianza msimu na Kocha Zoran Maki, akaja kocha wa muda Suleiman Matola, Juma Mgunda kama kocha mkuu kabla ya kuongezwa Sebastian Nkoma kwenye benchi! Haiwezi kuwa hali ya kawaida.

Hii sio Simba niliyoifahamu miaka minne iliyopita, hii sio Simba iliyoifunga mara mbali Al Ahly kwa Mkapa. Hii sio Simba iliyompiga As Vita. Makocha wanne ndani ya miezi miwili, kuna tatizo mahali. Timu haiwezi kuwa timamu kiroho na kimwili kwa utaratibu huu.

Ukiniuliza ni kwa nini Kocha Zoran ameondoka? Sina majibu. Ukiniuliza ni kwa nini Mgunda amepewa timu? Sina majibu pia!

Kabla ya Dirisha la usajili kufungwa karibu kila mchezaji alikuwa anataka kuondoka. Inasikitisha! Leo utasikia John Bocco anataka kuondoka, kesho utasikia Joash Onyango.

Kuna nini kinaendelea ndani ya Simba? Kama umepata habari zozote za ndani, tafadhali usisite kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Ukitazama usajili wenyewe ulivyofanyika ni Papatu Papatu tu! Timu inahitajika kocha hasa kutengeneza muunganiko wa timu.

Timu inahitahi watu hasa kuketa morali kikosini. Ushindani kila msimu unaongezeka na huenda msimu huu ukiwa mgumu zaidi kuliko misimu yote.

Ukitazama ubora wa washindani wa karibu wa Simba msimu huu kama Azam FC, Yanga na Singida Big Stars, unaogopa. Azam wako sawa mno. Singida ni balaa tupu. Hao Yanga ndiyo usiguse kabisa.

Simba wanahitaji kurudi relini mapema sana vinginevyo mambo yanaweza kuwa magumu. Sidhani kama timu iko sawa. Sidhani kama viongozi wako sawa.

Kocha Mkuu wa kudumu ni lazima apatikane mapema kwa sababu, hauwezi kwenda kushindana na wenzio kwa kutegemea kocha wa kuazima. Unahitaji kuwa na mtu mwenye uhakika wa ajira yake kutimiza malengo ya klabu.

Ule moto walionao Azam FC wakikukuta bado hujajielewa, unaweza kupigwa nyingi. Ule moto wa wazungu na Singida Big Stars wakikuta bado unajitafuta, wanaweza kukuaibisha.

Bado Simba ina wachezaji wazuri lakini bado hawana timu imara. Kuwa na wachezaji wazuri ni jambo moja, na kuwa na timu nzuri ni jambo la pili. Yale malengo ya kufika Nusu Fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hayawezi kutimia kwa kubahatisha.

Yale malengo ya kurejesha mataji yote ya ndani, hayawezi kutimia kwa kubadilisha makocha wanne ndani ya miezi miwili. Kuna kitu lazima kifanyike pale Simba tena kwa haraka sana. Sioni kama timu iko timamu kimwili na kiakili.

Viongozi na Benchi la Ufundi ni lazima warudi nyuma na kuziba panapovuja. Tulikuwa na ligi ya Farasi Wawili kwa miaka mingi sana lakini msimu huu, kuna timu kama nne zinazowania Ubingwa. Maisha yamebadilika. Sio msimu wa kujivutavuta. Sio msimu wa kujibembeleza. Unaweza kujikuta unatupwa kwenye nafasi ya tano.

Hao wachezaji wa Simba hadi sasa wameshafundishwa na makocha wanne ndani ya miezi miwili! Huenda Simba ndiyo timu ya kwanza duniani kuwa na makocha wengi msimu huu. Idadi ni kubwa sana. Chelsea wamebadili kocha lakini sio wanne. AFC Bournemouth wamebadili kocha lakini sio wanne.

Sidhani kama kuna timu imekuwa na makocha wengi msimu huu ndani ya miezi miwili kama Simba. Maisha ya soka hayawezi kwenda kwenye utamaduni huu.

Unataka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa kumuajiri kocha ambaye hajawahi kutwaa ubingwa? Sio kweli. Unataka kwenda Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa kumleta kocha ambaye hajawahi kabisa kushiriki michuano hiyo? Sio kweli.

Bado muda upo wa kujirekebisha. Bado muda upo wa kujiweka sawa. Baada ya kuwa na msimu mbaya msimu uliopita, wana Simba wanahitaji furaha msimu huu.

Wanataka kuiona timu yao ikileta makombe. Wanataka kuiona timu yao ikiwapa burudani. Maisha ya papatu papatu wana Simba hawayataki. Kama Kuna Degedege mahali, litibiwe mara moja.

Columnist: Mwanaspoti