Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwaheri Jemedari Magufuli, huna baya kwa wanamichezo

Jemedari Pic Data Kwaheri Jemedari Magufuli, huna baya kwa wanamichezo

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

NIANZE kwa kutoa pole kwa Watanzania kwa msiba mkubwa wa kuondokewa na kipenzi chetu Dk John Pombe Joseph Magufuli.

Ukiacha mambo ya maendeleo ya taifa aliyoyasimamia na kuyatekeleza, sisi watu wa michezo hususan soka tuna sehemu kubwa ya kumkumbuka.

Ni ujasiri wake ndio ulifanya Ligi Kuu Bara kuwa ligi ya kwanza Afrika kurejea baada ya mlipuko wa kwanza wa corona mwaka 2020.

Machi 2020 visa vya corona viliripotiwa sehemu kubwa ya Afrika na nchi zote zilisimamisha michezo.

Lakini baadaye Tanzania ikawa nchi ya kwanza kurudisha Ligi Kuu baada ya Rais Magufuli kuruhusu michezo kuendelea nchini kuanzia Juni 29, mwaka huo.

Wiki ya kwanza ya Julai ligi ikarudi na hakukuwa tena na kurudi nyuma hadi sasa.

Nchi zingine Zimbabwe kwa mfano, hadi sasa ligi yao haijarudi tangu Desemba 2019 pale msimu wao ulipokuwa ukihitimishwa.

Msimu wao mpya ulikuwa uanze Machi 2020, lakini ndiyo mwezi ambao corona iliingia Afrika na hadi leo ligi haijarudi tena.

Faida ya uamuzi wa Dk Magufuli kurudisha michezo nchini ndiyo tunaiona sasa kwa Simba SC na Namungo FC kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika.

Hii ni mara ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki taifa moja kuingiza timu mbili hatua ya makundi.

Pamoja na mambo mengine, timu zetu zimefaidika sana na kucheza kwa muda mrefu huku wenzetu wengi wakiwa wamefungiwa ndani au kuzuiwa kucheza.

Wakati Simba wanakutana na Plateau United ya Nigeria ilikuwa katika mwendelezo wa ligi ambayo ilikuwa katika mzunguko wa 13, lakini Nigeria hakukuwa na mpira kabisa.

Ilipocheza na Platinum FC ya Zimbabwe hali ilikuwa hivyohivyo kwa wapinzani wao, lakini wao walikuwa kwenye mwendelezo mzuri.

Simba na Namungo wakawa timamu kimwili na kiufundi huku wapinzani wao wakikosa utimamu kutokana na kutocheza muda mrefu.

Hakuna wa kumshukuru zaidi ya Mungu na Dk Magufuli. Mechi za nyumbani za Simba dhidi ya Plateau United na hata Platinum FC zilijaa mashabiki uwanjani waliohanikiza timu yao. Hii ni kwa sababu chuma, Dk Magufuli, aliruhusu mikusanyiko na watu kuendelea na shughuli zao ikiwemo kuingia kwenye viwanja vya mipira.

Lakini mechi za ugenini hakukuwa na mashabiki kwa sababu serikali zao ziliwazuia kuingia viwanjani.

Ushindi wa 4-0 nyumbani dhidi ya Platinum pia ulitokana na ‘vibe’ la mashabiki kutoka majukwaani. Ralph Kawondera yawezekana asingekosa bao la wazi yeye na nyavu kama siyo kuathirika na kelele kutoka mashabiki wa Simba Simba mchezo wote.

Namungo wamechezea nyumbani mechi zao nyingi za ugenini msimu huu.

Ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya De Agosto usingewezaka kama mechi ingechezwa Luanda jiji Angola.

Lakini haukuchezwa kule kwa sababu nchi yao ilikuwa na masharti magumu huku Dk Magufuli alitulegezea masharti hapa kwetu. Wakati anaruhusu michezo kuendelea alisema michezo huimarisha afya za wanaocheza kwa kuongeza kinga za mwili, hivyo kuwa na uwezo wa kupambana na maambukizi mengi yakiwemo ya corona.

Zaidi ya kurudisha michezo, Magufuli alikuwa mstari wa mbele kuamsha hisia za kukataa kushindwa kwa timu zetu.

Akizungumza na Taifa Stars, alishawahi kuelezea anavyochukia kushindwa kiasi cha kuwaza kutumia wanajeshi kwenye timu ya taifa.

Akiwa Kyela mkoani Mbeya akizungumzia kufanya vibaya kwa timu yetu ya taifa chini ya miaka 17 kwenye Afcon iliyofanyika nyumbani, Dk Magufuli alionesha kukerwa na matokeo hayo kiasi cha kushangaa tunafungwaje na timu ambazo nchi zina watu wachache kuliko yetu.

Hakuwa na maana kwamba idadi ya watu inahusika katika kuamua matokeo, lakini alikuwa anafikisha ujumbe kwamba mnapofungwa na nchi yenye idadi ndogo ya watu, mnawaumiza watu wengi zaidi (wa kwenu) kuliko wanaofurahia (wale nchi ndogo).

Hii ina maana kwamba viongozi wa michezo na wachezaji wanatakiwa kuweka kwenye akili zao kwamba wanatakiwa waelewe furaha kwenye nafsi za watu wetu zaidi ya milioni 50 kuliko kuacha furaha ikaenda kwenye nchi yenye watu chini ya milioni tano.

Wakati anatoa Sh50 milioni kwa Taifa Stars wakielekea Lesotho, aliwataka wasishinde la sivyo watazilipa hizo pesa. Hapa alikuwa anataka kuwatia hamasa ili wajione wanadaiwa na wananchi na Rais wao pamoja.

Ndiyo maana hata walipopoteza ule mchezo, hakuwadai kwa sababu haikuwa lengo lake.

Kauli aliyoitoa kwa Simba siku alipokuwa mgeni rasmi kwenye mechi yao ya mwisho ya msimu wa 2017/18 dhidi ya Kagera Sugar ndiyo chachu ya hasira yote hii unayoiona kutoka kwao.

Magufuli alianza kwa kuwatia hasira kwa kusema ‘wametobolewa tundu’ na Kagera Sugar halafu akawachana ‘live’ kwamba kwa kiwango walichokionyesha hawawezi kufika popote kwenye mashindano Afrika.

Simba wakafanyia kazi kiwango chao na walipoenda kwenye mashindano ya Afrika wakafuzu robo fainali. Siyo kitu kidogo! Japo hakuwa sana mtu wa michezo, lakini Dk Magufuli ameacha alama kubwa, hasa katika vichwa vya wanamichezo.

Ari ya kukataa kushindwa ambayo amekuwa akiisisitiza, ni kitu kikubwa sana katika mapambano ya kuusaka ushindi uwanjani.

Platinum FC ya Zimbabwe iliposti kutoa pole kwa watanzania kufuatia msiba huu, halafu wakasema walikutana na ari ya Dk Magufuli ya kukataa kushindwa pale walipocheza na watoto wake (Simba SC).

Platinum FC waliamini kwamba Simba walikuwa na ari ya baba yao, Dk Magufuli ndiyo maana walikuwa hawakamatiki.

Kuna mengi ya kusema kwa Magufuli kuhusi Michezo. Zawadi ya viwanja jijini Dodoma kwa wachezaji wote wa Stars waliofuzu kwa Afcon 2019.

Ahadi ya kujenga uwanja mkubwa zaidi ya Dar es Salaam jijini Dodoma.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz