Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa nini muhimu kupata chanjo

Chanjo Uganda Chanjo ya Corona

Wed, 4 Aug 2021 Chanzo: Mwananchi

Wakati utoaji chanjo dhidi ya virusi vya corona ukianza leo nchini kote, chanjo hizo zimeanza kugombewa, baada ya makundi ya watu kujitokeza kujiandikisha kuzipata.

Tanzania ilipokea awamu ya kwanza ya msaada wa dozi 1,058,400 za chanjo za corona aina ya Johnson & Johnson iliyotolewa na Marekani kupitia mpango wa Covax Facility.

Rais Samia Suluhu Hassan alizindua chanjo hiyo Julai 28, jijini Dar es Salaam kwa kuchanjwa, akifuatiwa na viongozi na watendaji wa Serikali.

Akizungumza na Mwananchi jana, Ofisa elimu wa afya kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Tumaini Haonga alisema tangu chanjo hiyo izunduliwe na kutangazwa vituo vya kutolea kumekuwa na mwitikio mkubwa wa watu wanaohitaji.

Alisema katika mfumo wa Tehama ambao unapokea maombi kuna idadi kubwa ya maombi, huku kwenye vituo vya afya navyo kuna waliokwenda kujiandikisha ili kupatiwa chanjo hiyo inayoanza kutolewa katika mikoa mbalimbali nchini.

“Watu wamekuwa na mwitikio mkubwa na inaonekana hata chanjo nyingine inaweza kuagizwa hivi karibuni kulingana na watu walivyoichangamkia. Hii ni hatua nzuri na tunaona hata kwenye mitandao sasa hivi inajadiliwa kwa mtazamo chanya,” alisema Dk Haonga.

Umuhimu wa chanjo

Wataalamu wa afya wanasema chanjo inamuongezea mtu nguvu ya kumkinga dhidi ya virusi hivyo na hata ikitokea amepata virusi vya corona asiugue sana

Wanasema chanjo hiyo pia inapunguza milipuko inayoweza kutokea mara kwa mara na ikijibainisha kwenye ugonjwa mkali unaohitaji matibabu ya muda mrefu, ikiwamo kulazwa wodini na kutumia mitungi ya oksijeni kwa gharama kubwa na dawa nyingine.

Pamoja na umuhimu wa chanjo hiyo kiafya, mtu aliyechanjwa ataweza kusafiri katika nchi mbalimbali ikiwamo zile zilioweka masharti ya kuchanjwa ili aingie katika nchi husika.

Wahariri wachanjwa

Jana, Wahariri wa vyombo vya habari nchini waliungana na makundi mengine kuunga mkono kampeni za uhamasishaji kwa vitendo uchomaji chanjo hiyo, wakisema ni salama na itasaidia kupunguza madhara kwa Watanzania.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema chanzo hiyo ni salama na itasaidia kupunguza athari kama ilivyoonyesha mafanikio katika mataifa ya Ulaya na Marekani.

Alisema Serikali kutoa chanjo kwa wanahabari ni uamuzi sahihi kutokana na asili ya majukumu yao yanayowafanya kuchangamana na watu mbalimbali.

“Wahariri na waandishi wa habari ni watu wanaofanya kazi mstari wa mbele kabisa, wanakutana na wagonjwa, madaktari, na wananchi wa kawaida. Tunaishukuru Serikali kwa uamuzi sahihi,” alisema Balile.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa vyumba vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu alisema, “Tunaamini shughuli za kiuchumi zimetuathiri sana, sasa bila afya kwa vyovyote vile harakati zetu za kukuza uchumi zitaathirika.”

Katibu tawala wa Handeni, Mashaka Mgeta ambaye pia ni mjumbe wa TEF, aliwataka wananchi kutumia fursa ya chanjo itakapowafikia kwa kuwa ndiyo njia salama ya kujikinga na ugonjwa huo uliogharimu maisha ya watu wengi. Waliozungumza na Mwananchi baada ya kupata chanjo walisema hawakuhisi madhara yoyote zaidi ya kusikia maumivu kidogo ya kuchomwa sindano.

RC Makalla atoa maagizo

Wakati utoaji wa chanjo ukiendelea, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alitangaza maelekezo kwa wasafiri wa daladala na mabasi kuvaa barakoa, akisema suala hilo ni lazima kwa lengo la kudhibiti corona.

Makalla alieleza hayo alipozungumza na na wanahabari kuhusu mwenendo wa uchukuaji wa tahadhari kwa wananchi, huku akisisitiza wananchi wachukue tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

“Ukiingia kwenye gari, kivuko lazima uvae barakoa, hili ni moja ya sharti. Nimefanya survey ukienda Kivukoni - Feri mtu anaingia na barakoa kwa sababu ya usimamizi akiwa ndani anaivua, akitaka kutoka anaiva tena,” alisema Makalla.

“Tumepokea taarifa ya utekelezaji wa mwongozo wa Wizara ya Afya kuhusu kujikinga na corona kutoka kila wilaya, tumebaini kuna ulegevu wa utekelezaji. Sasa utekelezaji wa hiari haupo tena bali ni lazima, ili kukabaliana na changamoto hii,” alisema Makalla.

Pia Makalla alikazia suala la abiria kukaa kwenye daladala kulingana na idadi ya viti vilivyomo ‘level seat’ akisema jambo hilo ni muhimu na wamiliki vyombo hivvyo vya usafiri kuanzia mwendokasi hadi daladala wanatakiwa kulizingatia.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume alisema mkoa huo umepata chanjo dozi 160,000, huku akieleza kumekuwa na mwamko mkubwa wa wakazi wa mkoa kuhitaji huduma hiyo tofauti na matarajio.

Msukuma abadili gia angani

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ ambaye awali alikuwa akisisitiza matumizi ya tiba asili na mitidawa kukabiliana na corona ni kama amebadilisha mtazamo huo na kuanza kuhimiza Watanzania kufuata ushauri wa wataalamu ikiwemo kupata chanjo. Akizungumza jijini Mwanza jana wakati wa hafla ya kukabidhi boti mbili za wagonjwa na uokoaji kwa mikoa ya Mwanza na Geita, Msukuma alisema; “Ninaamini sana dawa za kienyeji, lakini kwenye hilo la corona nawashauri Watanzani tuchome chanjo.

“Sisi wanasiasa tusibadilishe maneno…kama tunakunywa padadol tunashindwaje kuchanja? Mimi niko tayari kuwaongoza wananchi jimboni kwangu kuchanja,” alisema Msukuma.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel alisema boti hizo za Mv Ukerewe “Kazi iendelee” na Mv Nzera “kazi iendelee” zitahudumia zaidi ya wakazi 500, 000 wa maeneo ya visiwani ambapo kwa Wilaya ya Ukerewe yenye visiwa 38, boti hiyo itahudumia zaidi ya watu 476, 844.

Kwa upande mwingine, Mkoa wa Dodoma umepokea chanjo 50,000 za Covid 19 na hadi jana asubuhi watu 900 walikuwa wamejiorodhesha kuchanjwa.

Akizungumza baada ya kikao cha viongozi wa dini, siasa, kijamii na Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka alisema vituo 28 vimepangwa kutoa chanjo hiyo. Alisema kati vituo hivyo saba viko katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma Mjini na vituo vitatu tatu kwa kila halmashauri. Alisema uzinduzi wa chanjo kimkoa utafanyika leo, saa 3.00 asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

“Sisi katika mkoa tumeweka utaratibu chanjo zetu zimepelekwa katika wilaya saba. Maeneo yote yameainishwa kwenye hospitali na vituo vya afya,”alisema.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Best Magoma alisema chanjo hizo zimefika katika halmashauri na usambazaji katika vituo vilivyopangwa kutoa chanjo unaendelea.

“Mwitikio ni mzuri (wanaohitaji chanjo) tunapokea simu kutoka kwa watu mbalimbali wakiulizia kuhusu chanjo, kwa hiyo utayari ni mzuri, wananchi wameelewa na wako tayari kuchanjwa,” alisema.

Alisema jumla ya watu 900 walikuwa wamejiorodhesha hadi kufikia jana asubuhi na kwamba utoaji chanjo hiyo utatumia mfumo unaotumika kwa utoaji chanjo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Columnist: Mwananchi