Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa nini Polepole amepewa Ubalozi?

Polepole1 Humphrey Polepole

Tue, 15 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Mapinduzi ‘CCM’ alichokuwa akikitumikia kwa nafasi ya ukatibu mwenezi, kilikuwa kimemuweka kando.

Namzungumzia Humphrey Polepole ambaye kujulikana kwake kulianza wakati wa Bunge la Katiba na mchakato wake.

Jana na leo, Polepole amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa balozi wa Tanzania nchini Malawi.

Maisha ya hivi karibuni ya kijana huyo yamekuwa kama ya samaki anayetarajiwa kuvuliwa wakati wowote kutoka mtoni; hii ni falsafa ya maneno tu.

Kikubwa kinachomhusu Polepole ni kuonekana na baadhi ya watu kuwa haendi njia moja na msimamo wa chama chake cha CCM.

Mfano; Rais Samia alipozindua kampeni ya chanjo ya Uviko 19, yeye alisema “sichanji.”

Msimamo huo ulionekana kama utovu wa nidhamu kwa rais ambaye ni mwenyekiti wa chama chake na kuwaleta kilingeni baadhi ya wanachama wenzake na kushinikiza Polepole atimuliwe kwenye chama maana amekuwa msumbufu.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa CCM na Katibu Mkuu wake, Daniel Chongolo waliendelea kumvumilia Polepole ambaye alionekana kusemasema mitandaoni na wakati mwingine kuwaita majina mabaya baadhi ya wanachama wenzake.

Kupitia kipindi chake kwenye mtandao wa YouTube alichokiita Shule ya Uongozi, Polepole alikuwa akitupa madongo gizani akiwalenga baadhi ya wanachama wenzake ambao aliwatuhumu kumgombanisha na rais.

Ingawa haipendezi kuwataja majina watu alikuwa akivutana nao Polepole lakini ni wazi kuwa hakuwa kipenzi cha wengi ndani ya CCM hasa nyakati hizi.

Chongolo aliwahi kusema: Mbuzi aliyefungwa kamba kumshika kwake ni kuvuta kamba na kumalizana naye.

Kauli hiyo ilitafsiriwa kuwa ilimlenga Polepole ambaye wakati fulani shinikizo la kutaka avuliwe uanachama lilikuwa kubwa.

Hata hivyo, Polepole mwenyewe amekuwa haonekani kutishika pale anapoambiwa hivyo na mara nyingi amekuwa akijibu kuwa yuko tayari kwa lolote hata kupoteza ubunge.

Wakati watu wakijawa na hisia kuwa Polepole ni mtukutu ndani ya CCM na chochote kinaweza kumpata; ghafla ameteuliwa kuwa balozi, jambo lililowafanya baadhi ya watu kushangaa na kujiuliza uteuzi huo una maana gani?

Ifahamike kuwa uteuzi huo umemtoa Polepole kwenye nafasi ya ubunge ambayo kwa maoni ya wengi ina uhakika zaidi kuliko ile ya ubalozi ambayo amepewa.

Jicho mitandaoni limekumbana na mawazo kinzani kutoka kwa baadhi ya watu kwamba uteuzi huo umelenga kumziba mdomo kijana huyo mwenye uwezo mkubwa wa kuzungumza kwa hoja.

Aidha, wengine amejiaminisha kwamba huende akawa kwenye safari ileile ya kuondolewa.

Wanasema, kumtoa balozi kwenye nafasi yake ni rahisi kuliko mchakato wa kumtoa mbunge.

Yote haya ni maneno ambayo watu wamepewa uhuru kikatiba kuyajadili lakini Rais Samia amesema, amemteua Polepole aende akachape kazi Malawi na kwamba kabla ya kwenda huko atampeleka kwenye Chuo cha Diplomasia akamnoe kidogo kisha watakutana na kuzungumza kwa kirefu.

Columnist: www.tanzaniaweb.live