Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa mziki huu wa Simba... wataomba poo!

Mziki Wa Simba Wachezaji wa Simba SC wakiwa mazoezini

Tue, 17 Aug 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Ijumaa ya Agosti 6, kuliripotiwa taarifa ya umafia walioufanya Simba wa kumpora juu kwa juu beki kisiki Mkongomanii, Hennock Inonga Baka ‘Varane’ aliyekuwa akitakiwa na Yanga, lakini kuna watu waliguna, hata pale tuliporipoti alipoenda kupatiwa chanjo ya corona na kikosi hicho cha Msimbazi. Sasa katika kuonyesha hatubahatishi, beki huyo yupo Morocco akikiwasha na mabosi wake wamemtambulisha rasmi kumaliza utata.

Mabosi wa Simba walimtambulisha rasmi beki huyo mwenye rasta na kumaliza utata, lakini ujio wake Msimbazi na nyota wengine wapya kikosini, umewafanya mashabiki wa Simba kuamini kuwa wapinzani wao kwa msimu ujao wa mashindano lazima wataomba poo, huku benchi la ufundi sasa likikuna kichwa namna ya kuwatumia kuleta dhahama kwa wapinzani kwao, chama limekamilika!

Majembe hayo akiwamo Pape Ousmane Sakho, Duncan Nyoni ‘Monster’, Peter Banda na wengine yameongeza ushindani wa namba, lakini kwa benchi la ufundi la Simba bila shaka litakuwa na wakati mgumu katika kupanga kikosi cha kwanza cha timu hiyo, kwa vile watakuwa na machaguo mengi ya kibabe.

Usajili huo umefanya baadhi ya nafasi kuwa na nyota wawili hadi watatu ambao wanaonekana wana kiwango bora hivyo ni wazi kwamba kocha, Didier Gomes Da Rosa atakuwa na kibarua katika uteuzi wa kikosi lakini pia kingine ni kuhakikisha analinda viwango vya nyota wake kwa kubalansi muda wa kucheza kwa kila mmoja.

Wachezaji wapya mbali na kina Varane ni Saido Kanoute kutoka Mali na wazawa Jimson Mwanuke, Yusuph Mhilu, Abdulswamad Kassim, Kibu Dennis, Jeremiah Kisubi na Israel Patrick.

Kwa namna kikosi cha Simba kilivyo, uwezekano wa wazawa waliosajiliwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza ni finyu na ni wazi kwamba kwa anayetaka kuwa na namba anapaswa kufanya kazi ya ziada ili kulishawishi benchi la ufundi kumpa nafasi.

Huenda kusiwe na mabadiliko makubwa katika safu ya ulinzi na idadi kubwa ya wachezaji waliokuwemo katika kikosi cha kwanza msimu uliopita wana nafasi kubwa ya kuendelea kucheza kikosini

Upo uwezekano wa Varane’ aliyesajiliwa kutoka DR Congo kupewa nafasi ya kucheza kikosini kama beki wa kati sambamba na Joash Onyango ili waanze kuzoeana badala ya Pascal Wawa ambaye umri umeonekana kumtupa mkono huku Simba wakiwa hawana mpango naye wa muda mrefu.

Ibanga na Onyango watacheza pamoja na kipa Aishi Manula na mabeki wawili wa pembeni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomary Kapombe.

Kama kocha Gomes ataamua kutumia viungo wawili wa ulinzi, bila shaka Taddeo Lwanga ataendelea kucheza na nafasi nyingine moja kuna uwezekano mkubwa akapangwa nyota ambaye Simba wamempata kutoka Al Ahli Tripoli ya Libya, raia wa Mali, Saido Kanoute.

Lakini kama ataamua kutumia mfumo wa kuwa na kiungo mmoja wa ulinzi, ni wazi Kanoute atakuwa na nafasi kubwa ya kucheza kama akiwa fiti kwani ana uwezo mkubwa wa kuilinda safu ya ulinzi, kuchezesha timu na kuisukuma iende mbele.

Upande wa mawinga Gomes ndio ana mtihani mkubwa katika kuamua nani wa kuwepo katika kikosi cha kwanza kwani nyota wake watatu wapya, Nyoni, Banda na Sakho wameonyesha uwezo mkubwa wa kucheza katika nafasi hiyo, lakini wapo Bernard Morrison na Hassan Dilunga ambao msimu uliopita walitumika pia bila kuwasahau Mhilu na Mwanuke waliosajiliwa.

Uzoefu na mahitaji ya Simba vinaonekana vinaweza kuwafanya Duncan Nyoni na Sakho kupewa nafasi ya kuanza kwani Morrison mara nyingi huwa anafanya vizuri akiingia kutokea benchi wakati Banda anaweza asianzishwe mara kwa mara ili kumpunguzia presha pamoja na kumfanya azoee taratibu.

Bila shaka Rally Bwalya atapewa nafasi kubwa ya kucheza kama kiungo mshambuliaji lakini pia kama akikosekana, Sakho anamudu vyema kucheza katika nafasi hiyo.

Kama kocha Gomes ataamua kutumia mshambuliaji mmoja wa kati, nahodha John Bocco katika mechi nyingi anaweza kupewa nafasi ya kuanza lakini ikiwa atatumia washambuliaji wawili, ni wazi kwamba nyota huyo atapangwa sambamba na Chris Mugalu.

Kikosi na mfumo wowote ambao Gomes atautumia, bado atabakia kuwa na kundi kubwa la nyota katika benchi ambao anaweza kuwatumia kubadili mchezo pindi mambo yakionekana hayaendi sawa kwa wale walioanza.

Kikosi cha Simba katika mfumo wa 4-2-3-1 ambao Gomes anapenda kuutumia kinaweza kuwa hivi Aishi Manula, Kapombe, Tshabalala, Varane, Onyango, Lwanga, Nyoni, Kanoute, Bocco, Bwalya na Sakho.

Katika benchi kunaweza kuwa na Beno Kakolanya, Wawa, Erasto Nyoni, Morrison, Banda, Jonas Mkude na Mugalu.

Kocha Meja Mstaafu Abdul Mingange amesema usajili uliofanywa na Simba ni mzuri lakini vikosi vitapangwa kulingana na mahitaji ya kocha.

“Hao wachezaji waliosajiliwa, kocha ndio amewapendekeza na anajua atawatumia vipi hivyo bila shaka kila mmoja atapata nafasi kwa namna mwalimu alivyofanya tathmini ya aina ya wapinzani anaokwenda kukutana nao. Kwa mechi ambazo atapanga kushambulia atapanga wachezaji ambao anaamini watamudu hilo kama ambavyo itakuwa iwapo ataamua kucheza kwa kujilinda.”

Columnist: Mwanaspoti