Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa mivutano hii mtatokaje uchaguzi mkuu wa Oktoba?

98893 Pic+mnyika Kwa mivutano hii mtatokaje uchaguzi mkuu wa Oktoba?

Wed, 10 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKATI macho na masikio yanaelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, vyama vya upinzani vimeanza kunyang'anyana wanachama hali inayoashiria uhasama, kudhoofika, kugawana kura na hatimaye kuambulia kushindwa.

Kunyang'anyana wanachama ni dalili kwamba kila chama kimejiandaa kupambana kivyake katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Wapo baadhi ya wabunge kutoka Chadema kama Wilfred Lwakatare Bukoba Mjini ambaye ameshajiunga na Chama cha Wananchi (CUF), Anthony Komu Moshi Vijiji na Joseph Selesini (Rombo) waliotangaza kuhamia NCCR- Mageuzi.

Hizo ni dalili kwamba kila chama kinataka kujiimarisha, lakini pia katika kujiimarisha huko, kinaweza kudhoofisha upinzani iwapo kila mmoja ataamua kusimama kivyake badala ya kushirikiana.

Waswahili wanasema 'umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu', hivyo vyama vikiruhusu utengano, ni wazi kwamba vinajidhoofisha vyenyewe na vikishindwa visitafute visingizio.

Lakini pia, kuna wito uliotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kuvuta vyama vya upinzani kuandika maombi ya ushirikiano, ambapo kinasema, kinatafuta ushirikiano na vyama ambavyo kinaviita makini ili viungane kwa ajili ya uchaguzi huo wa rais, wabunge na madiwani.

Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, ndiye aliyetoa tangazo hilo hivi karibuni wakati akizungumzia wanachama wanaotaka kuwania urais, kwamba taarifa za kusudio la kugombea urais kupitia chama hicho zinapaswa kuwasilishwa katika ofisi ya Katibu Mkuu na baadaye zitajadiliwa na Kamati Kuu ya chama hicho na kutolewa uamuzi.

Tangazo la Chadema la kutaka ushirikiano linakuja wakati kukiwa na hilo tatizo la vyama vya upinzani kuchukuliana wanachama, hali kama niliyosema, huenda ikawa ni changamoto kwa upinzani kuwa na nguvu kama ilivyokuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Ushirikiano ambao chama hicho kinataka ni ngazi zote kuanzia nafasi ya udiwani, ubunge na urais lengo likiwa ni kuibuka na ushindi ingawa kwa mazingira yalivyo ya kuchukuliwa na wanachama yanaweza kuwa ni kikwazo cha kupata washirika wengi, hivyo ni muhimu vyama vya upinzani kutafakari mara mbili.

Pamoja na kuchukuliana wanachama, baadhi ya vyama vya upinzani vimetoa majibu kuhusu ombi la Chadema kwa ajili ya ushirikiano kila kimoja kikielezea jinsia, ambavyo kinadhani ushirikiano huo unaweza kusaidia kuvifanya vikaibuka na ushindi mwaka huu wa 2020.

WAITIKIA WITO

Chama cha ACT_Wazalendo kinaeleza kuwa kimeitikia wito uliotolewa na Chadema wa kushirikiana katika uchaguzi huo kwa kukiandikia barua ya kuanza rasmi mazungumzo ya ushirikiano huo.

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu. anasema, chama chake kinaamini katika ushirikiano kwa vile ndiyo silaha pekee ya kuhakikisha CCM inaondoka madarakani katika uchaguzi wa mwaka huu.

Ado anasema, vyama vya upinzani vikishikamana na kuweka tofauti za kiitikadi pembeni, vina fursa kubwa ya kuiondoa CCM madarakani, hivyo anaamini mazungumzo hayo na Chadema, yatafikia katika hatua nzuri, na kwamba jambo kubwa katika mambo ya ushirikiano ni utayari.

"Chadema wameonyesha hilo na wametangaza kwamba mchakato unaweza kuanza na sisi ACT-Wazalendo…tumeonyesha utayari na tumewajibu kwa barua, hiyo inakupa picha kwamba tunakoenda ni kuzuri," anasema Shaibu.

Anafafanua kuwa chama chao kina matumaini kwamba katika muda uliopo wa kujiandaa na uchaguzi mkuu, watafanikiwa kutengeneza vuguvugu kubwa kwa ajili ya ushindi katika uchaguzi ujao.

KUKATAA USHIRIKA

Chama cha NCCR-Mageuzi, kwa upande wake kinaviita vyama vingine vya upinzani kuungana nacho kwenye uchaguzi mkuu, na kwamba hakina shida ushirikiano, lakini kinashangaa kinavyochafuliwa kwenye mitandao kwa kupokea wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani.

Mwenyekiti wa chama hicho taifa, James Mbatia ndiye anayekaririwa na vyombo vya habari akisema hayo, lakini anaongeza kuwa chama chake kimeweka milango wazi kwa chama chochote kinachotaka ushirikiano na NCCR-Mageuzi.

"NCCR Mageuzi ni kati ya vyama vya siasa ambavyo vinaamini kwenye ushirikiano. Hata Ukawa ni zao la NCCR. Nasisitiza chama chetu kinaamini ushirikiano na umoja," anasema Mbatia.

MSIMAMO WA CUF

Wakati vyama hivyo vikisema hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba, amekuja na masharti ya ushirikiano kwa viongozi wenzake wa vyama vya siasa.

Anasema, chama chake kipo tayari kuungana na Chadema na ACT-Wazalendo, pamoja na vyama vingine vya upinzani, lakini anaweka sharti kwamba visipokee 'mabaki' kutoka CCM.

"CUF haiko tayari kushirikiana na vyama vinavyosubiria wagombea walioenguliwa na kuonekana hawafai katika nafasi mbalimbali ndani ya CCM," Prof. Lipumba anasema.

Hivyo vyama vinajiandaa kwa ajili ya kuikabili CCM katika uchaguzi mkuu, huku kukiwa na wito iliotolewa na Chadema kwa vyama vya siasa vyenye nia ya kushirikiana nacho.

ILIVYOKUWA 2015

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo, baadhi ya vyama vya siasa viliungana vikiwa chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioanzishwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba.

Vyama hivyo vilikuwa ni Chadema, NCCR- Mageuzi, CUFna NLD, ambavyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo vilishirikiana kwa kugawana baadhi ya majimbo na kata.

Hatua hiyo ilisaidia kuvifanya vyama hivyo kushinda baadhi ya majimbo na kata, huku Chadema na CUF vikifaidika zaidi na ushirikiano huo ambao sasa vimeanza tena mkakati wa kuufanikisha huku vikiwa vimechukuliana na wanachama, hali ambayo wakati mwingine inaweza kuchangia kuvigawa.

Ushirikiano unajengwa na umoja, sasa kama vyama vyenyewe vinachukuliana wanachama, vinaweza kuwa na umoja imara wa kuvifanya vikapenya kwenye uchaguzi huo?

Columnist: www.tanzaniaweb.live