Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa matokeo haya, acha Fei Toto ahangaike

Feisal Salum TFF 1 1140x640 Faisal Salum "Fei Toto"

Tue, 9 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna dhana mbili hadi sasa, Fei Toto aadhibiwe kwa kukaidi maagizo ya klabu yake ya kutakiwa kuripoti kambini na adhabu iwe kutimuliwa, au Yanga ishikilie hapohapo ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine na onyo kwa yeyote atakayetaka kuvunja mkataba wake kiholela.

Wale wanaotaka aadhibiwe ili suala lake lifikie mwisho, pia wanaamini kuwa kitendo cha Feisal Salum kuivimbia Yanga kwa kutomjali kimaslahi, amesaidia kundi la wachezaji wazawa ambao malipo yao yamekuwa ni ya chini kulinganisha na wachezaji wageni.

Kwa kuwa Yanga imetangaza kuongeza mikataba ya baadhi ya wachezaji kama Ibrahim Bacca na wengine na kuboresha maslahi yao, fikra za kundi hilo la pili zinachukulia kuwa mpango huo umetokana na kupata fundisho katika sakata la Fei Toto.

Hili kundi linasahau kuwa kila mwishoni mwa msimu huo kuna zile habari ambazo klabu zetu kubwa huziandaa kwa ajili ya kuwarusha mioyo mashabiki wao. Ipo klabu ambayo hutangaza kusaini mikataba mipya na wachezaji saa 7:00 mchana na kuwataka mashabiki na wengine kulipia vifurushi ili inapofika muda huo wajue ni mchezaji gani kasajiliwa au yupi ameongezewa mkataba na maslahi.

Ipo klabu nyingine maarufu kwa masofa meupe ya ofisi ya mmoja wa viongozi au wadhamini. Masofa hayo hutumika kutangaza usajili mpya au kuongeza mikataba ya wachezaji wanaokaribia kumaliza mikataba yao.

Na hawa huweza kuwashindisha macho mashabiki wao kwa kuamua kutangaza usajili huo au kuongeza mkataba majira ya saa 6:00 ama usiku wa manane.

Ni kwa jinsi hiyo, ni dhahiri kuwa uongezaji mikataba ambao mara zote huambatana na uboreshaji mikataba, haujaanza kwa sababu ya sakata la Fei Toto, bali ulishakuwepo kwa muda mrefu, tatizo linaloweza kuonekana ni uwezo mdogo wa wachezaji au mawakala au mameneja wao katika kukubaliana viwango vya malipo kwa kuzingatia ubora wa mchezaji na urefu wa mkataba.

Lakini la pili ni kwamba sakata la Fei Toto halihusu maslahi bali nia nyingine nje ya maslahi. Tangu sakatahilo lilipoanza, hakuna mahali ambako Fei Toto mwenyewe, wala wakala wake aliyewahi kusema kuwa kinachotakiwa ni kuboreshwa kwa maslahi, bali kutaka kuondoka.

Habari za maslahi madogo kwenye mkataba wake zimekuwa zikisambazwa na vyombo vya habari tu na hazijawahi kujengwa juu ya msingi wa ukweli fulani uliowahi kutokea, yaani kuwa zilitokana na kutokubaliana kati ya Yanga na Fei Toto kuhusu kuboreshwa kwa maslahi yake.

Angalau, kama kulikuwa na huo mchakato wa kujadiliana kuboresha mkataba halafu ikashindikana, au madai ya mchezaji ya kutaka kuboreshewa maslahi kupuuzwa, basi uvumi kwamba Fei Toto anataka kuondoka Yanga kwa sababu imeshindwa kumboreshea maslahi yake ungekuwa na msingi.

Lakini, zaidi ya yule mama kusema kuwa wamekuwa wakiishi maisha magumu, kiasi cha kula ugali na sukari, hakuna taarifa zozote za kulalamikia maslahi madogo licha ya umuhimu wake mkubwa kwenye timu.

Kwa hiyo, yale maelezo ya baadhi ya wachambuzi kuwa sakata la Fei Toto limeanza kunufaisha wazawa, hazina msingi wowote za kubuni na kuunganishaunganisha matukio. Fei Toto hajawahi kueleza kuwa anataka kuondoka kwa sababu klabu imeshindwa kumlipa kulingana na utashi wake.

Na hata mwanasheria wake yule wa kwanza alikuwa akikaririwa mara kwa mara akisema Fei Toto hataki tena kuichezea Yanga, lakini hakuwa na sababu nzito za kueleza sababu za kufikia uamuzi huo.

Kundi la pili ambalo linataka Yanga ishikilie hapohapo ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine watakaotaka kuvunja mikataba yao kiholela, linaamini kuwa Fei Toto anapotezwa na watu ambao wako nyuma yake na hawataki kujitokeza hadharani kutokana na sheria za soka kuwa kali dhidi ya watu wanaokiuka kanuni za ununuzi wa wachezaji.

Kundi hili, ambalo hata mimi naliona liko sahihi, linaamini kuwa Fei Toto hawezi kutaka kuvunja mkataba kwanza, halafu 'eti' kesho ndio aanze kutafuta klabu ya kujiunga nayo. Ni sanaa.

Ni lazima kuna klabu ambayo imefanikisha yote hayo kama kulipia zile Sh112 milioni na baadaye kumpeleka Dubai kwa mazoezi binafsi, mambo ambayo yangekuwa magumu kuyafanya kwa kudunduliza Sh4 milioni za mshahara wa kila mwezi kupata zaidi ya shilingi milioni mia moja na nyingine za safari ya Dubai.

Kubadilisha wanasheria ni ishara ya kuzidiwa nguvu kwa upande wake na hivyo kuanza kushika popote panaposhikika ili kujiokoa.

Kwa hiyo kunaonekana kuna tatizo la ushauri wa kisheria kwa Fei Toto kiasi cha kufikia hatua mchezaji anashindwa kucheza kwa takriban miezi mitano sasa, lakini hao wanaoitwa wanasheria wake hawalioni hilo na athari zake kimpira.

Binafsi naamini kuwa wakala au mwanasheria aliyejikita katika mpira wa miguu, hujali sana kiwango cha mchezaji ndio maana kila anapompigania huhakikisha mchezaji haathiriki na mzozo wa kisheria kuhusu maslahi yake au uhamisho wake kwenda klabu nyingine.

Mara zote unasikia mazungumzo ya mchezaji na klabu bado hayajafikia muafaka, lakini mchezaji anaendelea kuonekana uwanjani na kucheza kwa kiwango chake cha juu hadi yanapokamilika kwa pande zote kukubaliana au kukubaliana kutokubaliana.

Tuliona sakata la Kylien Mbappe, Paris Saint Germain na Real Madrid mwaka jana. Mbappe alikuwa ameshaamua kuondoka kwenda klabu ambayo amekuwa anaiota, lakini wakati wa kuelekea mwishoni mwa msimu, wanasheria wake walifanya kazi kubwa hadi mchezaji akaghairi na kubaki PSG. Katika muda wote huo, Mbappe aliendelea kusakata soka bila kuathirika na hadi leo hana tatizo lolote licha ya taarifa mpya za kutaka kutimiza ndoto yake.

Kwa hiyo, ukiangalia unagundua kuwa kuna tatizo la ushauri wa kisheria kuhusiana na utamaduni wa soka. Unabaini kuwa masuala ya haki yanaangaliwa zaidi nje ya mfumo wa mpira wa miguu na ndio maana safari za kwenda ofisi za Shirikisho la Soka (TFF) haziishi. Pengine pia kuna matumaini ya sakata hilo kuamuliwa kwa busara zaidi ya zile zilizo katika kanuni za soka.

Wakati nikifuatilia sakata hilo kwa makini, ndipo nikakutana na taarifa za TFF kwamba mtu mmoja tu amefaulu mtihani wa uwakala wa wachezaji wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa). Nikajiuliza, hivi bado tu hili somo halijaeleweka?

Kwangu si mara ya kwanza kusikia habari hizo. Mara kadhaa hawa jamaa wanaojitokeza kufanya mitihani ya uwakala wa wachezaji au mechi, hufanya vibaya sana na wakati mwingine hakuna hata mmoja anayefaulu.

Ni mitihani inayohitaji ufahamu mkubwa wa uendeshaji wa shughuli za mpira na sheria zake na hivyo umekuwa ni mzigo mzito kwa Watanzania wanaotaka kuingia kwenye sekta hiyo. Tangu Watanzania waanze kujitokeza kufanya mitihani hiyo, ni wachache sana na pengine hawazidi hata kumi ambao wamewahi kufaulu. Katika mazingira hayo, unategemea nini katika sakata la Fei Toto?

Unapoona wachezaji wetu wanashindwa kupata timu huko nje, huoni hili kundi linalojihusisha na wachezaji linakuwa sehemu kubwa ya vikwazo kwa kukosa ufahamu mkubwa wa masuala ya sheria zinazosimamia mambo hayo?

Binafsi nilichoka baada ya taarifa hiyo kwa kuwa nilijua hali imeshaanza kubadilika tangu enzi zile walipofeli wote waliofanya mtihani. Na kama hali bado ni hiyo, wachezaji wenye sakata kama la Fei Toto na wengine, watahangaika sana.

Mawakala ni nguzo muhimu sana kwa wachezaji na maslahi yao. Kama hawaelewi mambo ya msingi ambayo Fifa huyauliza kwenye mitihani yao, basi tunakosa kitu muhimu sana kwenye soka letu.

Columnist: Mwanaspoti