Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa hili lililotokea kwa Mkapa, tujiangalie

Uwanja Wa Benjamin Mkapa Stadium Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam

Sat, 1 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki moja iliyopita katika safu hii niliandika jinsi utunzaji wa Uwanja wa taifa wa Benjamin Mkapa ulivyo kielelezo cha utamaduni wa utunzaji wa mali zetu hasa viwanja.

Nilieleza kushtushwa na Uganda kulazimika kutumia uwanja wa Suez ulioko Ismailia Misri kama uwanja wa nyumbani dhidi ya jirani yake Tanzania.Kwenye makala hiyo nilitoa tahadhari kwamba yanayowakuta waganda nasi yanaweza kutukuta iwapo hatutaweka nidhamu katika utunzaji wa uwanja huu na viwanja vingine vilivyopo na vitakavyojengwa.

Juzi katika mchezo wa kufuzu mashindano ya mataifa ya Afrika (Afcon) kati ya Taifa Stars na Uganda mchezo ulilazimika kusimama kwa takribani dakika 38 kupisha marekebisho ya taa baada ya mwanga wa taa kupungua.

Tukio hilo lililoshuhudiwa na makumi elfu ya watanzania wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa lilikuwa si tu ni aibu kwa Taifa, bali ni kama onyo kwamba tunakoelekea si pazuri. Mchezo huo uliosimama tangu dakika ya 37 ya mchezo ulilazimika kuendelea baada ya zaidi ya nusu saa kupita kisha kumalizia dakika 8 zilizobaki kwenda mapumziko.

Hadi sasa wahusika hawajaomba radhi kwa umma wa watazamaji waliopata usumbufu kwa tukio hilo wala hawajaeleza nini kilitokea mpaka tukapatwa na aibu hiyo. Bila kujali kama tukio hilo lilikuwa la bahati mbaya kwa vile hutokea hata kwenye viwanja vingine.

Bila kujali ni hujuma, uzembe, ajali au mapenzi ya Mungu, ni muhimu kwa wahusika kuelewa kwamba hiyo ni kadi ya njano kwamba kitakachofuata hatutakuwa tofauti na Uganda, inabidi tujitathmini sana na tusione jambo hili lililotokea kama ishu ya kawaida ambayo ni nyepesi. Tulifikirie kwa mapana yake. Vinginevyo tutawakaribisha wageni kwenye sebule za majirani kama wanavyofanya majirani zetu kama Uganda na Sudani Kusini.

Nimebahatika kuona mawasiliano ya Februari kutoka Shirikisho la Soka Africa (CAF) kwenda Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambamo CAF wanaeleza kushtushwa na hali ya uwanja huo wa Benjamin Mkapa ambao umeelezwa kuwa ni uwanja wa kisasa uliokosa matunzo au unaohitaji kufungwa hili kufanyiwa ukarabati.

Upungufu mwingi umeelezwa kuanzia kwenye sehemu ya kuchezea,sehemu za kukaa mashabiki na hata vyumba vya ndani.Barua hiyo inaendelea kuelekeza kuwa uwanja huo usitumike kwa mashindano ya klabu ya Afrika baada ya michezo ya makundi.

Bila shaka wahusika watakuwa wanachukua hatua. Tujaribu kufikiria na madhara yatakayotokea kwenye nyanja mbalimbali kama itatokea siku kutokana na kilichotokea juzi Uwanja wetu ukakumbana na adhabu yoyote kutoka kwa mamlaka za soka za Afrika au Duniani.

Mdharau mwiba mguu huota tende. Tukio la kukosa mwanga katika mchezo wa juzi tusilifumbie macho eti kwa sababu limepita bali litusukume zaidi na zaidi kuchukua hatua si tu za ukarabati wa haraka wa miundombinu yetu bali kuongeza nidhamu katika kutunza miundombinu ya michezo ya umma na hata ya binafsi.

Columnist: Mwanaspoti