Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa hili la makombe TFF/TPLB wajipange!

ASFC 2022 Kombe la Azam Sports Federation

Thu, 7 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ushaliona taji la Ligi Kuu ya Ujerumani? Kama ni mfuatiliaji wa ligi ni wazi utabaini, bingwa hunyakua taji lililo kama sahani. Katika Ligi Kuu England je? Vipi La Liga au Ligi ya Mabingwa Ulaya nako mataji yake si mnayafahamu kwa urahisi?

Vipi katika Ligi Kuu Bara, umefuatilia kwa misimu 10 iliyopita? Umeona mabingwa wanavyokabidhiwa makombe tofauti? Hata kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) nalo kila msimu huwa na kombe jipya. Hakuna kombe linalotambulisha michuano hiyo, sawa tu na kwenye Ngao ya Jamii. Fuatilia mechi za Ngao za Jamii kwa misimu 10 iliyopita ndio utajua Mwanaspoti tunamaanisha nini. Kila msimu inatolewa taji jipya.

Yaani inachanganya, hujui tatizo ni nini, hata wasimamizi wa michuano hiyo wameshindwa kutengeneza mataji yanayotambulisha kwa urahisi michuano husika.

Kule England, taji la Ligi Kuu halifanani na lile la Kombe la Ligi ama Kombe la FA. Ni sawa tu kwenye michuano kama hiyo katika nchi za Ujerumani, Hispania, Ufaransa na hata Italia.

TATIZO LILIANZA HAPA

Mara baada ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na Wadhamini Wakuu wa Ligi Kuu, Benki ya NBC kutambulisha kombe alilopewa bingwa wa msimu huu ambaye ni Yanga, mijadala mbalimbali iliibuka kwenye mitandao ya kijamii.

Mijadala hiyo iliibuka kutokana na muonekanao wa kombe hilo walilokabidhiwa Yanga baada ya kumaliza kibabe Ligi Kuu msimu wa 2021-2022, huku wengine wakienda mbali zaidi kwa kulitengenezea vibonzo vya utani na kulifananisha na jagi la kusagia juisi. Wapo pia waliolitania eti ni mashine ya kusaga.

Kombe hilo jipya walilobeba Yanga msimu huu ni tofauti na walilopewa Simba msimu uliopita ingawa ni kwamba wadhamini wa ligi ni tofauti.

Sio kombe la Ligi Kuu tu kwani hata kombe la FA na hata Ngao ya Jamii yote yamekuwa tofauti kila msimu ingawa kwa misimu miwili ya karibuni 2019/2020 na 2020/2021, wadhamini wa FA, Azam Media wamejitahidi kuja na kombe la aina moja kwenye ASFC.

Mfano Ngao ya Jamii imekuwa na muundo tofauti kila mwaka kwani kuna wakati ilitolewa ya kioo na wakati mwingine ya mbao hivyo kuwachanganya wadau wa soka ambao wanahoji kwa nini kusiwe na aina moja ya ngao hiyo kila mwaka.

Pia kombe la Ligi Kuu Bara nalo limekuwa likibadilika badilika kila mwaka hata lile kombe walilokabidhiwa Simba msimu uliopita ni tofauti na walilopewa Yanga msimu huu.

Licha ya kwamba wadhamini wa ligi wamekuwa wakibadilika badilika lakini hiyo imetajwa kuwa sio sababu ya kufanya makombe ya ubingwa kubadilika kimuonekano na wengi kushauri liwe la aina moja kama ilivyo kwa ligi mbalimbali duniani ikiwemo Ligi Kuu ya England na lipambwe kwa rangi ya jezi za bingwa husika wa wakati huo.

Katika Ligi Kuu ya England kombe la ubingwa limekuwa la aina moja kwa muda mrefu licha ya kwamba kulikuwa na mabadiliko ya wadhamini.

Pia hata makombe ya FA na Ngao ya Jamii ya nchini humo nayo yamekuwa yaleyale yanayotolewa kwa mabingwa kila msimu hivyo kuwa rahisi kwa mashabiki wa soka duniani kutambua kuwa hili ni kombe la mashindano fulani.

Sio kwenye ligi ya England tu, pia hata kwenye ligi nyingine kubwa kama La Liga ya Hispania, Bundesiliga ya Ujerumani na Ligi ya Mabingwa Ulaya (Uefa) huwa kuna kombe la aina moja linalotambulisha michuano hiyo.

Kuna mfano mwingine wa Kombe la Ligi nchini Engaland ambalo kwa sas linajulikana kama Carabao Cup kutokana na kudhaminiwa na kampuni hiyo.

Kombe hilo la Ligi lilikuwa la miundo mitatu, iliyoundwa na kutengenezwa na Mappin & Webb na lina uzani wa kilo 2.976 na kipimo cha sm 27 kwa sm 20.5 ambalo lilianza kutumika katika mashindano ya mwaka 1980/ 81.

Mwaka 1981 hadi 1986 kampuni ya Marketing Board walidhamini mashindano hayo na hivyo kuamua kutengeneza aina nyingine kombe la ubingwa kama ilivyokuwa mwaka 1987 hadi 1990 ambapo Littlewoods iliingia kudhamini mashindano hayo na kuamua kutengeneza kombe lao wenyewe.

Hata hivyo, ilipofika mwaka 1990 hadi sasa licha ya mashindano hayo kudhaminiwa na wadhamini tofauti na lakini bingwa alikabidhiwa aina moja ya kombe kama lile lililotolewa mwaka 1980/81.

ASFC BALAA

Tangu michuano ya FA irejee baada ya kusimama kwa miaka zaidi ya 10 kutoka mwaka 2003-2015, kombe la michuano hiyo limekuwa likitofautiana kila msimu.

Taji walilopewa Yanga wikiendi hii jijini Arusha, sio kama lile walilopewa watani wao Simba na wala halifanani kabisa na lile walilokabidhiwa wao walipotwaa kwa mara ya kwanza mwaka 2015-2016.

Taji lao lililokabidhiwa kwa nahodha wa Yanga enzi hizo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kutoka kwa Rais wa TFF kipindi hicho, Jamal Malinzi ni tofauti na lile walilopewa Simba waliotwaa msimu uliofuata yaani 2016-2017 na pia ni tofauti na lile la Mtibwa Sugar iliyobeba jijini Arusha.

Hata taji walilotwaa Azam kwa kuicharaza Lipuli, mjini Lindi msimu wa 2018-2019 halikufanana na la Mtibwa Sugar na pia lilitofautiana na yale mawili iliyobeba Simba mara mbili mfululizo kabla ya Yanga kulitwaa safari hii kwa kuifunga Coastal Union kwa penalti 4-1.

Hii ni tofauti na mataji ya FA iliyochukua Man United, Chelsea, Arsenal, Liverpool ama Man City pale England, kwani muundo ni ule ule mfanano ni uleule kama ilivyo pia kwa Carabao Cup, kuonyesha kuna mahali wasimamizi wa soka la Tanzania na wadhamini wanakosea.

MPANGO WAJISHTUKIA

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia anasema wameanza kuboresha mchakato wa kuwa na utambulisho wa vikombe vyao.

“Tangu nimeingia madarakani hatujawahi kutoa ngao ya kioo, ngao inapaswa kuwa ya ngozi au mbao sana sana inakuwa ya fedha au shaba.

“Tunakwenda tunaboresha na kama kuna mdau anatoa wazo zuri tunalipokea, hakuna mtu asiyependa jambo zuri, hata kabla sijawa Rais wa Shirikisho, nilikuwa na mawazo mengi, mengine ndiyo nayatekeleza sasa,” alisema Karia aliyechaguliwa kwa muhula wa pili mwishoni mwa mwaka jana.

“Kwanini sikufanya wakati ule, sababu sikuwa na fursa, japo niliyawasilisha katika uongozi, hivyo tunapokea mawazo na yale mazuri tunayafanyia kazi, huku pia tukiendelea kuboresha, lengo ni kufanya hizi tuzo tunazozitoa kuwa bora zaidi.

“Kwenye FA tumeanza kuwa na kombe linaloitambulisha, kwenye Ligi msimu huu pia tumebadilisha lakini tunahitaji kuboresha tuzo zetu zote ziwe na ubora, kombe la Ligi litakuwa ni hili la msimu huu.”

Karia anasema watakuwa na utaratibu wa kutoa mfano wa kombe kwa mabingwa na lile halisi linarudi kama ambavyo Fifa wanafanya kwenye Kombe la Dunia.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo anasema kombe lililotolewa kwa bingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu Bara ndilo litakalotolewa pia kwa mabingwa wa misimu ijayo.

“Labda itokee mabadiliko mengine mbele ya safari, lakini kwa sasa kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara litakuwa ni hili lililotolewa msimu huu, hili ndilo litakuwa kombe letu halisi kwa mabingwa wote wajao,” anasema Kasongo.

WASIKIE WADAU

Mchambuzi wa soka na nyota wa zamani wa kimataifa, Ally Mayay anasema kuwa kombe linaloitambulisha ligi linaongeza thamani ya ligi au mashindano husika.

“Ile ni brand, inaitambulisha Ligi na kuipa thamani yake, kila mmoja anakuwa anafahamu kombe halisi la Ligi yetu, FA na hata Ngao ya Jamii ni hili,” anasema.

Anasema utaratibu wa kuwa na kombe la aina moja kwenye Ligi ya Tanzania ni kitu ambacho miaka ya nyuma hakikuwepo, lakini kwa nchi zilizoendelea huo ndiyo taratibu wao.

“Inajulikana kombe la ligi fulani ni hili, msimu huu Bodi ya Ligi imefanya jambo kubwa kwa kutambulisha kombe la Ligi na ndivyo nchi zilizoendelea kwenye soka zimefanya miaka mingi.

“Japo kombe letu lina utani wa hapa na pale msimu huu, lakini kila mmoja anafahamu shepu ya kombe la Ligi Kuu Tanzania bara ni hili,” anasema Mayay.

Kipa wa zamani wa Simba, Moses Mkandawile anasema TFF kuwa na utambulisho maalumu wa makombe yao ni jambo la maendeleo akitolea mfano Ligi mbalimbali duniani ambazo zimekuwa na makombe yanayoitambulisha miaka yote.

“Japo tumechelewa, lakini si vibaya kuanza sasa utaratibu huo, hii itaipa thamani ligi yetu na wadau kufahamu kombe halisi la ligi yetu,” anasema.

Columnist: Mwanaspoti