Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa hili la Lissu, Profesa Mbele unatupotosha

1060ba071c6d8ee605d79551a5ba9f42.png Kwa hili la Lissu, Profesa Mbele unatupotosha

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

NIMESOMA andiko la Profesa Joseph Mbele lililochapishwa hivi karibuni kwenye mtandao wa Jamii Forum akihalilisha matamshi ya Tundu Lissu juu ya kuichafua nchi ya Tanzania katika mijadala mbalimbali ughaibuni.

Lakini pia nikasoma andiko la Mwandishi mahiri ambaye pia ni Mhariri wa Makala wa gazeti hili, Hamisi Kibari. Andiko la Profesa Mbele lilikuwa na kichwa cha habari kisemacho: Tundu Lissu haichafui nchi, kumsema Spika wa Bunge na Serikali siyo kuichafua nchi.

Hata Nyerere alisema CCM ni kansa. Katika makala ya Kibari, ambayo kupitia safu yake ya Tukubaliane Kutokubaliana, akaja na makala yenye kichwa kisemacho: Ukiisema serikali vibaya, unachafua nchi.

Nakubaliana na hoja za Kibari moja kwa moja bila kuathiri haki ya Profesa Mbele aliyo nayo kikatiba ya nchi ya Tanzania, ibara ya 18 inayosema:

Mosi: Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

Pili: Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

Profesa Mbele anaamini Lissu anachozungumza nje ya nchi kwenye mihadhara ya vyuo na majukwaa mengine ughaibuni ni sahihi kwani vyuoni kujenga hoja na kutofautiana ni moja ya uhai wa taaluma.

Kwa kuwa katiba inampa haki ya kutoa mawazo yake, yuko sahihi, lakini je yuko sawa kwa faida ya Watanzania? Profesa anasema: “Lakini kutofautiana mitazamo ndio utamaduni wa watu wanaofikiri. Ndio utamaduni wa watu walioelimika. Vyuo vikuu ni mahali ambapo tunatofautiana na kulumbana muda wote. Ni uhai wa vyuo vikuu. Ni uhai wa taaluma.

Tunawajibika sisi walimu kujenga tabia hiyo miongoni mwa wale tunaowafundisha.” Profesa Mbele anabainisha pia: “Mimi ninaufahamu vizuri utamaduni wa vyuo vikuu vya Marekani, kwa sababu nilisomea kule na ninafundisha kule. Nimeshatoa mihadhara katika vyuo vingi, sio Marekani tu bali sehemu mbali mbali za dunia.”

Maneno ya Profesa Mbele ya kuamini kwamba utamaduni wa vyuo vikuu ni kujenga hoja za kutofautiana, si tu kwangu yanapotosha dhana nzima ya kujenga hoja zenye mashiko na mustakabali wa nchi bali pia yanakera.

Nasema yanakera kwa kuwa vijana wa sasa wanaomaliza vyuo si Marekani tu hata hapa Tanzania wengi wao (si wote) hawajengwi na maprofesa kutoa hoja zenye kuleta tija bali kutoa malumbano ya hoja. Kama makala ya Kibari inavyoeleza, Profesa Mbele ameshindwa kabisa kufuatilia hoja za Lissu akiwa mwanasheria, mwanaharakati na baadaye mwanasiasa.

Kimsingi, hoja za Lissu anapokuwa kwenye mihadhara ya vyuo vikuu au majukwaa ya kisiasa na hata alipokuwa mbunge katika Bunge la Tanzania, haziendani na uhalisia si kwa yale yaliyotendeka, yanayoendelea kutendeka au yatakayotendeka kwa manufaa na mustakabali wa nchi na Watanzania kwa ujumla.

Kwa kuwa ni vigumu kurudia yote katika hoja alizojenga huko nyuma kama vile kutaka kukwamisha suala la makinikia ambalo limeleta tija kubwa kwa nchi, kuzuia ndege zisiweze kunuliliwa kwa faida ya Watanzania wa leo na vizaji vijavyo, nitaegemea katika mfano mmoja ili ubainishe hoja yangu.

Katika hili la makinikia Kibari anasema: “Alipoulizwa (Lissu) suala la Barrick kuingia makubaliano na Serikali ya Tanzania, alichojibu (Lissu) hakikuwa kweli. Mtu mwenye taarifa sahihi asingeweza kusema kuwa hakukuwahi kuwa na makubaliano yoyote baina ya serikali ya Tanzania na Barrick (isipokuwa dola milioni 300 ambazo nazo hazikulipwa).

Kibari aendelea kujenga hoja: “Wakati anajibu hayo, mtandao unaoheshimika sana wa Bloomberg unaokusanya na kusambaza habari na taarifa za uchumi, uwekezaji, mitaji na fedha, ulikuwa umetangaza kuwa serikali ya Tanzania na Barrick wako katika hatua za mwisho kusaini makubaliano.

Mpaka leo hajawahi kukiri upungufu!” Ikumbukwe Lissu aliporejea hapa nchini Julai 27, mwaka huu akitokea Ubelgiji, moja ya hoja aliyoona ina nguvu ni kubeza Mradi wa Umeme wa Mto Rufiji.

Lissu alinukuliwa akisema mradi huo unaendeshwa chini ya kapeti kwani serikali haisemi utatumia gharama kiasi gani na una faida gani kwa wananchi. Ikumbukwe kwamba maelezo ya mradi huo yalikuwa yakitolewa mara kwa mara na wataalamu wa Wizara ya Ujenzi lakini pia Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi pamoja na Rais John Magufuli mwenyewe kila alipopata nafasi kuzungumza na wananchi.

Kabla ya Lissu kubeza mradi huo, Rais Magufuli aliwahi kunukuliwa akisema: “Mradi huu umepigwa vita sana kwa hiyo sishangai kama mawazo haya ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere tangu mwaka 1970 leo ndiyo tunakuja kuweka saini zaidi ya miaka 40, nilijua matatizo waliyokuwa wanapambana nayo”.

Rais Magufuli hakuishia hapo, alitoa takwimu kuonesha faida lukuki za mradi kwa Watanzania akisema: “Nafahamu wapo wanaosema mradi huu utaharibu mazingira, hiyo si kweli hata kidogo ninavyojua mradi huu utasaidia kutunza mazingira. Kwanza ni kwa sababu umeme wa maji ni rafiki wa mazingira, pili eneo la kutekeleza mradi huu ni dogo ambalo ni asilimia 1.8 hadi 2 ya eneo zima la Selous.”

Akasema mradi utakapokamilika utazalisha umeme kwa miaka 60 na gharama za kuzalisha umeme wa maji ni ndogo kuliko zingine, gharama za kuuza pia itakuwa nafuu kwa hiyo ukikamilika umeme utashuka.

Akaongeza kwamba bei ya umeme kwa nchi yetu ni kubwa kuliko nchi zingine na kutoa mfano umeme hapa kwetu kwa uniti unauzwa Dola za Marekani senti 10.7 wakati Misri ni senti 4.6, Korea ya Kaskazini ni chini yasenti 8, China nayo ni hivyo hivyo chini ya senti 8.

Rais Magufuli pia alioanisha na matumizi ya mkaa ambao unamaliza misitu. Ni mengi ambayo yalifafanuliwa kuhusu faida za mradi huo na pia gharama za mradi mzima. Naye Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani akasema mradi huo ukikamilika utakuwa mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki kwa kuzalisha megawati 2,115.

Akasema bwawa linalofuata kwa kuzalisha umeme mwingi ni la Bujagari nchini Uganda, likitarajiwa kuzalisha megawati 300 tu. Lissu hakujushughulisha si kwa takwimu akiwa kama mwanasheria ambaye tunaamini ni lazima awe na rejea kabla ya kujenga hoja na huyo huyo akitaka mataifa yamwamini akisema hakuna taarifa zinaoweza kuonesha kwamba mradi huo utakuwa na faida kwa Watanzania badala ya kuharibu mazingira.

Lakini kama nilivyosema awali, Profesa Mbele ahangaiki na nini kinachoweza kutokea kwa matamshi ya kuipaka nchi matope. Anaamini katika utamaduni wa watu walioelimika.

“Vyuo vikuu ni mahali ambapo tunatofautiana na kulumbana muda wote”. Kwake yeye, nchi haiguswi ukimsema vibaya Rais wake, miradi anayoisimamia na matumizi ya fedha katika kujenga miundombinu na kukarabari barabara, bandari na meli, kununua ndege, kutoa elimu bila malipo, kujenga zahanati, kununua dawa za hospitali na mengine lukuki ambayo Rais Magufuli amelifanyia Taifa hili kwa kipindi kifupi.

Profesa anasema: Kuna haya madai kwamba Tundu Lissu anaichafua nchi. Binafsi, sijawahi kuona popote au siku yoyote ambapo Tundu Lissu ameichafua nchi. Anazilalamikia mamlaka za nchi, kama vile serikali na Bunge.

Lakini serikali si nchi. Bunge si nchi. Anapomshutumu Spika, haichafui Tanzania. Spika si Tanzania. Hizo ndizo hoja za Profesa Mbele kwa jinsi anavyoyachukulia matamshi ya Lissu nje ya nchi na haoni madhara yoyote kwani haamini kama anaisema nchi vibaya.

Nimesema nazikubali hoja za Kibari moja kwa moja anayesema kwamba ukiisema serikali vibaya, unachafua nchi na kuhoji katika makala yake: “Je, ni kweli mtu anapozisema vibaya mamlaka za nchi haisemi nchi? Sijui wewe unayesoma hapa lakini mimi, mtu anaponiambia mamlaka za nchi fulani zilizowekwa na wananchi, tuseme Marekani, zinafanya hiki na kile, kwangu haiji picha ya ardhi, mipaka wala milima ya Marekani bali nchi ya Marekani.: Anaongeza: “Mimi sielewi Profesa anataka mtu anapoichafua nchi aseme nini ingawa katika andiko lake kwenye mtandao kuna waliomuunga mkono!”

Hata mimi, sijawahi kumwelewa Lissu kwa kuwa kwangu mimi ni mtu anayejali masilahi binafsi na yuko tayari kuiuza nchi kwa wageni ilimradi apate fedha. Tatizo ninaloliona mimi ni jinsi maprofesa wengi (si wote) wanavyojaribu kuwajenga vijana kujenga hoja za malumbano bila kuwapa uelewa wa ujenzi wa hoja zenye mantiki, nguvu na zenye tija kwake na kwa jamii inayomzunguka kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.

Columnist: habarileo.co.tz