Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa Mkapa, tulishasahau maelekezo muhimu ya CAF

Mkapa Stadium Lupaso Mkapa Kwa Mkapa, tulishasahau maelekezo muhimu ya CAF

Tue, 7 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Uwamja wa Benjamin Mkapa utazuiwa kwa muda ili wamiliki wapate nafasi ya kuboresha sehemu ya kuchezea ambayo hivi sasa inasikitisha kila unapoangalia mechi zinazochezwa uwanjani hapo.

Ni kama vile wapiga picha za video waliamua kuonyesha hali inavyozidi kuwa mbaya uwanjani hapo kutokana na kuonyesha kila mara sehemu zenye rangi ya brauni kwa kutumia kamera ya juu uwanjani.

Na baadhi ya waandishi walipoona hali hiyo mbaya hawakusita kupaza sauti, ingawa watendaji wa wizara waliibuka na kutoa majibu mepesi, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limesaidia kuturudisha kwenye mstari ili tulinde na kutunza vya kwetu.

Uwanja huo ni moja ya viwanja vikubwa barani Afrika vyenye ubora na hadhi ya Olimpiki, kwa kuwa vinaweza kutumiwa kwa zaidi ya mchezo mmoja - mbali na soka ni riadha, kurusha tufe, kurusha mkuki, kuruka chini, kuruka juu na miruko mitatu.

Michezo mingine imekuwa haitumii sana uwanja huo kwa kuwa baadhi ni kama haipo au inapumulia mashine na hivyo mchezo wa soka kutawala kila wiki.

Mechi za Ligi Kuu ya soka ndizo zimetawala matumizi ya uwanja huo, lakini mapato yatokanayo na mechi hizo hayakidhi gharama za usafi na matengenezo ya baadhi ya sehemu yatakayohitajika baada ya uwanja huo kutumiwa.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa gharama za uwanja hutolewa kwa asilimia ya mapato ya mlangoni yaliyopatikana siku hiyo. Kama mechi haikuvuta watu wengi, basi mapato yatakuwa ni madogo na hivyo asilimia itakayotengwa kwa ajili ya usafi na baadhi ya matengenezo, itakuwa ni ndogo.

Ni dhahiri basi kwamba kwa mfumo huo wa mapato yanayokwenda kwa mmiliki kutolewa kwa asilimia, itakuwa ngumu kuutunza vizuri uwanja huo ili uendelee kuwa katika ubora unaokusudiwa.

Hivi sasa kila bada ya wiki takriban mbili una mechi mbili za michuano ya kimataifa kutokana na klabu za Simba na Yanga kufikia hatua za juu za michuano ya Afrika.

Bado una mechi za kimataifa za timu zetu za taifa, yaani Taifa Stars, Twiga Stars na timu za taifa za umri. Nazo zikichachamaa mashindanoni mechi zinakuwa nyingi zaidi.

Ni kweli mechi hizo zinaweza kuhamishiwa viwanja vingine kama Azam Complex, Uwanja wa Uhuru, CCM Kirumba, Mwanza au Sheikh Amri Abeid Arusha, lakini kuna gharama zinazoambatana na kuhamishia mechi huko au umuhimu kubadilika kadri timu hizo zinavyosonga mbele.

Kwa hiyo, kuna changamoto kubwa katika utunzaji wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao ni moja ya tuzo kubwa kwa nchi hii.

Haitakiwi majibu mepesi mepesi kutatua tatizo kubwa, bali kukaa chini na kujadili kwa kina nini kifanyike ili matumizi yasizidi uwezo wa utunzaji na hivyo hazina hiyo kuendelea kuwa haipungui.

Tunazungumzia sana mipango ya maendeleo lakini hatuzungumzii ujengaji na uboreshaji wa miundombinu ya michezo. Akili yetu ni kwamba serikali ndiyo yenye jukumu hilo na hivyo kazi ya wadau wa michezo imekuwa ni kuweka mikakati mingine ya maendeleo ya michezo yao au klabu zao.

Wiki mbili zilizopita Simba na Yanga ziliamua kufanya kampeni za kuhamasisha mashabiki kujazana kwenye uwanja huo wakati wa mechi zao za makundi za michuano ya CAF.

Ni kazi ambayo ilifanywa kama kwa dharura kwa sababu ya umuhimu wa mechi hizo nyumbani. Lakini si mkakati wa kudumu wa klabu hizo wala nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza.

Ushirikishwaji na ujumuishaji wa mashabiki katika shughuli mbalimbali (fans engagement), kitu ambacho ni muhimu katika michezo ya dunia ya sasa. Uhusishaji mashabiki katika shughuli za klabu kiasi kwamba wajisikie sehemu ya mechi, ni kitu ambacho kinafanywa sana na klabu kubwa duniani, hasa za barani Ulaya.

Ni mambo gani ambayo watendaji wa klabu wanatakiwa kuyafanya, ni jambo ambalo wanatakiwa kukuna vichwa kuyatafuta badala ya kudhani kuwa na maneno mengi ni kuvutia mashabiki na hivyo watavutika kwenda viwanjani. La hasha! Kuna mambo makubwa sana ndani ya dhana ya fans engagement. Watu wa habari wa Yanga na Simba walifanya fan engagement kabla ya mechi zao dhidi ya TP Mazembe na Raja Casablanca kwa kuwa fuata mashabiki nje ya uwanja, kitu ambacho ni muhimu sana.

Lakini hilo ni moja tu na halitakiwi kufanywa kwa dharura bali kuwa na mkakati wa muda mrefu ambao utaongeza mapenzi ya mashabiki kwa klabu zao wakiwa Dar es Salaam, mikoani na hata nje ya nchi.

Hao maofisa habari wanafanya hivyo kama sehemu ya kutangaza klabu, lakini watu wa masoko pia wana jukumu kubwa la kutekeleza majukumu yao kuhakikisha mechi zinavuta watu wengi pamoja na kampuni zinazotaka kuwekeza kwenye klabu zao.

Hivi sasa ukiangalia mabango yanayozunguka sehemu ya kuchezea mechi za Ligi Kuu, utaona yale ya kawaida tu - Azam, Tanzania Premier League Board, NBC, SportsPesa na M-Bet kama sijataja yote.

Hii maana yake ni kwamba watu wa masoko wa klabu zetu wanashindwa kuvutia wadhamini wa siku za mechi (match day sponsorship) na hivyo makabati ya fedha yanaendelea kuwa na kiwango kilekile kinachotumbukizwa na Mo Dewji, GSM, SportsPesa, M-Bet, NBC na Azam. Hakuna akili mpya si tu ya kupata wadhamini wapya, bali hata kujua fursa zinazotengenezwa na mechi zinazorushwa moja kwa moja.

Nimezungumzia haya yote kujaribu kuonyesha ni jinsi gani tunavyofanya mambo kwa mazoea kiasi kwamba hatuoni sehemu nyingine zaidi ya Uwanja wa Mkapa au kuililia serikali ifanye vitu ambavyo vinaweza kufanywa na wadau wengine wa michezo.

Ni mara chache sana viwanja hujengwa na serikali za nchi na hii hufanyika kisiasa zaidi ili kupunguza munkari wa wananchi kwa kuwapa burudani. Ndio maana serikali za nchi kama za mashariki, za Kiarabu ndizo ziko mstari wa mbele katika ujenzi wa viwanja.

Lakini katika nchi za kidemokrasia kama yetu, wadau wa michezo ndio huhusika zaidi katika kujenga viwanja. Mabenki, kampuni kubwa kama Allianz na pia klabu zenyewe.

Lakini ni lazima wadau hawa waone thamani ambayo itawalazimisha kujipiga mifukoni ili kushiriki katika ujenzi. Ni kwa kiasi gani klabu zetu au vyombo vyenyewe vinavyosimamia michezo vimeonyesha thamani hiyo kiasi cha kuvutia wawekezaji katika soka au michezo mingine? Kama hadi klabu kongwe za Simba na Yanga zinalazimika kuingia mtaani kusaka mashabiki, vipi kuhusu Singida United, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar au Namungo?

Ajabu ni kwamba hata klabu za Simba na Yanga zinapozungumzia mipango ya ujenzi wa viwanja zinakuwa zinatumia kama siasa. Simba walianzisha mchango wa ujenzi wa uwanja wao wa Bunju, lakini suala hilo huibuka na kutoweka kama mvuke. Yanga ndio wameshasahau kabisa. Lilianzishwa kama kampeni, uchaguzi umeisha, nalo limeisha.

Bado hatujaweka umakini katika miundombinu ya michezo. Ni kweli serikali itatujengea, lakini mkono wake hautaweza kufika kila sehemu. Ni lazima wadau wengine wa michezo waanze sasa kuweka suala la miundombinu kama ajenda katika kila jambo wanalotaka kulifanya. Yaani kila jambo liangaliwe kwamba litahusikaje na ujenzi wa miundombinu.

Tusisubiri kuwaahidi mashabiki ushindi na kudhani kuwa tumemaliza kila kitu pale ushindi unapopatikana. Ushindi unapopatikana unatakiwa uwe ndio mwanzo wa mikakati mikubwa zaidi ya kuboresha klabu na si kubweteka kwa kudhani ile presha imeisha.

Tusipotilia maanani suala hilo, basi ratiba za mashindano yetu zitatibuliwa kila mara na wamiliki wa viwanja na wadau wao kama CAF.

Columnist: Mwanaspoti