Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa Maguire, usirushe ngumi kwa mtu aliyepiga magoti

Rekodi: Bila Maguire Man U Hawatoboi Harry Maguire

Sat, 28 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jumatano ya Septemba 13 alfajiri niliwasha simu na kukuta meseji nyingi za kawaida na zile za WhatsApp. Kila mtu alikuwa ananikumbusha niandike kitu mtandaoni kuhusu kujifunga kwa Harry Maguire katika pambano la England dhidi ya Scotland. Sikufanya hivyo. Nilikaa kimya.

Wanajua namna nilivyokuwa namshambulia Maguire mitandaoni. Wanajua namna nilivyorusha vipande vingi vya video vikionyesha makosa ya kipuuzi ya Maguire. Hata hivyo sikufanya chochote baada ya Maguire kujifunga dhidi ya Scotland.

Sikuhitajika kufanya hivyo. Wanasema usiendelee kumrushia ngumi mtu aliyepiga magoti na kunyanyua mikono yake juu. Haifai. Kwangu mimi nikiwa kama shabiki wa Arsenal imetosha kumsema vibaya Maguire. Naangalia mitandaoni nakuta baadhi ya wachezaji wa zamani ambao kwa sasa ni wachambuzi wanaungana na hisia zangu.

Maguire ameponzwa na vitu vingi katika maisha yake Manchester United. Nisiwe mnafiki. Wakati akiwa na Hull City nilitamani kumuona akichezea Arsenal. Beki mrefu, mwenye nguvu na anayeweza kucheza mpira wa Kiingereza hasa. Niliwahi kumtamani. Akaangukia zake Leicester City kutengeneza Leicester mpya baada ya kile kizazi kilichowaletea ubingwa wa maajabu wa England kufika mwisho.

Na pale alifanya vyema. Tatizo lilianzia alipotua Manchester United. Kitu cha kwanza kilichomponza ni bei yake. Pauni 80 milioni. Wakati huohuo Virgil Van Dijik alikuwa ametoka Southampton kwenda Liverpool kwa Pauni 75 milioni. Van Dijik akawa beki bora Ulaya kando ya kina Sergio Ramos. Tukaanza kulinganisha bei ya Van Dijik na Maguire.

Ukweli ni kwamba Van Dijik alikuwa bora kwa mbali kulinganisha na Maguire. Kilichotuuma wengi wetu ni dau la mchezaji wa Kiingereza. Tunawachukia Waingereza na pesa zao. Tunajua hazina uhalisia. Mpaka leo mchezaji wa Kiingereza ambaye amenunuliwa kwa dau kubwa huwa tunataka akosee ili tuwashambulie Waingereza na dau lao.

Ilikuja kwanza kwa Jack Grealish aliponunuliwa kwa dau la Pauni 100 milioni na Manchester City kutoka Aston Villa. Msimu wake wa kwanza aliyumba tukaanza kuwasema Waingereza na bei zao. Bahati yake baada ya hapo alirudi katika ubora wake kiasi cha kuwapa City ubingwa wa Ulaya. Ndio maana tumerudisha mapanga yetu nyuma.

Hata huyu Declan Rice tulikuwa tunasubiri kutoa mapanga yetu baada ya Arsenal kulipa Pauni 105 milioni kumpata. Bahati nzuri kwa Rice ameendelea pale alipoishia. Ameingia katika kikosi cha kwanza moja kwa moja na tumerudisha visu vyetu katika ala. Maguire hakuweza kuipata bahati hii. Maisha yalimuendea kombo Old Trafford na kitu kibaya zaidi ni nafasi yake anayocheza.

Maguire anacheza nafasi ya ulinzi ambayo makosa yake ni rahisi kuonekana. Makosa yake yanazalisha mabao ya wapinzani. Bahati mbaya kwake alipoanza kuingia kwa mguu wa bahati mbaya wapinzani tukashikilia hapo hapo. Akapoteza uwezo wake wa kujiamini na kamwe hakuweza kurudisha uwezo wake huo.

Kiukweli aliwahi kuwa na uwezo huo. Ungemtazama Maguire wa Juni hadi Julai 2018 katika michuano ya Kombe la Dunia pale Russia ungejua kwamba United hawakufanya makosa kuipatia Leicester hizo noti kwa ajili ya kupata huduma yake. Tatizo aliingia na bahati mbaya Old Trafford kiasi kwamba kila alichogusa kiligeuka kuwa kinyesi.

Kitu kingine kilichomponza Maguire ni ukweli kwamba alikwenda katika timu ambayo ilikuwa katika anguko. Tangu aondoke Sir Alex Ferguson mwaka 2013 United haijawahi kuwa na timu imara.

Ni rahisi kung’amua makosa yake kwa sababu ni beki, lakini United imezika vipaji vya wachezaji lukuki pamoja na makocha tangu Ferguson aondoke.

Kina Angel Di Maria, Radamel Falcao, Paul Pogba na msururu wa mastaa wengi ambao waliingia United kwa mbwembwe wakaondoka wakiwa wameinamisha vichwa chini. Maguire angekwenda katika timu ambayo ipo kati si ajabu angekuwa na maisha mazuri. Wanasema dandia boti inayokwenda kasi ufike haraka.

Van Dijik alipata bahati hii. Alipokwenda Liverpool timu ilikuwa ya moto. Ilikuwa rahisi kwake kufanya vyema katika timu ambayo muda wote ilikuwa inakaa na mpira na kushambulia.

Leo Liverpool imepotea na hata Van Dijik ameanza kuonekana kuwa beki wa kawaida. Hata Trent Alexander alikuwa anabebwa zaidi na ubora wa Liverpool wakati ule ikishambulia muda wote. Upungufu wake katika ulinzi ulianza kuonekana baada ya Liverpool kupoteza kasi yake.

Maguire angekuwa katika vikosi vya Ferguson si ajabu angeonekana kuwa mchezaji mzuri. Ni wachezaji wangapi wa kawaida katika kikosi cha Sir Ferguson walionekana kuwa wazuri? Mfano ni Phil Neville. Hawa ndio wachezaji ambao timu ilikuwa inawabeba. Maguire hajawahi kubebwa na Manchester United. Aliingia katika nyakati ngumu.

Msimu uliopita alikaribia kuuzwa kwenda West Ham. Timu zilikubaliana ada ya uhamisho, lakini mwisho dili lilishindikana. Hatimaye alibaki United na ameendelea kupigania nafasi yake kupitia majeraha ya Lisandro Martinez. Ameanza kufanya vizuri na katikati ya wiki hii aliipatia Manchester United bao la ushindi dhidi ya FC Copenhagen. Nilifarijika.

Nilifarijika kwa sababu katika maisha yangu ya soka sijawahi kukumbuka kama nimewahi kumuona mchezaji aliyeandamwa kama Maguire. Ameandamwa na kila mtu. Ameandamwa na mashabiki wa timu pinzani, mashabiki wake, makocha wa zamani hadi wachambuzi. Ameandamwa na kila mtu.

Ukijaribu kujiweka katika nafsi yake unajua mateso makali anayopitia. Unajaribu kumfanya kuwa ni kaka yako unagundua kwamba kinachoendelea sio ubinadamu. Binafsi nitarudi kumuandama tena pale atakaporudi katika ubovu. Kwa sasa ni ngumu kuendelea kumpiga makonde mtu ambaye amekaa chini.

Siku moja ataandika kitabu cha maisha yake ya soka na kueleza hali ambayo anapitia hivi sasa. Ni hapo ndipo ambapo tutagundua mateso ambayo anapitia sasa hivi yeye na mke wake. Kuna walinzi wengi wanafanya makosa mengi ya kipuuzi kila siku, lakini hatuwaandami kwa sababu akili zetu tumezielekeza kwa Maguire.

Tunafurahia anguko lake kwa sababu ya bei yake ya Kiingereza. Lakini kama ni bei kubwa basi aliuzwa Eden Hazard kwenda Real Madrid akitokea Chelsea, lakini hakufanya lolote la maana na tumekaa kimya. Unajua kwa sababu gani? Kwanza sio Mwingereza, pili hachezei Manchester United.

Lakini vilevile akiwa na Madrid Hazard usingeweza kumuona katika makosa ambayo yaliifanya Madrid kufungwa. Hata hivyo kama Hazard angekuwa Mwingereza kisha akaenda Old Trafford nadhani tungefurahia anguko lake na la timu yake kwa ujumla. Hicho ndicho ambacho kinamponza Harry Maguire.

Sitaki kumtetea lakini mashambulizi dhidi yake yamekuwa mengi kiasi cha kumfanya aonekane kama paka aliyejibanza ukutani akirushiwa mawe na watoto wa shule.

Binafsi najitoa kwa muda katika mashambulizi haya. Sidhani kama Maguire ndiye beki mbovu zaidi kuwahi kutokea duniani.

Columnist: Mwanaspoti