Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kwa Fei Toto, Yanga walisahau kusoma alama za nyakati

Feisal Salum Winning Goal Kwa Fei Toto, Yanga walisahau kusoma alama za nyakati

Wed, 28 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Namna ambavyo Feisal Salum ‘Fei Toto’ alivyochafua hali ya hewa hakuna aliyetarajia. Ilianza kama mzaha hivi. Kulikuwa na minong’ono kwamba Azam walikuwa tayari kulipa kiasi cha fedha ambacho kingeweza kumuondoa Fei Yanga na kutua kwao.

Hatimaye Fei aliondoka nyumbani na kwenda benki kuweka kiasi cha Sh112 milioni katika akaunti ya Yanga. Ni kiasi ambacho kwa kufikiria kwa haraka haraka utajua tu kwamba atakuwa amepewa na watu wa Azam kwa mujibu wa minong’ono ilivyokuwa kabla ya tukio lenyewe.

Azam wamejikausha vilivyo. Kama vile hawahusiki. Katika hili hapa kuna namna ambavyo Azam hawajafanya sawa. Kwamba kuna uwezekano walimshawishi mchezaji kinyume cha taratibu. Wazungu huwa wanaita ‘tapping’. Hili litabainika pale Azam watakapomtangaza rasmi Fei kuwa mchezaji wao. Kwa sasa wamemuacha Fei apambane na timu yake.

Wanaweza kudai kwamba pesa sio zao. Lakini ni kweli akaunti ya Fei inaweza kuwa na pesa hizo? Naandika huku nacheka. Watu wa Takukuru wakimbana Fei aeleze pesa alikozitoa anaweza kujikuta anaingia matatani. Kiasi inachekesha.

Tukiachana na hilo Fei ametoa somo dogo kwa watu wa Yanga. Hatua aliyoichukua haikufikirika kwa sababu tumezoea kuwachukulia poa wachezaji wa kizawa. Ni wachache ambao wamekuwa na uthubutu kama wa Fei. Kwamba unacheza Yanga, unang’ara, Yanga yenyewe inang’ara, kila kitu kinaonekana kwenda sawa halafu ghafla unahama.

Mara nyingi wachezaji wetu wazawa huwa wanajisahau na ustaa wao. Wengi huwa hawapendi kusaka maisha mazuri nje, au kufanya kile ambacho Fei amekifanya. Haishangazi kuona kwamba watu wa Yanga wameshtuka na huenda wakatapatapa zaidi.

Mchezaji wa mwisho kufanya hivi alikuwa ni Mrisho Ngassa lakini hali haikuwa hivi. Wakati ule chini ya Mwenyekiti Imani Madega, Yanga walionekana kuchoka kiuchumi na wakamuuza Ngassa kihalali. Safari hii Yanga wana tajiri Ghalib Mohammed lakini mipango yao ya kiuchumi pia imekaa vizuri.

Imekuwaje pamoja na yote haya Fei amefanya alichofanya? Nadhani watu wa Yanga walisahau kusoma alama za nyakati. Katika siku za hivi karibuni kumeanza kuwa na mwanamko wa mashabiki kutoa shinikizo kwa wachezaji mastaa wanaong’aa klabuni kulipwa sawa na mastaa wa nje. Fei amekuwa akifanywa kama mfano.

Msimu uliopita na msimu huu Fei amekuwa wa moto. Watu wamekuwa wakihoji kwanini Aziz Ki alipwe mshahara mkubwa mara nne ya ule anaolipwa Fei? Kwanini mchezaji kama Jesus Moloko alipwe pesa nyingi kuliko Fei? Nadhani watu wa Yanga walikuwa wanapuuza hali hii lakini si ajabu Fei akawa amefungua boksi la Pandora.

Mchezaji kama Dickson Job naye anaweza kufuata mkumbo huu huu tu kama Yanga hawatakuwa makini. Wachezaji wazawa wameanza kuwa na akili za mashabiki. Pale Simba itafika mahali Mohammed Hussein Tshabalala atapima mchango wake klabuni na kutaka kulipwa kama anavyolipwa Henock Inonga. Viongozi wetu wajiandae na alama hizi za nyakati.

Tukiachana na hilo ni wazi kwamba pia viongozi wa Yanga hawakusoma alama za nyakati kuhusu kile ambacho kimepaniwa na viongozi wa Azam. Mara zote watu wa Simba na Yanga wamekuwa wakifanyiana umafia. Yanga hawakuona umafia huu kutoka kwa Azam. Hawakusoma alama za nyakati.

Mwanzoni mwa msimu watu wa Azam walipanda dau kubwa kwa Aishi Manula. Simba nusura liwatokee puani lakini walipambana kumbakisha Aishi. Yanga hawakusoma alama za nyakati kwamba jambo hili linaweza kuwafikia. Hawakujiandaa. Walipaswa kujua kwamba linaweza kutokea kwao.

Kwa yote haya mawili Yanga walipaswa kuwa makini. Walipaswa kuwa makini katika suala la wachezaji mastaa wazawa kuanza kuwa na msukumo wa kulipwa kama wageni. Na walipaswa kuwa makini baada ya Aishi kunusurika kurudi zake Azam. Yanga walipaswa kumuongezea mkataba na mshahara Fei.

Kwa mfano, pale Arsenal kuna mchezaji anaitwa Gabriel Martinelli. Bado ana mkataba wa miaka miwili klabuni lakini Arsenal wameamua kumuongezea mkataba na mshahara. Kwanini? Kwa sababu kuna wakubwa wengine watamuahidi mshahara mkubwa kwa mujibu wa mkataba wake wa sasa.

Pia ni tahadhari kwao kwamba huenda muda si mrefu Martinelli na wasaidizi wake watapima mchango wake klabuni na kugundua kwamba analipwa pesa kiduchu kuliko baadhi ya mastaa ambao hawana mchango mkubwa kama yeye. Kwa wenzetu sio lazima usubiri mkataba wa mchezaji uishe au ukaribie mwisho ndio umpe mkataba mwingine na mshahara mwingine.

Na hapo hapo kitu kingine ambacho Yanga walijisahau katika hili ni namna ambavyo walishindwa kugundua kushuka haraka kwa thamani ya shilingi yetu. Wakati ule wanampa Fei Shilingi 112 milioni ilikuwa pesa nyingi na hawakuona kama kuna mtu ambaye angeweza kurudisha katika akaunti yao. Lakini kwa sasa hiyo pesa imegeuka kuwa ya kawaida tu.

Sitaki kujua nani yupo sahihi kati ya Yanga au Fei lakini kuna somo ambalo tunalipata katika mkasa mzima. Baada ya kila kinachotokea nadhani kutaanza kuwa na mabadiliko makubwa kuhusu mtazamo wa klabu dhidi ya wachezajj wazawa. Lakini pia Fei atakuwa amewaamsha wachezaji wengine wazawa ambao ni tegemeo pale katika klabu zao.

Nadhani hata Azam nao wakae mkao wa kuliwa. Kuna akina Ayoub Lyanga ambao wanaupiga mpira mwingi kuliko wageni nao watataka kulipwa sawa na kina Prince

Columnist: Mwanaspoti