Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kutokana na haya nitaendelea kumuunga mkono Magufuli

E12ba7c9566c39fac06fbdc2758fbf1c Kutokana na haya nitaendelea kumuunga mkono Magufuli

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

“TANU ina vita vya kulitoa Taifa letu katika hali ya unyonge na kulitia katika hali ya nguvu; vita vya kuwafanya wananchi wa Tanzania (na wananchi wa Afrika) watoke katika hali ya dhiki na kuwa katika hali ya neema.

Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na tusipuuzwe tena.”

Haya ni sehemu ya maandiko yaliyo ndani ya Azimio la Arusha. Azimio ambalo lilikuwa limetupiliwa mbali sana kwa muda mrefu tangu lianzishwe.

Miaka zaidi ya hamsini tangu kuanzishwa kwa azimio hilo kumetokea kiongozi wa nchi ambaye anaonesha mapenzi ya kurejesha nchi kule ambako tulionekana kupakimbia.

Katika vipindi tofauti Rais wa awamu ya tano, John Magufuli amekaririwa akiyarudia maneno haya, hata kama si kwa mpangilio huo hapo juu, huku akiwasisitiza watanzania kufanya kazi kwa kujituma pasipo kujali dini wala kabila kwa maslahi mapana ya taifa letu.

Sambamba na hayo amekaririwa akiwafariji watanzania kwa kuwaonesha utajiri nchi yetu ilionao.

Maneno haya ya kuwatia moyo watanzania yamezidi kuhamasisha uwajibikaji kwa Watanzania hususani wanaojitambua.

Kimsingi watanzania sasa wanaonekana kumuelewa sana. Nahisi hii inajibu swali la Baba wa Taifa aliposema “Tunataka mtu anayetaka kuwa Rais wetu ajiulize anataka kuifanyia nini nchi yetu na siyo nchi yetu itamfanyia nini?”

Pia aliwahi kusema Ikulu ni mzigo na mtu safi kabisa kabisa hapikimbilii. Bila shaka kila mtu mwenye akili iliotulizana, anaona namna Magufuli anavyolibeba kwa umahiri mkubwa zigo hili.

Wote tunakumbuka ni kwa kiasi gani alibezwa mwanzoni wakati anaanza urais, wengine walidiriki kusema ni nguvu za soda hasa pale alipokuwa akifanya ziara za kushtukiza kwenye mawizara na taasisi mbalimbali.

Baadhi ya wanasiasa walimuona kama kiongozi anayeweweseka pasipokujua anachokifanya. Kudumu kwa msimamo wake katika utendaji umemfanya ajizolee umaarufu mkubwa, siyo kwa Tanzania pekee bali dunia nzima.

Mara nyingi nabii hakubaliki nyumbani kwake, lakini kwa utendaji huu wa kulinda rasilimali za taifa, kuwajibisha mtu anapokwenda kinyume na maelekezo yanayolenga kuwanufaisha watanzania, kupigania na kujenga upya heshima ya nchi, kuwakumbusha kila mmoja utendaji uliotukuka, ni nani atampenda?

Kuna waliofikiri kwamba nchi itaendelea kwa Rais kusafiri nje ya nchi mara nyingi, lakini tumeshuhudia kipindi chote cha utawala wake alivyosisitiza kwamba hakuwa Rais ili asafiri bali kuwatumikia wananchi na akiongeza jitihada zake katika kutimiza majukumu yake pasipo kujali maneno ya wasioitakia nchi yetu yaliyo mema

Kwa nyakati tofauti baba wa taifa alisisitiza utunzaji wa maliasili kwa ajili ya vizazi vijavyo ambavyo ndio sisi tuliopo sasa na wajao. Pamoja na kauli hiyo ya Baba wa Taifa, maliasili zetu ziliwanufaisha walio wachache huku wananchi walio wengi wakizidi kunyanyasika ndani ya nchi yao.

Dhana yake ya kutamani madini yachakatwe hapa hapa nchini inazidi kutoa matumaini kwa watanzania walio wengi kwa kuwa sasa kitakachotoka nchini ni zao la mwisho la maliasili zetu.

Kuchakata madini hapa nchini na kuruhusu kuuza vitu vinavyotokana na madini hayo kutazidi kuongeza kipato kwa mtanzania na kupajua wigo wa ajira.

Japokuwa ni wazi kwamba tukifikia hapo Rais Magufuli atazidi kuchukiwa na wanaonufaika na hali ya sasa wakuwemo mabeberu na vibara wao wa ndani, lakini umma mkubwa wa Watanzania waliompigia kura watazidi kumuunga mkono.

Hadi leo najiuliza wale wapinzani waliokimbilia ughaibuni ati wametishiwa uhai wao walikuwa wanawaza nini? Ni kweli walikimbia kwa hofu ya uhai wao au kwa hofu ya kushindwa kutekeleza maelekezo ya mabeberu waliokuwa wamewatuma?

Kimsingi kama walikuwa na nia njema na watanzania na maslahi yetu sote mbona mara nyingi walibeza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ilikuwa ikitekelezwa na serikali ya awamu ya tano?

Sijawasikia lakini nahisi huko waliko wamenuna sana kwa hatua ya Rais Magufuli kwa kurejesha somo la Historia lenye nia ya kukuza uzalendo baina ya watanzania vijana ambao ndiyo wengi zaidi na anapigania maslahi yao ya sasa na ya baadaye.

Bila kurejesha somo la Historia, vijana watajua wapi kuhusu Azimio la Arusha lililokuwa limesheheni mtazamo kuntu kama maneno niliyoanza nayo makala haya?

Kimsingi, Azimio la Arusha lilibainisha njia kuu za Uchumi kuwa ni ardhi, misitu, madini, maji, mafuta na nguvu za umeme; njia za habari, njia za usafirishaji; mabenki, na bima; biashara na nchi za kigeni na biashara za jumla.

Nyingine ni viwanda vya chuma, mashini, silaha, magari, simenti, mbolea; nguo, na kiwanda chochote kikubwa ambacho kinategemewa na sehemu kubwa ya watu katika kupata riziki zao au kinachotegemewa na viwanda vingine.

Njia kuu za uchumi pia zinahusisha mashamba makubwa na hasa yale yanayotoa mazao ya lazima katika viwanda vikubwa.

Lakini katika haya yote serikali hutegemea kodi ili ifanikiwe katika mambo yake, hakuna nchi hata moja duniani yenye kutoa fedha zake bure bila masharti kwa nchi masikini.

Kwanza, hatuwezi kuzipata. Japo inawezekana zipo nchi ambazo zaweza na zapenda kutusaidia. Lakini hakuna nchi hata moja duniani ambayo iko tayari kutupa misaada au mikopo au kuja kujenga viwanda katika nchi yetu bila lengo la kutimiza shabaha zake za maendeleo na kunufaika na rasilimali zetu.

Nchi zenye dhiki ni nyingi sana duniani. Na hata kama nchi zote zenye neema zingekubali kuzisaidia nchi zenye dhiki, bado ingekuwa msaada huo hautoshi.

Lakini nchi zenye neema hazitakubali. Hata katika nchi ile ile, matajiri huwa hawatoi fedha zao kwa hiari ili zisaidie serikali kuondoa dhiki. Njia ya kuzipata fedha za matajiri ili zisaidie umma ni kuwatoza kodi wakipenda wasipende.

Katika kutambua haya, Baba wa Taifa alisisitiza watanzania kufanya kazi kwa maendeleo yao wenyewe na kwamba tusitarajie kwamba atakuja mtu kutoka nje kutusaidia katika naendeleo yetu hata siku moja.

Jambo hilo pia limesisitizwa sasa na Magufuli, yaani umuhimu wa kupiga kazi na kutafuta maendeleo yetu kwa vile hatuna mjomba nje wa atakayetuletea maendeleo tunayoyataka.

Katika jitihada zake amekumbwa na changamoto kadha wa kadha dhidi ya wakwepa kodi na wala rushwa ambao walimuandika na kumsema vibaya kila mara.

Msimamo wake wa kuendelea kuwatumikia watanzania pasipo kujali vitisho vya mataifa makubwa na matajiri wakubwa kunanifanya nizidi kumuunga mkono bila aibu yoyote na kumtaja kama Rais wangu kila kona. Ni wito wangu kwa watanzania wenzangu wote kukumbuka maneno ya hayati Baba wa Taifa aliposema “Tutaijenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe. Akipatikana mtu wa kutusaidia tutashukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya watanzania wote, ni kazi ya watanzania wenyewe. Si kazi ya mtu mwingine”.

Kwa kufanya anayofanya Magufuli historia itatusoma kama awamu iliosaidia kuleta maendeleo endelevu kwa watanzania wote wa sasa na kizazi kijacho.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni +255712-246-001: [email protected]

Columnist: habarileo.co.tz