Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kutoka Ronaldo de Lima, zidane hadi Arda Guler

Zudane Pic Zinedine Zidane "Zizzou"

Sun, 16 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jinsi mwanadamu alivyo kiumbe mnafiki. Mwanzoni mwa miaka ya 2000. Kama Ilker Casillas angeruhusu bao katika lango, katika uwanja wowote wa Ligi kuu ya Hispania, iwe Santiago Bernabeu au Vicente Calderon au popote pale, kuna watu kamera zingewamulika.

Angemulikwa David Beckham. Kisha angemulikwa Luis Figo, halafu Zinedine Zidane, kisha Ronaldo de Lima, halafu Raul Gonzalenz. Kamera pia isingemkosa Roberto Carlos. Unafiki mtupu. Kwamba pamoja na kuwa mna timu ya namna hii lakini bado mnafungwa.

Nyakati zinakwenda wapi? wakati ule mtu mmoja jeuri mwenye pesa zake, Florentino Perez aliamua kukusanya wachezaji wenye majina makubwa zaidi duniani akawaweka Santiago Bernabeu. Mradi huu uliitwa Galacticos.

Nimeukumbuka mradi huu majuzi. Nilikuwa nasoma mahala namna ambavyo Real Madrid kwa mbwembwe kabisa walivyompokea kinda mahiri wa Kituruki, Arda Guler kutoka Fenerbahce. Wamejaribu kulipa hela nyingi kwa kinda wa umri wake. Ana miaka 18.

Kabla yapo Real Madrid wamelipa pesa nyingi kwa staa wa kimataifa wa England, Jude Bellingham ambaye wamemnunua kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa dau la pauni 88 milioni. Sio pesa nyingi kama akina De Lima wangekuwa wananunuliwa leo. Nadhani wangekuwa pauni 200 milioni kwa kila mmoja.

Madrid wamenikumbusha jinsi ambavyo mpira umebadilika. Wamenikumbusha namna nyakati zinavyokimbia. Hatuna tena Galacticos siku hizi. Lakini hata kama wangekuwepo, bado tuna wababe wengi sokoni siku hizi.

Kwa sasa Madrid wanatengeneza timu nzuri ambayo ina damu changa zenye vipaji vikubwa. Kuna wenzao walikuwa wanafanya hivi zamani lakini wao wameamua kufanya hivi sasa hivi. Kuna mambo mawili hapa. Kwanza kabisa Wahispaniola hawana pesa.

Ni tofauti na zamani ambapo walikuwa na pesa nyingi. Sasa hivi hali zao ni tete. Wao na rafiki zao Barcelona hali zao sio nzuri. Lakini hata kama Perez angekuwa na pesa hizo kwa sasa, ni wachezaji gani wana hadhi ya kuitwa Galactios kwa sasa? Katika soko la sasa ni wawili tu. Erling Haaland na Kylian Mbappe.

Hawa wawili ndio unaweza kuwakusanya katika timu moja na dunia ikashtuka. Wakati ule aliweza kuwakusanya Zidane, Figo, Beckham na De Lima katika timu moja. Na hapo hapo Madrid tayari alishakuwa na majina makubwa kama Raul Gonzalez na Roberto Carlos.

Nje ya Madrid wakati huo tayari kulikuwa na majina makubwa kama ya akina Rivaldo, Ronaldinho, Thierry Henry na wengineo. Leo, pamoja na pesa zake za wakati ule nadhani Perez angepata wakati mgumu wa kuwakusanya mastaa wakubwa duniani. Angewatoa wapi?

Kuna mastaa wengi lakini hawajafikia hadhi zile. Ambao walikuwa wamefikia hadhi zile ni hawa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Ambaye alikuwa chini yao ni Neymar ambaye kamwe hakuwafikia akina Messi. Maisha yake ya soka yalikuwa na mkanganyiko mkubwa. Hakuweza kufikia mafanikio ya Messi na Ronaldo kuanzia katika ngazi ya klabu hadi timu ya taifa.

Baada ya hapo kulikuwa na daraja kubwa na wanaowafutia akina Eden Hazard. Mungu bariki wamekuja kutokea akina Mbappe na Haaland ambao tunaweza kusema kwamba kwa sasa ni Galactos wetu. Baada ya hapo kuna wachezaji wengi wazuri lakini hawajajiweka katika hadhi ya kuwa Galacticos.

Bahati mbaya kwa Perez pia ni kwamba sasa hivi kuna pesa nyingi za Waarabu. Kuna wachezaji wengi ambao wangeweza kucheza Real Madrid, Barcelona, Manchester United, Juventus, Chelsea na kwingineko lakini wameishia kucheza Manchester City au PSG kwa sababu ya pesa.

Wachezaji kama Kevin de Bruyne, Sergio Aguero, Thiago Silva na wengineo wangeweza kucheza katika klabu hizi hizo lakini katika ubora wao wamechagua mishahara mizuri ya Waarabu kuliko kwenda kucheza kwao.

Hata Mbappe ilikuwa wampate katika dirisha kubwa lililopita la majira ya majira ya joto lakini akaamua kubaki Ufaransa kwa ajili ya kupata mshahara mkubwa wa Waarabu. Sasa hivi nasikia anataka kuondoka na anaweza kwenda zake Madrid lakini hata hivyo wanaweza kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa pesa za Waarabu za Saudi Arabia au hata pesa za Waarabu za Ulaya.

Ni labda tu yeye mwenyewe aamue lakini ukweli ni kwamba Madrid hawana ubavu wa kupambana na Manchester City kama kila timu itaweka mezani pesa ya kumtaka Mbappe. Huu ni mkweli mchungu ambao Perez anapambana nao kwa sasa baada ya kutesa katika zama za Galacticos.

Mchezaji kama Guler ni mahiri sana. Lakini enzi hizo asingeweza kwenda Real Madrid kabla ya Mbappe. Ambacho kingetokea ni kwamba angekwenda katika klabu yoyote kubwa duniani kisha akajenga jina zaidi halafu Perez angemtwaa kwa rekodi ya uhamisho wa dunia.

Mchezaji kama Bellingham angeweza kutoka Dortmund kisha akaenda Manchester United halafu baada ya hapo Perez angeweza kuchomoza mbawa zake na kumtwaa kwa dau la uhamisho wa dunia. Hiki ndicho kitu ambacho kilikuwa kinaukonga mtima wake.

Maisha ya soka yamebadilika kwa sasa. Kila kitu kimebadilika. Sidhani kama zama zile zitarudi kwa urahisi tena. Na kitu kikubwa zaidi ni kwamba akina Pep Guardiola wamekuja kuuvuruga mpira wenyewe. Siku hizi mpira umekuwa mchezo wa kitimu zaidi. Wakati ule ulikuwa mchezo wa mchezaji mmoja mmoja zaidi. Ni ngumu kutengeneza wachezaji wenye ubora zaidi wakati mchezaji haruhusiwi tena kuonyesha uwezo wake binafsi na kitu kikubwa zaidi ni namna gani unaweza kucheza pamoja na wenzako.

Columnist: Mwanaspoti