Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kurejeshea maji waliokatiwa hatua muhimu vita ya corona

MAJI HUDUMA Kurejeshea maji waliokatiwa hatua muhimu vita ya corona

Fri, 8 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKATI huu ambao dunia inaendelea kukabiliana na janga la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, moja ya vitu muhimu vinavyohimizwa na wataalamu wa afya, ni matumizi ya maji tiririka kwa ajili ya kunawa mikono na sehemu zingine za mwili ambazo zinaweza kupata maambukizo ya virusi.

Pamoja na kuhimizwa matumizi ya maji tiririka, kuna changamoto kwamba si watu wote wanapata majisafi ya kunawa kama sehemu ya kujikinga, kutokana na baadhi kusitishiwa huduma za maji na mamlaka za maji kwa sababu ya madeni ya Ankara.

Kimsingi, hali hiyo inakuwa ni kikwazo dhidi ya kujikinga kwa kila mmoja kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka na sabuni, tena wakati huu ambao watu wengi wameitikia ushauri na maelekezo ya wataalamu wa afya na serikali.

Jambo la kutia moyo ni uamuzi uliotangazwa jana na serikali wa kuiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kuwarejeshea huduma za maji wateja wote nchini waliokatiwa huduma hiyo kutokana na madeni kwa makubaliano.

Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso, katika uamuzi huo ilifafanua kuwa lengo ni kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma hiyo katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya maambukizo ya ugonjwa wa COVID 19.

Aweso alitoa agizo hilo jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza mambo mbalimbali na menejimenti ya Ewura, yakiwamo malalamiko ya ankara kubwa za maji zinazotolewa kwa wateja.

Alisema taifa liko katika mapambano na vita dhidi ya corona, hivyo jambo muhimu ni kuchukua tahadhari na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu.

Alisema silaha pekee ya kukabiliana na maambukizo ya virusi hivyo ni maji tiririka na kunawa kwa sabuni, serikali imeamua wateja wote waliokatiwa maji warejeshewe kisha Ewura iweke utaratibu mzuri wa kulipa madeni yao.

Alieleza kuwa, zipo mamlaka za maji ambazo ni vinara kwa kuwabambikia na kuwapandishia wananchi bei za maji kiholela, hivyo aliiagiza Ewura kuhakikisha inafikisha ripoti ya mamlaka za aina hiyo wizarani ili kuzichukulia hatua stahiki, kwa kuwa mana wizara ndiyo yenye mamlaka ya mwisho.

Uamuzi huo unastahili kupongezwa kwa kuwa serikali imeona kuwa wenye madeni ya ankara za maji kukosa huduma hiyo kutarudisha nyuma jitihada zinazochukuliwa za wananchi kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona.

Lakini pia, kauli za Naibu Waziri Aweso zinaonyesha kuwa hata serikali imebaini mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya mamlaka za maji nchini kuwabambikia watumiaji wa maji ankara za maji zisizo na uhalisia, hivyo kushindwa kulipa na matokeo yake kukatiwa huduma.

Hatuamini kama kuna mtumiaji wa maji anayeweza kukaidi kulipa Ankara ya maji makusudi, hivyo tunaona ulazima wa Ewura kulichukua suala la ankara kubwa za maji zisizo na uhalisia kama changamoto ya kuifanyia uchunguzi na kuipatia suluhisho la haraka.

Tunachokihisi ni kuwa baada ya serikali ya sasa kuzibana mamlaka za maji kuacha kufanya kazi kwa mazoea ya kutegemea kupewa ruzuku kutoka serikalini, baadhi ya mamlaka zinawabambikia ankara watumiaji ili kupata mapato zaidi ya kujiendesha.

Ni matarajio yetu kuwa Ewura itatekeleza maagizo yote iliyopewa na serikali kama ilivyoahidi haraka iwezekanavyo hususan kurejeshea watumiaji maji huduma na kuweka utaratibu mzuri wa kulipa.

Utaratibu wa kulipa madeni hayo haunabudi kwenda sambamba na wateja kushirikishwa kwa uwazi na mamlaka husika za maji katika suala la ankara ili kuepukana na Ankara zisizo na uhalisia.

Ewura pia izisimamie mamlaka za maji kuhakikisha zinaweka dawa za kutibu maji wakati huu wa tahadhari dhidi ya maambukizo ya virusi vya corona. Kwa kufanya haya, ni matarajio yetu kuwa tutakuwa timechukua hatadhari ya kutosha.

Columnist: www.tanzaniaweb.live