Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kura moja ina nguvu ya kuleta mabadiliko chanya

Bc81b48858be127d68488a6c44d75015 Kura moja ina nguvu ya kuleta mabadiliko chanya

Mon, 26 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

OKTOBA 28, 2020 ni siku muhimu na ya kihistoria katika Taifa letu kwani siku hiyo watanzania watatumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wanaowania nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi na udiwani ili kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997, watanzania wanapata fursa ya kutimiza haki hii ya kidemokrasisa ya kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu mara moja katika kila kipindi cha miaka mitano.

Hivyo basi, fursa wanayopata wananchi ya kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu ni fursa adhimu sana kwani ina uhusiano wa moja kwa moja na mustakabali wa maendeleo ya nchi.

Hii inatokana na ukweli kwamba viongozi bora ni chachu ya kufikia maendeleo ya wananchi katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Viongozi bora wanapatikana baada ya wananchi kutimiza wajibu wao wa kikatiba wa kupiga kura. Mtaji wa ushindi kwa wagombea wa nafasi za uongozi ni kura nyingi watakazopigiwa na wananchi katika sanduku la kura siku ya uchaguzi.

Kimsingi, ili kupata viongozi bora, ni lazima wananchi wenyewe wenye kiu ya kupata na kuongozwa na viongozi bora watimize wajibu wao wa kidemokrasia kwa kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kuwachagua viongozi bora.

Baadhi ya wananchi wana dhana potofu kuwa hata bila kupiga kura, wagombea wanaowapenda wanaweza kushinda na kutangazwa kuwa washindi baada ya zoezi la kuhesabu kura kumalizika.

Hii ni dhana potofu, kwani msingi wa ushindi ni mgombea kupata kura nyingi MAKALA kutoka kwa wapiga kura na siyo vinginevyo.

Lengo la makala hii ni kutoa wito kwa wananchi wote waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi siku ya Jumatano ya Tarehe 28 Oktoba, 2020 ili kuchagua viongozi bora.

Ni kwa kufanya hivyo maendeleo yataweza kuwafikia kwa kuwa watakuwa wamechagua viongozi bora kwenye kata, jimbo na nchi kwa ujumla. Ieleweke kwamba viongozi hawa wana nafasi kubwa katika kuboresha au kudidimiza maendeleo yetu ya kila siku.

Kura moja ya mwananchi ina uwezo wa kusababisha ushindi wa diwani, mbunge na hata rais. Wananchi ni mashahidi kwa namna ambavyo katika chaguzi za kura za maoni ndani ya vyama vya siasa hasa katika nafasi za udiwani na ubunge, baaadhi ya wagombea walifungana kwa idadi sawa ya kura na wengine wakizidiana kwa kura moja tu.

Hii maana yake ni kwamba kura moja ambayo mjumbe alipiga wakati wa kura za maoni ilisababisha wagombea kufungana kwa idadi ya kura na hivyo mmoja wao asingepiga wasingefungana.

Halikadhalika kura moja ya mjumbe ilisababisha tofauti ya kura moja katika ya mgombea mmoja na mwingine.

Kwa mantiki hii, mwananchi hapaswi kuidharau kura yake moja kwa kudhani kuwa kura yake haichangii chochote katika kuleta ushindi wa mgombea anayemwamini katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Kila mwananchi anapaswa kuamini kuwa kura yake moja ndiyo mtaji wa ushindi kwa mgombea anayemtaka na bila kura yake ushindi hautapatikana. Maelfu ya kura atakayopata mgombea ni matokeo ya kujumlisha kura moja moja alizopigiwa na wananchi.

Hivyo, bila kuanza na mtaji wa kura moja, hakuna makumi, mamia, maelfu, makumi elfu wala mamilioni ya kura anayoweza kuyapata mgombea katika uchaguzi.

Kutokana na kiu ya wananchi ya kupata viongozi bora, kila mwananchi athamini kura yake kuwa ndiyo sababisho la ushindi na kupata viongozi bora.

Ni muhimu pia katika nyakati hizi za kuelekea mwisho wa kampeni kila mtu akawa makini kusikiliza sera za wagombea ili kujua ni mgombea gani anafaa kumpigia kura.

Nchi yetu, pamoja na maendeleo makubwa yaliyopatikana, bado ina changamoto katika sekta za elimu, afya, maji, nishati, mifugo, miundombinu, kilimo, uvuvi, masoko na kadhalika.

Ni kupitia kwa viongozi tutakaowachagua wiki ijayo, changamoto hizi zitapata ufumbuzi kupitia viongozi hao na kama tutachagua vibaya ikiwa ni pamoja na kusgindwa kutojitokeza kupiga kura, basi kama wanavyosema vijana itakuwa imekula kwetu.

Kura moja ya mwananchi itachangia mafanikio ya utatuzi wa changamoto hizi kutokana na uongozi bora utakaopatikana ambao utajikita katika kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Kutokana na nguvu ya kura moja katika kusababisha ushindi wa wagombea na mabadiliko/ matokeo chanya ya kimaendeleo, mwananchi hapaswi kubaki nyumbani siku ya uchaguzi badala yake ajitokeze kwenda kupiga kura na hasa kwa kuzingatia kwamba siku ya Uchaguzi itakuwa siku ya maapumziko.

Moja ya jambo ambalo limeufanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa wa kipekee, ni uchaguzi kufanyika katikati ya juma badala ya siku za wikiendi ambazo watu wengine huenda kwenye nyumba za ibada au kubanwa na shughuli zingine za mwisho wa juma kama kufua au kutembelea mashamba.

Hii inatoa fursa kubwa kwa wananchi waliojiandikisha kupata wasaa wa kupiga kura bila kizuizi chochote.

Wakati wa wananchi kufanya maamuzi sahihi juu ya mustakabali wa maendeleo ya kata, majimbo na nchi yao ni sasa kwa kuhakiksha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuchagua viongozi bora wenye nia ya kuwatumikia wananchi.

Mwananchi usidharau kura yako moja, kura moja ni mtaji wa ushindi kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi. Mwananchi, jitokeze Oktoba 28 kupiga kura. Kura yako mwananchi ndiyo huamua hatma ya maendeleo. Mwananchi, tafakari, chukua hatua.

Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali ilioko Kongwa mkoa wa Dodoma.

Mawasiliano yake ni 0765-409249.

Columnist: habarileo.co.tz