Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kuondoa madhara ya corona kisaikolojia kwa wanawake

89ef40139916bdbe59589988499d1d4e Kuondoa madhara ya corona kisaikolojia kwa wanawake

Fri, 26 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

LILIPOIBUKA janga la homa kali ya mapafu (Covid-19), wanawake wakiwa walezi wakubwa wa familia na wazalishaji katika sekta isiyo rasmi, walikuwa miongoni mwa waathirika wakubwa hasa kiuchumi na kisaikolojia.

Kwa mfano, Violet Longo, mjasiriamali na mkazi wa Idundilanga mjini Njombe, ni mama wa watoto watatu. Anasema ugonjwa wa corona ulipoibuka mwaka jana ulimkuta akiwa katika marejesho ya mkopo wa Sh milioni 10 alizokopa benki.

Anasema: “Kwa kweli hakuna kipindi kilichokuwa kigumu kwangu na kilichonitesa, kama ilipoibuka corona mwaka jana maana corona ilinikuta kwenye deni na wateja wa biashara yangu wakapungua huku nikiwa ninapaswa kufanya marejesho... Kwa kweli nilikuwa na stress (msongo) sana.”

Kwa mujibu wa uchunguzi wa HabariLEO, hali imewafanya wengine kuzalisha na kulea hofu inayowaathiri wengi hata kujidhani wanaumwa na pengine kupoteza maisha, kumbe hawaumwi.

Hali hiyo ndiyo inamfanya Rais John Magufuli aendelee kuwatia moyo Watanzania ili wazidi kumwomba Mungu na kuondoa hofu huku wakiendelea na shughuli zao kwa kuzingatia kanuni za wataalamu wa afya mintarafu namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali hususan yanayoambukizwa kwa njia ya hewa ukiwamo wa Covid-19.

Mkurugenzi na Mtaalamu wa Saikolojia katika taasisi ya Global Source Watch ya Dar es Salaam, Dismas Lyassa, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Benezeth Bwikizo na Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Joyce Shebe, wanasema kwa nyakati tofauti kuwa tatizo kama hili la Covid-19 linapotokea, wanawake ‘wapewe jicho la kipekee’ na kusaidiwa ili kuepusha madhara zaidi kwa jamii.

Bwikizo anasema tafiti nyingi zinaonesha kwamba hofu na mashaka ni vitu vinavyoua sana kutokana na kupunguza kinga ya mwili.

Mwenyekiti wa Sauti ya Wanawake Wenye Ulamavu Tanzania (Swauta), Angella Michael anasema: “Kutokana na hali hiyo, Covid-19 ilipoibuka mwaka jana, wanawake wengi wenye ulemavu waliyumba kiuchumi maana walibaki kukaa nyumbani tu…”

Anaongeza: “Wakati wa corona, watu wengi hawakutaka kuwasaidia kwa kuwa wanaogopa maambukizi kwa kugusana au kusogeleana kwa hiyo wenye ulemavu wakabaki tu, na msongo hawana tumaini maana wanawake wengine wenye ulemavu, ili kupata huduma mbalimbali lazima washikwe na wengine hawaoni hivyo, lazima washikiliwe na kuongozwa.”

Mmoja wa washiriki wa mafunzo kwa wanahabari yaliyoendeshwa na Tamwa kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la UN-Women yakilenga kuibua changamoto zilizowakumba wanawake katika kipindi cha corona mwaka jana na namna walivyozikabili, fursa na namna ya kujiandaa kwa wakati mwingine linapotokea tishio au janga kama hilo, alisisitiza wanahabari na jamii kutambua nafasi na umuhimu wa wanawake katika jamii kwa kutoa kipaumbele kwa habari chanya zinazowahusu na kuwasaidia na si kinyume.

Katika mafunzio hayo alisema: “Tutoe (wanahabari) elimu ili katika vipindi kama hivi, jamii ishirikiane kuwasaidia wanawake, badala ya kuwaacha wenyewe au kuwaingiza katika mateso zaidi ya kiuchumi, kisaikolojia na kijamii… Habari zetu zijikite kuwasaidia na kuwatia moyo ili wanyanyuke na kuimarika na si vinginevyo.”

Wadau hao wanasema yapo mambo mengi yanayosababisha mateso makubwa ya kiuchumi na kisakolojia kwa wanawake katika nyakati na mazingira ya majanga kama mlipuko wa Covid-19 ukiwamo msongo wa mawazo wakihofia familia kupoteza mzalishaji mkuu wa mapato ambaye mara nyingi ni baba na hata mateso ya kuuguza na kufiwa.

Kupitia mafunzo hayo, wanahabari wanahimizwa kutafuta na kuandika au kutangaza habari zinazoelimisha, kuwatia moyo na kuwahamasisha na kuwainua wanawake katika vipindi vigumu kama hicho.

Wadau wengine katika mradi huo ulioendesha mafunzo hayo ni WiLDAF (Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika), TGNP (Mtandao wa Jinsia Tanzania), TDC (Kituo cha Demokrasia Tanzania) na AWLN (African Women Leaders Network).

Lyassa anasema: “Wanawake wengi huingiwa hofu zaidi kuliko wanaume na kama ni mjamzito, hofu hiyo haimfanyi mtoto kuwa salama maana msongo unaweza kuathiri vibaya makuzi ya mtoto huyo tumboni hali inayoweza kusababisha azaliwe akiwa na hali isiyotarajiwa ama kimaumbile, au kitabia…”

Anaongeza: “Unajua katika jamii zetu, wanawake wengi bado wanategemea wanaume katika mahitaji; sasa anakuwa anafikiria, kama ataugua yeye au kufa, watoto wake watalelewa na nani na kama kwa mfano ugonjwa unaendelea, hatima ya kazi ya mume inayowapa riziki itakuwaje...”

Kuhusu madhara ya msongo kwa wanawake kijamii, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Ngorongoro, Bwikizo, anasema ni pamoja na kusababisha mabadiliko hasi ya kitabia na hata kupenda kujitenga, kuwa na hisia zinazobadilika badilika kila mara bila sababu; mara furaha, mara huzuni au hasira na hata kununa ovyo.

Kuhusu hili, Lyassa yeye anasema: “Msongo unaweza kubomoa ndoa kwa mke kutopenda hata kumsogelea mume, hali inaweza kumfanya mmoja ajisikie hatendewi haki na kuchukua uamuzi usio mzuri…”

Madhara mengine Lyassa anasema: “… Pia kuna kutukana au kupiga watoto hata kwa kosa dogo na la kawaida … Kwa hali hiyo hata kama mama anafanya biashara, kila mteja anapomfikia akiiona, anaamua kwenda kununua sehemu nyingine hivyo, biashara na kipato cha familia kuporomoka na inaweza kumsababisha hasara kwa upotevu wa mali.”

Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), ajira isiyo rasmi ni chanzo kikuu cha ajira barani Afrika zikichangia asilimia 85.8 ya ajira zote. Karibu sekta yote ya kilimo barani Afrika ni ile isiyo rasmi (asilimia 97.9).

Naye Mwenyekiti wa Tamwa, Joyce Shebe, anasema uwepo wa wanawake wengi katika sekta isiyo rasmi kiuchumi, uliwafanya wengi kuathirika kimapato katika kipindi cha Covid-19 mwaka jana baada ya wengi kupunguzwa kazi na wengine kusitisha shughuli kama biashara au taasisi zao kusitisha utendaji na uzalishaji.

Anasema hali hii iliibua na kuchochea msongo wa mawazo miongoni mwa wanawake wengi kwa kuwa ndio walezi wakuu wa familia na wazalishaji wakubwa katika sekta binafsi.

Shebe anasema: “Iwepo mikakati ya pamoja ya kuwasaidia badala ya kuwaacha wenyewe kwani kufanya hivyo, kunaleta madhara makubwa zaidi katika jamii nzima...”

Kwa nyakati tofauti Shebe na Bwikizo wanasema, kukaa kwa wengi nyumbani kulisababisha kuwapo kwa matukio kadhaa ya udhalilishaji, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake wakiwamo wenye ulemavu hasa vipigo, ubakaji, ulawiti na ukosefu wa mahitaji muhimu.

“Katika nyakati ngumu kama hizo za corona na nyingine, wanawake wengi hufanyiwa unyanyasaji wa kiuchumi na kihisia na hilo, linachochea msongo na madhara makubwa zaidi,” anasema Bwikizo.

Watu mbalimbali wanasema katika kipindi hicho, msongo wa watoto na mume, ulihamia kwa wanawake kwa namna mbalimbali ama ukali, au ukaribu kupitia kiasi hali iliyosababisha mimba zisizokusudiwa.

Naye Shebe anasema: “Unajua mwanamke unaweza kuwa kwenye ndoa ukabakwa, au usiwe kwenye ndoa, pia ukabakwa… Tulichojifunza kikubwa ni kuwa, kwa kuwa ndio wazalishaji wakubwa katika sekta isiyo ramsi ikiwamo kilimo na biashara na pia, walezi wa familia, linapotokea janga, wasiachwe peke yao, bali wasaidiwe ili waendelee kutimiza wajibu wao maana wakiachwa, mambo mengi kama kilimo biashara na mengine yatasimama.”

Kwa mujibu wa Shebe, serikali ishirikiane na wadau mbalimbali zikiwamo taasisi za dini na nyingine zisizo za kiserikali kuweka mipango ya kimkakati kuhusu wanawake, watoto na watu wenye ulemavu ili majanga kama hili yanapotokea, visiwepo vitendo vya unyanyasaji na ukatili, bali wasaidiwe kisaikolojia, kiuchumi na kijamii na kuheshimiwa.

Miongoni mwa namna ya kuwasaidia, Bwikizo alisema ni pamoja na maofisa maendeleo kuwasaidia kujiunga katika vikundi na kupata mikopo ya asilimia 4 zinazotokana na mapato ya ndani ya halmashauri zao kwa ajili ya vikundi vya wanawake.

“Lakini pia, ikitokea hali kama hiyo, halmashauri hizo ziwasaidie kwa kuongeza muda wa marejesho ya mikopo waliyokopa kwa kuwa biashara zao zinaweza zisipate wateja kama ilivyokuwa mwanzo,” alisema.

Bwikizo anasema wataalamu wa maendeleo ya jamii wajitokeze zaidi kuwasaidia wanawake kuanzisha na kuendesha miradi isiyoathirika na tatizo lililopo.

“Kwa mfano, hapa Ngorongoro na Karatu, wanawake wengi ni wajasiriamali wanaotegemea biashara ya utalii yakiwamo mapambo ya asili kama shanga, maonesho ya ngoma za jadi na hata uuzaji vinyango. Mambo haya mwaka jana yaliathirika sana covid- 19 ilipoingia nchini maana watalii walipungua.”

Bwikizo anaongeza: “Sasa watu kama hawa, wafundishwe na kusaidiwa kuanzisha miradi na shughuli nyingine zisizotegemea utalii kama kilimo…”

Watalaamu mbalimbali wa saikolojia wanasema, vinapotokea vipindi kama hicho cha janga la corona, wanawake waepuke msongo kwa kukubali hali halisi na kutambua ukweli kuwa itapita.

“Epuka kusikiliza au kusoma habari zinazoonesha ukubwa wa tatizo na kutisha zaidi, bali zenye matumaini na zinazoelimisha kuhusu nini cha kufanya na kubwa zaidi, fikiria kitu chanya cha kufanya na si kukata tamaa…” kinasema chanzo mimoja mtandaoni.

Lyassa na Bwikizo wanasema namna nyingine ni wanawake kukaa na watoto wanaocheza ili wawaambukize furaha, badala ya kukataa michezo na tabia zao hasa zisizo na madhara.

Columnist: habarileo.co.tz