Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kuna waamuzi wamepotea jumla - 7

WAAMUZI Kuna waamuzi wamepotea jumla

Wed, 11 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika mfululizo wa Ripoti Maalumu ya Waamuzi Bongo, jana tuliona ishu ya waamuzi na rushwa, lakini wakati huohuo tukagundua ni kwanini waamuzi wengi wa Bongo wameshindwa kuwika kimataifa kwenye michuano mikubwa kama Afcon, Chan na hata Kombe la Dunia, leo tunatazama mambo mengine mbalimbali, ikiwemo waamuzi waliopotea jumla kuchezesha mechi za Ligi Kuu na nyinginezo.

WALIOPOTEA

Suala la ubora wa waamuzi wa Tanzania limekuwa mjadala mkubwa kwa mashabiki na wadau wengi wa soka hapa nchini kila yanapoibuka makosa ya kiuchezeshaji kwenye ligi za madaraja mbalimbali lakini hasa Ligi Kuu Bara.

Ligi Kuu Bara ina waamuzi wengi wa kati na wa pembeni wanaochezesha mechi mbalimbali huku baadhi wakipewa mechi kubwa zinazohusisha Simba na Yanga kutokana na wao kuonekana bora ingawa wakati mwingine nao wamekuwa wakifanya makosa ambayo yamekuwa yakizua maswali kwa mashabiki.

Baadhi ya waamuzi ambao wanaaminiwa sana kuchezesha mechi kubwa zinazohusu Simba na Yanga kwa sasa ni Elly Sasii, Ramadhan Kayoko, Ahmed Arajiga, Emmanuel Mwandembwa na Hans Mabena.

Lakini kuna waamuzi waliowahi kuwika kwa watawala tofauti wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanzia kipindi cha Leodegar Tenga hadi sasa rais Wallace Karia.

Waamuzi hao waliwika kutokana na ubora wao lakini hawakukwepa baadhi ya vifungo kutokana na kuvurunda baadhi ya mechi huku wengine wakiweza kumudu katika utawala wa marais wote watatu na wengine wakiishia njiani na kuwashuhudia wapya wakiibuka.

OSMAN KAZI

Mwamuzi huyu aliwika sana kipindi cha utawala wa Tenga akitajwa kama mmoja kati ya waamuzi bora kuwahi kutokea kwenye soka la Tanzania.

Mara nyingi alipokuwa uwanjani akichezesha Dabi alisimamia ipasavyo sheria za soka na alikuwa mwenye misimamo mikali.

Hata hivyo, mwaka 2009 mwishoni Kazi alipata bahati mbaya baada ya kufungiwa maisha kujihusisha na soka kutokana na kuhusishwa na rushwa.

Kazi pamoja na waamuzi wenzake wasaidizi watatu ambao ni Omari Miyala, Kamwanga Tambwe na Omari Mfaume walifungiwa na TFF wakihusishwa na rushwa kutokana na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Mtibwa Sugar na Majimaji.

Hata hivyo, baadaye Kamati ya Nidhamu ya TFF iliyokuwa chini ya Kamanda wa zamani wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana ilitengua adhabu za kufungiwa maisha kwa Kazi, na kumpunguzia adhabu hadi miezi mitatu wakati waamuzi wenzake walitakiwa kutumikia adhabu kwa miaka mitatu.

Hata hivyo, Kazi licha ya kumaliza adhabu hiyo hakuwahi kurejea tena kuchezesha Ligi Kuu Bara na badala yake alijikita kuchezesha mechi za mitaani na mabonaza na sasa anafanya kazi Azam TV.

“Baada ya ile adhabu ya kufungiwa nikaamua kuacha kuchezesha kwani niliona kama mizengwe kwangu imekuwa mingi hivyo nikaona hata ndoto zangu ambazo nilizipanga kuwa siku moja niwe mwamuzi wa kwanza Tanzania kuchezesha Kombe la Dunia niliona hazitatimia kutokana na mambo yaliyokuwa yakitendeka dhidi yangu.

“Sasa hivi nimebaki kama mkufunzi wa waamuzi kupitia kipindi cha Kipyenga cha Mwisho kinachorushwa kila Alhamisi kwenye Azam Tv na naamini wanaotaka kujifunza wakinifuatilia huko kuna vitu vitawasaidia kuwa waamuzi wazuri,” anasema Kazi.

ALEX MAHAGI

Huyu ni mwamuzi mwingine ambaye aliwika katika utawala wa marais wawili, Tenga na Malinzi lakini kashindwa kupenya katika utawala wa sasa wa Karia.

Mahagi aliyekuwa mwamuzi kutoka Mwanza alisifika na wachezaji kuwa mmoja ya waamuzi wanaokumaliza uwanjani huku akitabasamu.

Aliwahi kupata dhahama ya kufungiwa mara kwa mara lakini moja ya matukio yake makubwa yaliyotikisa ni la mwaka 2014 baada ya kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa kuchezesha Ligi Kuu Bara kwa kosa la kukiuka maadili ya soka na weledi kwenye taaluma yake baada ya mchezo kati ya Mgambo Shooting na Yanga.

Mahagi alipewa adhabu hiyo baada ya kutaka kumpekua mchezaji Mohamed Neto wa Mgambo Shooting kwa madai ameficha kitu kinachodhaniwa kuwa ni hirizi kwenye sehemu zake za siri na alipomgomea alimtoa kwa kadi nyekundu.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi wa wakati huo, Silas Mwakibinga alisema mwamuzi huyo hakupaswa kumpekua mchezaji ndani ya uwanja hali iliyotafsiriwa ni kumdhalilisha.

ITAENDELEA KESHO...

Columnist: www.tanzaniaweb.live