Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kuna siri Simba wanaificha kwa watani zao Yanga SC?

Yanga Vs Simba Kirumba Kuna siri Simba wanaificha kwa watani zao Yanga SC

Wed, 19 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Jumapili jioni Simba na Yanga zinacheza uwanja wa Taifa. kama Yanga wakiifunga Simba nitacheka sana halafu nitachanganyikiwa. Sio mimi tu, hata mashabiki wa Yanga watachangikiwa. Na mashabiki wa Simba pia watachanganyikiwa zaidi.

Juzi Jumapili usiku tulipata matokeo mkononi. Yanga ilitolewa rasmi na Al Hilal ya Sudan. Simba ilikuwa imepita dhidi ya CD Primeiro de Agosto ya Angola. Sitaki kuzungumza kuhusu mbinu za uwanjani. Kila mmoja ameona kilichofanywa na kina Moses Phiri Uwanja wa Mkapa na kile kilichofanywa na kina Fiston Mayele kule Khartoum. Vitu viwili tofauti.

Wiki ijayo wanacheza wenyewe kwa wenyewe na huenda Yanga wakaifunga Simba, lakini hata wakiifunga Simba itabidi wajicheke. Kuna mahala timu hizi mbili zimeamua kuchukua mwelekeo tofauti. Mwingine anakwenda Magharibi wakati mwingine anakwenda Mashariki

Kama wakiifunga Simba inaweza kuwa mechi ya tatu mfululizo wanaifunga Simba. Lakini subiri kwanza. Tusikimbie katika topiki ya msingi. Kwa nini nguvu kubwa ya maandalizi ya kimwili na kiakili kama wanavyofanya katika mechi za Simba wasihamishie pia katika mechi za kimataifa?

Wiki iliyoisha kuna kitu kimedhihirika kwamba kuna kitu Simba inafahamu, halafu watani zao hawafahamu. Sijui ni kitu gani lakini ukweli Simba ipo hatua nyingi mbele ya Yanga linapokuja suala la mechi za kimataifa.

Ukweli ni Simba haikucheza na wapinzani wagumu sana lakini imefanya kazi yake ugenini na kisha nyumbani. Yanga haikucheza na wapinzani wagumu sana lakini imeshindwa kufanya kazi yake nyumbani kisha ugenini.

Unaweza kusema Yanga ilicheza na wapinzani wagumu Al Hilal, lakini kumbe sio ajabu usingesema hivyo kama wapinzani wao wangecheza na Simba. Unaweza kudhani Simba imecheza na wapinzani wepesi De Agosto, lakini kumbe usingesema hivyo kama De Agosto ingecheza na Yanga.

Kuna kitu Simba inacho katika mechi za kimataifa halafu Yanga haina. Wanajiamini, wanajua wanachofanya ndani na nje ya uwanja. Kitu hicho kimesambaa kwa wachezaji, mashabiki, viongozi na benchi la ufundi. Wanahisi wanapita halafu kweli wanapita.

Mechi dhidi ya Simba kwa watu wa Yanga inakuwa ngumu. Ushabiki mkubwa, hisia kali, na hapo hapo Simba ni wagumu. Inakuaje Yanga wanaweza kushinda? Kwanini hisia kama hizi wasizimiashie katika mechi za kimataifa? Ni swali ambalo wataendelea kujiuliza.

Simba wana siri ambayo wanaificha kwa Yanga. Kwa kikosi ambacho Yanga walikuwa nacho nadhani walistahili kusonga mbele dhidi ya Al Hilal. Kinachokosekana ni mwamko wa mechi yenyewe ndani na nje ya uwanja. Simba wanacho kitu hiki na wamejenga imani.

Ni kama ilivyo kwa Liverpool linapokuja suala la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Kuna kitu kinawasukuma na kuwaambia ni michuano yao. Na linapokuja suala la Uwanja wa Anfield huwa kuna mizimu yao inawasukuma zaidi mashabiki na wachezaji.

Mwaka 2005 wakati wanachukua ubingwa wa Ulaya ilikuwa kama vile wanaurudisha ubingwa waliouzoea nyumbani. Walishindwa kuingia Top Four lakini wakafanikiwa kuchukua ubingwa wa Ulaya. Kumbuka kwamba walikuwa wana miaka 25 hawajachukua ubingwa wa Ligi Kuu ya England lakini wakafanikiwa kutwaa Ulaya.

Hii imani ndio ambayo wanayo Simba na michuano hii. Timu zao zinabadilika lakini moto wao uko palepale. Miaka ya karibuni alikuwepo Emmanuel Okwi akaondoka zake, akaja Luis Miquissone akaondoka zake na sasa kuna Augustine Okrah. Sio tu kwamba aina hii ya watu wanafanya vizuri katika michuano ya ndani lakini wameacha alama hata katika michuano ya kimataifa. Hii ni achilia mbali kina Clatous Chotta Chama.

Yanga wanahitaji kuibeba imani hii katika mioyo yao. Miongoni mwa mambo ambayo yamewashinda mpaka sasa pia ni kuugeuza Uwanja wa Mkapa kama silaha yao kubwa. Simba wamefanikiwa kuugeuza huo kuwa Anfield yao. Yanga walishinda mechi mbili nyepesi dhidi ya Zalan lakini katika pambano dhidi ya Al Hilal walipaswa kuhakikisha wageni hawatoki. Kama unafahamu kwamba Uwanja wa Khartoum ni mgumu basi unapaswa kushinda kwako kabla ya kufikiria mengine.

Simba iliwahi kufungwa mabao matano katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Al Ahly na AS Vita lakini katika mechi za marudiano ilikuwa kama vile wanacheza na timu mbili tofauti. Simba ya ugenini ilikuwa tofauti kabisa na ya nyumbani. Mechi mbili za Yanga dhidi ya Al Hilal tumeshuhudia Yanga ilikuwa ile ile tu katika mechi zote. Tofauti pekee labda ilikuwa bao la Fiston Mayele alilofunga Kwa Mkapa.

Watu wa Yanga wanaweza kuomba kikao cha siri na watu wa Simba. Ni katika suala la mechi za kimataifa. Kabla ya siri nyingine ambazo wanaweza kuambiwa lakini kwanza wahakikishe wanabeba siri nzito ya kuhakikisha Uwanja wa Mkapa hatoki mtu. Kuna kitu Simba wanafanya na wanaambukizana katika vizazi vyao. Timu zinabadilika, mashabiki wanabadilika, viongozi wanabadilika lakini imani yao huwa inabakia pale pale tu. Ni kitu ambacho Yanga wamekielekeza zaidi katika pambano la watani wakati Simba wamekielekeza zaidi katika mechi za kimataifa.

Unaweza kuona kundi la Simba linapangwa na timu ngumu lakini mashabiki wa Simba wakaanza kujinasibu kwamba wanatoboa. Hatimaye wanatoboa kweli. Hii ni imani chanya ambayo inawapa wachezaji msukumo mkubwa wa kufanya kweli.

Yanga bado hawajaingiwa na imani hii. wachezaji wao pia bado hawajaingiwa na imani hii. Aziz Ki wa ASEC Mimosas na Ki Yanga ni wawili tofauti katika mechi za kimataifa. Kuna kitu Yanga inabidi wafanye. Timu wanayo, inaweza kuwa nzuri kuliko Simba, lakini Simba wana kitu wanacho. Wakati mwingine kitu hicho hakihitaji timu nzuri.

Columnist: Mwanaspoti