Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kuna jipya kwa Joe Biden dhidi ya Afrika?

E7d43c10fef580da236637d07bddbf7b Kuna jipya kwa Joe Biden dhidi ya Afrika?

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MNAMO Januari 20, mwaka huu, Joe Biden na Makamu wake Kamala Harris, waliapishwa kuwa Rais wa Marekani. Kwa kiapo hicho Biden anakuwa Rais wa 46 wa taifa hilo ambalo ni tajiri kwa kutegemea maliasili kutoka karibia mataifa yote ulimwenguni huku makamu wake akiwa wa 49.

Kwa minajili ya kuboresha makala haya, Kamala anakuwa Makamu wa Rais wa kwanza mweusi kwa Taifa hilo linalojiita baba wa demokrasia lakini kwa miaka yote halikuwahi kutambua nafasi ya mwanamke katika utawala wa nafasi kubwa.

Kwetu Tanzania ni tofauti maana tulianza kutambua hilo mwaka 2015 baada Rais Magufuli kumteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ulipofika wakati wa kutoa hotuba yake kama Rais muapishwa, Biden aligusia mambo mengi lakini ya msingi kwa minajili ya makala haya aligusia kuerejesha demokrasia iliyokuwa imefubazwa na mtangulizi wake Donald Trunp na umoja wa wamarekani. Biden aliongeza kwamba serikali yake itaongeza kasi katika kuziba mimomonyoko iliyokuwa imesababishwa na Trump, kurejesha yaliyokuwa yameharibiwa, kutengeneza tiba zaidi, ujenzi wa nchi yao na pia kuifaidisha nchi yao.

Ni vyema ikakumbukwa kwamba Biden kabla ya kuwa rais aliwahi kuwa makamu wa rais wa 47 wa Marekani wakati wote wa utawala wa Baraka Obama. Akiwa makamu wa rais alitoa ushauri sana kuhusu Iraq na Afganstan na Libya.

Kwa kuwa Muammar Muhammad Abdu Minyar al Gaddafi maarufu kama Muammar Gaddafi aliuliwa katika kipindi cha utawala wa Obama. Nakumbuka katika moja ya hotuba za Obama baada ya kumaliza muda wake wa urais alisema moja ya mambo makuu anayojutia ni kuridhia kuondolewa madarakani kwa Gaddafi kabla ya kuandaa mtu mwingine wa kuchukua nafasi yake baada ya kuuawa kwa mwamba huyo mmoja wapo wa Afrika.

Mwaka 2010 Biden alipokuwa Kenya alisema “Natumaini haya nitakayosema hayataonekana kama mafundisho kwenu… lakini utajiri wenu mwingi umepotea kwasababu ya rushwa na viongozi wakubwa wanaonekana kushiriki katika jambo hili’. Hata hivyo, wakati anayasema haya Marekani ilikuwa ikijinasibu kuwa baba wa demokrasia ulimwenguni.

Kwa sasa sijui kama Biden anaweza kuyasema maneno haya akiwa Rais na huku akipambana na kupokwa kwa demokrasia hiyo hiyo na kiongozi mtangulizi wake? Hili ni swali tunalopaswa kujiuliza kama Waafrika lakini pia na Biden mwenyewe kama ataweza kunyanyua kidole chake tena dhidi ya mataifa ya Afrika au atagundua kwamba vidole vitatu vilivyobaki vitakuwa vinamtazama yeye vikimtaka ajisafishe na taifa lake kwanza! Ni wazi bila kificho katika utawala wa Trump mataifa mengi ya Afrika yalidhalilishwa sana tena wazi pasipo na kificho. Udhalilishaji huu ulianzia kwenye kunyimwa visa za kuingia kwenye taifa hilo, ubaguzi wa rangi na mengine mengi.

Waafrika walidhalilishwa kwa kutojua maana ya demokrasia na kitu pekee wanachofahamu ni kuzaliana tu. Na wakipewa silaha wanauana tu. Wakati udhalilisha huo unatokea Trump alisahau kwamba baadhi ya mataifa ya Afrika yanayopata taabu katika masuala mazima ya utawala wa kisiasa ulisababishwa na wao kwa lengo la kuiba mali asili.

Hali hii inanifanya nijiulize kama Biden atafanya nini kuisafisha Afrika kwa ulimwengu wote? Atafanya nini kwa Afrika ili kubadilisha msimamo na mitazamo yetu dhidi yao? Hivi kwa uzembe wa kupoka demokrasia kwa taifa hilo kwenye kipindi cha Trump kutamfanya Biden anyooshee kidole taifa lolote la Afrika kuhusu demokrasia?

Kimsingi itabidi kwanza wapambane na maapungufu yao kabla ya kutoa jicho Afrika. Ni wazi uozo huu utawachukua muda sana. Marekani kwa muda mrefu sana ilizoea kuingilia masuala ya kisiasa, uchumi na utawala wa mataifa mengine mengi ulimwenguni huku muathirika mkubwa likiwa Bara la Afrika. Imani yangu ni kwamba kwa hali ilivyo Marekani sasa Biden atahitaji kuwa makini sana kwenye maneno yake atakayotaka kusema kuhusu Afrika.

Katika Uchaguzi wa Uganda uliopita, nilifurahishwa sana na kilichofanywa na Rais Museveni alipozuia mitandano ya kijamii kuingilia uchaguzi wa nchi hiyo. Ni wazi kwamba Robert Kyagulanyi mgombea wa upinzani alitegemea msaada mkubwa kutoka Marekani katika uchaguzi huu lakini Rais Museveni alikabiliana nao bila hofu na hoja yake ya msingi ilikuwa ni ujinga uliotokea Washngton usijeletwa Uganda. Je, huu ndo uwe msimamo wa Afrika kwa sasa?

Kwa sasa kazi kubwa ya Biden itakuwa ni kusafisha uozo wa Trump mtangulizi wake. Je, ataweza kufuta uozo wote na kumaliza makovu aliyowasababishia Waafrika kwa kipindi cha miaka minne? Pengine atatumia kisingizio cha kuwa na makamu wa rais Mwafrika akiwa ndio mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Afrika kushika nafasi hiyo kwenye taifa hilo kubwa.

Ni wazi kwamba mataifa yote 54 ya Afrika hayajawahi kuwa na sauti moja kubwa ya kusikika kwenye ulimwengu wote japokuwa kila taifa lina kiti kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa.

Hali hii inakuwa ngumu kwa Waafrika kwa kuwa kila taifa linazungumza lugha yake na hivyo kukosa ajenda moja ya msingi ya kuhusu maendeleo ya bara hilo. Je, hii ndiyo nafasi ya msingi ya kutumiwa na Waafrika kufikisha sauti yao kwa ulimwengu? Je, Biden ataruhusu jambo hili kufanikiwa?

Pengine, inawezekana wimbo huu wa umoja wa Afrika utakuwa unaimbwa na viongozi wachache katika bara kwa kuwa wengi wanalenga matumbo yao wenyewe. Imani yangu isiyo na kificho ni wazi kwamba Magufuli ana wimbo huo ndani mwake, Museveni ana wimbo huo pia, Je, mataifa mengine? Suala la sauti ya Afrika kwenye mataifa yote ulimwenguni ni muhimu sana.

Lakini sauti hii haiwezi kupatikana kupitia kwenye vikao vya mwaka vya Umoja wa Mataifa. Kuna umuhimu wa Waafrika kuonesha uhitaji wa muungano huu na kuondoa tofauti za kimipaka baina ya mataifa yetu na kuanza kuunganisha nguvu katika kulijenga bara letu.

Wakati Marekani inapambana na kurejesha heshima walioipoteza, sisi tuunganishe nguvu katika kuungana ili kupambana dhidi ya uonevu kwa bara letu na kusubiri kupangiwa jinsi ya kuishi na mataifa yaliyoshiriki katika kutawala bara letu na hadi sasa wanaendelea kwa njia tofauti.

Siamini kama hiki ni kipindi cha Afrika kuwa na matumaini makubwa kwa utawala wa Biden kwa kuwa lazima atalinda maslahi ya taifa lake ambapo moja kubwa ni kuhakikisha linabaki kuwa taifa tajiri kwa mataifa mengine duniani.

Kama Waafrika huu ni wakati wa kuimarisha muungano wetu kwa maslahi ya vizazi vilivyopo na vijavyo. Kufanya hivi tutakuwa tumejibu kiu ya wazee wetu akiwemo Mwalimu Julius Nyerere (Tanzania), Kwame Nkrumah (Ghana), Nelson Mandela (Afrika Kusini) na wengineo wengi. Huu si wakati wa viongozi wa Afrika kuweka masikio yao sawa kusikia Biden atatoa misaada kiasi gani kwa Afrika badala yake watumie nafasi hii kujiimarisha kiuchumi kwa maslahi mapana ya bara hilo.

Nafurahishwa sana na maeneno ya Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli ya kutaka Watanzania kufanya kazi kwa nguvu na akili zote ili kuleta maendeleo taifa hili lililoshamiri kwa amani.

Magufuli anaamini kabisa kwamba maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla hayawezi kuletwa na watu wengine isipokuwa wao wenyewe. Maneno haya hayatofautiani na ya Rais Museveni aliposema uzalendo wa kweli ni kuwa na mapenzi mema kwa Afrika, Afrika Mashariki na Uganda kama Taifa. Basi ni wakati sasa Afrika ifute mawazo ya utegemezi na kujijenga yenyewe kwa kuwa na mipango mikakati mikubwa.

Mwandishi anapatikana kwa mawasiliano haya: +255 712 246 001; flugeiyamu@ gmail.com

Columnist: habarileo.co.tz