Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kuna inzi anasumbua usoni mwa Harry Kane, tuendelee kusubiri

Harry Kane Bundasliga Kuna inzi anasumbua usoni mwa Harry Kane, tuendelee kusubiri

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ni Krismasi sasa hivi. Msimu wa Krismasi. Barafu inaanguka kule Ulaya. Ujerumani inaaguka hasa. Wenzetu huwa wanasiamisha Ligi zao kwa mapumziko mafupi ya kupisha kumwagika kwa barafu. Ni rafiki zetu Waingereza tu huwa hawasimamishi.

Harry Kane yupo likizo yake ya kwanza sasa hivi ya baridi tangu aanze kucheza soka. Hajawahi kuzoea hali hii. Amekwenda Ujerumani amekumbana na hali hii. Wote tunajua kwanini alihamia Ujerumani kutoka Tottenham.

Harry hajawahi kutwaa taji lolote kubwa wala dogo pale England. Amejaribu kutafuta njia ya mkato ya kupata taji kwa urahisi. Wakati mwingine ukiwa mchezaji au kocha jibu linaweza kuwa rahisi tu. unahamia tu Bayern Munich pale Ujerumani.

Pale Ujerumani kwa muda mrefu sasa Bayern Munich wamekuwa ‘sterling’ wa Kihindi. Wanapiga kila mtu na wanashinda kila kitu. Wana uwezo wa kwenda sokoni wakafukuzwa na watu elfu moja na bado wasishikwe. Kwa mfano mpaka sasa wametwaa mataji 11 mfululizo ya Bundesliga. Tangu mwaka 2013 wamekuwa wakitwaa wao tu mfululizo.

Wana pesa na wana kila kitu. mchezaji mzuri akiibuka katika timu nyingine pale Ujerumani basi inakuwa kama vile ameandaliwa akacheze kwao. Na katika soko jingine la Ulaya bado wana uwezo wa kugombania wachezaji na akina Manchester City, Real Madrid, Manchester United, Chelsea, Arsenal na wengineo.

Kane kwenda Bayern Munich ilikuwa njia ya mkato kutwaa taji lake la kwanza kubwa katika maisha ya soka wakati huu akiwa ana miaka 30 huku akiwa ameionyesha dunia uwezo wake mkubwa wa kuziona nyavu za makipa.

Lakini kuna inzi ametokea na ameanza kurukaruka mbele ya uso wa Kane. Wakati yeye akiwa na uzingativu na anachofanya, huku akifunga mabao mengi kama kawaida, ghafla kuna inzi anaruka mbele yake akijaribu kumsumbua na kuharibu ndoto yake ya kutwaa taji kubwa la kwanza katika maisha yake ya soka.

Ghafla wametokea Bayer Leverkusen. Wana mtu anakaa katika benchi anaitwa Xabi Alonso. Unamkumbuka? Kiungo mahiri wa zamani wa Liverpool, Real Madrid, Bayern Munich na timu ya taifa ya Hispania. Ni kama inzi aliyeanza kuighasi sura ya Kane.

Alonso amefanya wizi ambao Mikel Arteta na makocha wengine wameufanya kwa Pep Guardiola. Ameuchukua mpira wa Pep na kuupeleka Ujerumani. Bayer Leverkusen wapo katika ubora wao wa kucheza soka la kisasa ambalo Pep analifundisha.

Msimu huu wamekuwa moja kati ya timu bora barani Ulaya. Wameishika Ligi Kuu ya Ujerumani mkononi. Mpaka sasa wanaongoza Ligi wakiwa na pointi 42 huku Bayern Munich wakishika nafasi ya pili na pointi 38 mkononi huku wakiwa na mechi moja kiganjani.

Labda kitokee kile ambacho kiliitokea Arsenal msimu uliopita lakini vinginevyo ndoto za Kane kutwaa taji lake la kwanza kubwa katika soka zipo hatarini. Kwa mpira wa Ujerumani ulivyo haionekani sana kama Bayer Leverkusen anaweza akapotea njia mpaka mwishoni wa msimu.

Anaweza kuharibu hapa na pale lakini ataendelea kuishikia kooni Bayern Munich mpaka mwishoni mwa msimu. Kuna timu pale Ujerumani huwa zinaongoza Ligi kwa muda mrefu halafu ghafla huwa zinapitwa na Bayern Munich kama zimesimama.

Kwa namna ninavyowatazama Bayer Leverkusen msimu huu sioni kama itakuwa timu ya namna hii. Bayern Munich itabidi wajipange kweli kweli kumpatia Kane taji lake la kwanza kubwa. Haya yanaendelea huku Bayern wenyewe wakiwa wamepungua makali. Ni vile tu kwamba walitengeza pengo kubwa kati yao na timu nyingine. Ni kama msimu uliopita wakati walipochukua ubingwa katika siku ya mwisho ya msimu kutokana na ujinga wa Borussia Dortmund.

Tayari Bayern wameshatolewa katika michuano ya DFB Pokal ambayo ni kama FA ya Ujerumani. Wametolewa na timu ya daraja la tatu iitwayo Saafbrucken. Wanadamu wanaoamini katika nyota wanaamini kwamba Harry Kane amewapelekea gundu Bayern kwa kutolewa na timu hii.

Kwamba labda ni mwendelezo wa mataji kumkimbia Kane. Lakini pia Kane ana taji la Ligi ya mabingwa wa Ulaya. Unapochunguza kwa makini sio lazima Bayern Munich itwae taji hili. Hawajatwaa siku nyingi na hawana ulazima sana wa kulitwaa. Kuna wababe wengi Ulaya kuliko Ujerumani ndio maana hawajalitwaa muda sasa.

Ubingwa wa lazima kwao ni Bundesliga. Huu ndio ubingwa ambao hata wachezaji wa kawaida wameudoea kuupata pale tu walipojiunga na Bayern. Ndio ubingwa ambao jaribu kufikiria kwamba Pep Guardiola aliuchota kwa misimu yote mitatu aliyokuwa pale lakini alishindwa kutwaa taji la Ligi ya mabingwa wa Ulaya.

Na sasa Kane analazimika kupambana na Alonso kwa ajili ya kutwaa taji lake la kwanza kubwa la soka duniani. Kane anaifanya kazi yake kwa ufasaha sana. Anafunga kama mwehu. Anafunga kama kawaida. Tatizo lake kubwa ni Alonso.

Na endapo kama Bayer Leverkusen itatwaa ubingwa mbele ya Bayern Munich basi itakuwa kama vile Kane amepeleka gundu lake Ujerumani. Inakuaje katika msimu wake wa kwanza tangu atue klabuni hapo ndipo Bayern Munich inapokosa taji lake la kwanza la Bundesliga tangu mwaka 2013?

Kwa namna nilivyo mnafiki kuna mambo mtatu nilikuwa natamani yatokee halafu hayawezi kutokea kwa pamoja. Nilikuwa natamani Kane atwae ubingwa wake wa kwanza kwa sababu anastahili. Amepoteza mabao mengi bure pale Tottenham Hotspurs na nisingependa apoteze mabao yake bure pale Bayern Munich.

Lakini hapo hapo sipendi utawala uliopitiliza wa Bayern Munich pale Ujerumani. Ligi yao haisisimui tena. Tunapenda ligi ambazo watu wanabadilishana mataji. Akichukua mmoja kwa muda mrefu huwa inakera na mashabiki wengi wanaamua kuipa kisogo ligi ya namna hiyo.

Lakini hapo hapo kwa sisi mashabiki wa soka tunapenda mpira mzuri ushinde. Haishangazi kuona wengi wetu ni mashabiki wa Manchester City kimya kimya. Tunapenda timu zetu zicheze kama Manchester City basi tu tunakosa namna.

Acha mpira utembee. Acha mpira mzuri ushinde. Hatutamani kuona tena makocha kama Jose Mourinho wakijitokeza katika soka. Makocha ambao wanashinda bila ya mpira mzuri. Roho nyingine ya kinafiki inaniambia acha Leverkusen achukue ubingwa na mpira wake mzuri.

Columnist: Mwanaspoti