Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kuna haja ya kocha mpya Simba?

Kocha Mbrazil Kuna haja ya kocha mpya Simba?

Tue, 3 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sina tatizo na Kocha Roberto Oliveira kutua Msimbazi. Sina tatizo kabisa, lakini ni kweli Simba wanahitaji kocha mpya? Jibu langu ni hapana. Juma Mgunda ni kocha mzuri sana. Juma Mgunda alipaswa tu kuongezewa nguvu kwenye kikosi chake na kwenye benchi la ufundi.

Nimejaribu kuangalia nyuma ya Kocha wa Manchester United, Erik Ten Hug nimegundua kuwa anasaidiwa na makocha 20. Maana yake benchi la Ten Hug lina watu 21.

Pep Guardiola ni fundi kweli wa mpira lakini nyuma yake ana wasaidizi tisa. Benchi la Manchester City lina jumla ya watu 10. Benchi la ufundi Arsenal linaongozwa na Mikel Arteta, lakini nyuma yake kuna wasaidizi 12. Nyuma pale Arsenal wako wanaume 13. Pale nyuma ya Juma Mgunda kuna makocha wangapi? Wanahesabika kwa vidole.

Kocha mkuu anapaswa kuwa na wasaidizi wengi wa daraja la juu. Yeye anapaswa kuwa mtoa ramani ya vita kisha wasaidizi wake wanatekeleza. Anapaswa kuwa bosi wa timu sio mpanga koni uwanjani. Kocha mkuu hatakiwi kuwa mbeba maji ya wachezaji. Huu ulikuwa muda wa kumfanya Mgunda kuwa bosi. Huu ulikuwa muda wa kumuweka juu Mgunda.

Kocha wa Bayern Munich, Julian Nagelsmann siku moja aliwahi kusema ufundishaji mpira kisasa unahitaji mambo makubwa mawili tu - uhusiano mzuri wa kocha na wachezaji wake uwe kwa asilimia 70 na ufundi wa kocha uwe 30.

Mgunda ni mmoja wa makocha wenye kupendwa na wachezaji. Tazama tangu ameichukua Simba karibu kila mchezaji ana furaha. Karibu kila mchezaji anapata dakika za kucheza. Anafahamu mpira wetu. Anafahamu utamaduni. Anaifahamu vizuri Simba.

Nilidhani ni wakati wa kuongezewa zaidi nguvu. Nilidhani ni wakati wa kuongezewa watalaamu kwenye benchi lake la ufundi. Sina tatizo na kocha Roberto Oliveira na wala kocha mwingine yeyote lakini sidhani kama Simba wanahitaji kocha mpya kwenye kipindi hiki. Ukileta mtaalamu wa kuchambua mechi, ukimpa mtaalamu wa video, ukimpa mtaalamu wa viungo, Mgunda anaweza kukufikisha nchi ya ahadi.

Mgunda anahitaji zaidi kupewa wachezaji wa daraja la juu wawili tu kwenye kila nafasi.

Simba ni kama ina kikosi cha kwanza tu. Ukitazama kwenye benchi huoni mtu anayeweza kuja kuleta maajabu uwanjani. Simba inahitaji kuwa na wachezaji walau wawili wanaokaribiana ubora katika kila nafasi uwanjani.

Leo ukimkosa Mohammed Hussein, huoni mbadala wake. Leo ukimkosa Clatous Chota Chama walau utasema kuna Saido Ntibazonkiza. Vipi ukimkosa Moses Phiri? Kama Simba watatulia na kuongeza nguvu walau ya wachezaji wanne wa

nguvu na Mgunda kuongezewa nguvu, mwakani hawashikiki.

Ni kweli Simba inahitaji kocha mpya? Jibu langu ni hapana. Huu ni muda wa kumuongezea Mgunda nguvu na sio muda wa kumletea kocha mpya. Huu ni muda wa kuongeza wachezaji kama watano hivi wa maana, kisha tumuache Mgunda apige kazi. Sina tatizo na makocha wa kigeni, lakini wakati mwingine timu zetu zinajirudisha nyuma sana. Kila siku huanza upya. Haina afya sana kwa klabu.

Simba chini ya Mgunda boli linatembea. Kiwango kizuri kimataifa ni ishara tosha kwamba kocha akiongezewa nguvu kwenye benchi la ufundi na wachezaji, Simba wanaweza kuwa pazuri sana msimu ujao. Tusikariri kwamba siku zote Watanzania ndio wawe wasaidizi wa makocha Wazungu. Simba leteni Wazungu hata watano wafanye kazi chini ya Mgunda. Waleteni wamsaidie. Mgunda tayari ana ramani ya vita.

Mgunda tayari ameleta morali ndani ya timu. Kumleta kocha mgeni ni kujirudisha nyuma. Mgunda angeaminiwa walau mpaka mwisho wa msimu tayari tungeona mwelekeo wake. John Bocco ambaye tayari alikuwa anapotea kaibuka upya baada ya kupewa nafasi na Mgunda. Chama naye alirudi Simba akiwa hoi. Akiwa amechoka lakini chini ya Mgunda ni kama amezaliwa upya. Natamani kuona Mgunda akiendelea kuwa kocha mkuu Simba.

Columnist: Mwanaspoti