Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kuna John Bocco mmoja tu

Bocco Bao 3 John Bocco

Fri, 25 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mabao matatu aliyafunga John Bocco kwenye ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Ruvu Shooting yameendelea kumuweka pazuri kuifikia rekodi ya Mohamed Hussein ‘Mmachinga’.

Bocco ambaye ni nahodha wa Simba amebakiza mabao manane kufikia rekodi ya Mmachinga aliyefunga mabao 153 ndani ya misimu 13 akizichezea Bandari Mtwara, Yanga, Simba, Mmbanga FC na Twiga Sports.

Bocco hadi sasa amefunga mabao 145 ndani ya misimu 15 akicheza Azam FC na Simba, huku akiwa na rekodi yake nzuri ya kutupia kila msimu.

Katika misimu 15 ya kucheza soka Ligi Kuu Bara, Bocco ametengeneza rekodi ya kufunga kila msimu na kumfanya afikishe jumla ya mabao 145 hadi sasa. Hat trick dhidi ya Ruvu Shooting imemtofautisha na wachezaji wengine wa kizazi cha sasa. Washambuliaji wamekuwa wakiibuka kwa kasi na kupotea ghafla kwenye ramani ya ushindani huku Bocco akiendelea kuonyesha ukomavu.

Hapa tunazungumzia mabao ya Ligi Kuu Bara na hatujaorodhesha yale ya Kombe la FA, Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi, Kombe la Kagame au Timu ya Taifa ya Tanzania.

Mwanaspoti linakuorodheshea misimu 15 ya Bocco katika Ligi Kuu na idadi ya mabao aliyofunga na kumfanya asiwe na mpinzani mbele ya wenzake.

KAZI IMEANZA

Jumamosi iliyopita wakati Ligi Kuu ikiendelea, Bocco alituma salamu baada ya kukosekana kwenye mechi sita kati ya 12 ilizocheza Simba akianza dhidi ya Ruvu Shooting akatupia kambani mabao matatu timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Bocco alikosekana kwenye mechi dhidi ya Geita Gold, Kagera Sugar, Tanzania Prisons, Singida Big Stars, Ihefu FC na Mtibwa Sugar. Lakini alianza mechi mbili dhidi ya Dodoma Jiji ambayo ilichezwa Oktoba 2 na Ruvu Shooting na kutupia mabao matatu, huku dhidi ya Yanga, Azam FC, Namungo na KMC akianzia benchi.

Kitendo cha Bocco kufunga mabao matatu na kufikisha mabao 145 kwa misimu 15 mfululizo wengi wanajiuliza, nyota huyo ndio kazinduka, je, nini kitakachofuata?

Ni suala la kusubiri na kuona, japokuwa mwenyewe amesisitiza kiu yake ni kurudisha taji la Ligi Kuu Msimbazi kisha mengine yafuate.

“Natamani kuisaidia tena Simba kurudisha taji tulilopoteza msimu uliopita na mataji mengine, naamini hata mafanikio yangu binafsi yatajiseti tu yenyewe,” anasema Bocco. Anasema ligi ndio kwanza imeanza hivyo, mashabiki wa Simba na wale wanaoipenda timu yao waendelee kuwasapoti, ili wawape raha kwa kuamini msimu huu ni moto zaidi kuliko uliopita.

MAMBO MAGUMU

Majeraha ya mara kwa mara yalimuandama Bocco msimu wa 2021-22 na kumfanya ashindwe kuonyesha makeke yale, japo hakutoka patupu, kwani alizitumia nafasi chache alizopata kucheza msimu huo wa 14 kwake kwa kufunga mabao matatu, huku tuzo ya mfungaji bora ikienda kwa George Mpole anayekipiga Geita Gold aliyekwamisha wavuni mabao 17.

Majeraha hayajamuacha salama hadi msimu huu ambao amekuwa akianzia benchi na muda mwingine kukosekana kwenye kikosi cha Simba ambacho kinaongozwa na mshambuliaji Moses Phiri ambaye tayari ametupia mpira nyavuni mara sita.

REKODI ZAKE

2008-2009 (bao 1), 2009-2010 (14), 2010-2011 (15), 2011-2012 (19), 2012-2013 (7), 2013-2014 (7) na katika msimu huu ndipo alipotwaa taji lake la kwanza la Ligi Kuu akiwa na Azam.

Mabao yake mengine ni ya msimu wa 2014-2015 (3), 2015-2016 (12), 2016-2017 (10) uliokuwa wa mwisho kuitumikia Azam kabla ya kuhamia Simba 2017-2018 (mabao 14), 2018-2019 (15), 2019/20 (9) na 2020/21 (16), 2021/22 (3) na 2022/23 hadi sasa amefunga mabao (3). Bocco aliachana na Wana Lambalamba akiwa ameacha mabao 88 msimu wa 2011/12 ndio alifunga mabao mengi zaidi akiingia kambani mara 19 na kwa Simba ni mabao 16 msimu wa 2020/21 na ambapo msimu aliofunga mabao machache ni 2008/9, bao moja.

REKODI ZA MMACHINGA

Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ alianza 1993 akafunga mabao 13, 1994 (20), 1995 (21), 1996 (14), 1997 (12), 1998 (26), 1999 (11), 2000 (13), 2001 (4), 2002 (3), 2003 (5), 2004 (4), 2005 (7).

Mabao hayo aliyafunga wakati akichezea Bandari Mtwara, Yanga, Simba, Mmbanga FC na Twiga Sports.

Columnist: Mwanaspoti