Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kumtoa Nsajigwa Uwanja wa Mkapa lilikuwa kosa

Uwanja Wa Mkapa Kumtoa Nsajigwa Uwanja wa Mkapa lilikuwa kosa

Wed, 1 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna msemo maarufu katika lugha mbalimbali duniani, ambao kwa Kiswahili unasema 'Ulichonacho hujui thamani yake hadi usiwe nacho.'

Hiki ndicho kimelikuta taifa la Tanzania baada ya uwanja pekee wenye hadhi ya CAF na FIFA, Benjamin Mkapa, kufungiwa.

Zilianza kama tetesi na hatimaye imekuwa kweli baada ya Kaimu Mkurugenzi wa michezo, Ally Mayay, kuthibitisha mbele ya vyombo vya habari.

Tangu uzinduliwe na kutumika kwa mara ya kwanza mwaka 2007, Uwanja wa Mkapa umekuwa bora siku zote kiasi cha kuwa mfano kwa wengine.

Timu kadhaa kutoka nje ya Tanzania zimekuja kuchezea hapa mechi zao za kimataifa baada ya viwanja vyao kufungiwa.

Lakini sasa, timu za Tanzania itabidi kutafuta viwanja vya kuchezea nje ya nchi, yaani ghafla tu Tanzania iliyokuwa kimbilio la wakimbizi, na yenyewe inaanza kutafuta hifadhi.

Naam, Uwanja wa Mkapa umefungiwa na CAF kwa kukosa sifa. Mwanzoni mwa Februari, siku ambayo Simba walicheza na Al Hilal ya Sudan, kulikuwa na taarifa zilizotolewa na gazeti hili kuhusu uchafu kwenye uwanja huo.

Serikali ikatoa waraka mrefu kupinga taarifa ile lakini ukisoma vizuri waraka ule, utaona kwamba kweli tatizo lilikuwepo ila serikali ilitaka kuficha.

Serikali ilisema picha zilizotumika kwenye taarifa ile zilikuwa za mwaka 2020, lakini ikakiri kwamba tatizo lile lipo na ikasema imekuja na mapendekezo manne ili kuondokana na hali ya uchafu, na isiwe uwanja wa taifa pekee, bali viwanja vyote vinavyomilikiwa na CCM nchi nzima.

ULICHONACHO

Tatizo la uwanja wa Mkapa lilianzia Agosti 9 mwaka 2022 pale aliyekuwa Waziri wa Utamaduni na michezo, Mh. Mohamed Mchengerwa, alipomuagiza aliyekuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, Dkt Hassan Abbasi, kumtoa kwenye nafasi yake meneja wa uwanja huo Gordon Nsajigwa.

Ni kweli kwamba uwanja kama taasisi, uwanja wa Mkapa ulikuwa na changamoto zake, lakini hata hivyo kwa asilimia kubwa zilitokana na madhaifu yaliyoanzia juu.

Hata hivyo, haikuwahi kutokea hata mara moja matatizo hayo kuwa makubwa kiasi cha uwanja kufungiwa. Lakini miezi 7 baadaye, uwanja unakosa sifa na kufungiwa na CAF.

Maana yake ni kwamba meneja mpya aliyechukua nafasi ya Nsajigwa ameshindwa kazi yake.

Sasa ndiyo tunajua thamani ya Nsajigwa baada ya kuwa ameondoka. Wakati akiwepo, alichukuliwa poa tu, sasa hayupo ndiyo tunaona haya mazonge zonge.

Watu kuondolewa kazini kwenye nafasi zao ni jambo la kawaida lakini ni lazima kuhakikisha anayekuja badala ya anayetoka, ni maridadi vya kutosha kuifanya kazi hiyo.

Haya mambo ya kuamka asubuhi na kumtoa mtu kisa umemchoka, yanalipeleka taifa pabaya.

Kufungiwa uwanja wa Mkapa ni aibu kwa taifa na aibu kwa mwenye jina. Mzee Mkapa amejipumzikia huko, lakini jina lake linachafuliwa kirahisi tu kwa watu kushindwa kuwajibika.

Yawezekana ndiyo maana mwenyewe katika uhai wake alikataa jina lake kutumika uwanjani pale.

Labda aliyajua haya, jina lake safi na lenye sifa kuhusishwa na vitu visivyo na sifa au ndiyo yale ya Magufuli kukataa jina lake kutumika kwenye stendi ya Mbezi kwa sababu kama hizo hizo.

Tunapotoa majina ya watu wenye heshima zao kwa vitu vyetu, tuvitunze kuwaenzi wenye majina yao.

Wenyewe waliyajenga na kuyalinda haya majina, leo tunayatumia vibaya na kuyachafua...siyo sawa. Siyo haki. Siyo uungwana! Uwanja wa Mkapa ndiyo pekee unaomilikiwa na serikali kupitia wizara ya michezo, lakini uko katika hali mbaya.

Vipi kama wizara ingemiliki viwanja angalau 10, si ndiyo ingekuwa balaa kabisa?

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ana ndoto ya kuandaa AFCON 2027. Ndoto hii itafanikiwa kweli kwa utendaji wa namna hii? Kwa wasaidizi kama hawa ambao kuutunza uwanja wa Mkapa tu changamoto, wataweza kusimamia miradi mikubwa itakayofanikisha Tanzania kuwa na sifa za kuandaa AFCON?

Maana wizara inayosimamia uwanja wa Mkapa ndiyo hiyo itakayokuwa msaidizi namba moja wa Rais kwenye kampeni za kuandaa AFCON, itaweza?

Wizara ina watu wenye uwezo kweli, kama kutoka Nsajigwa tu, tayari pengo linaonekana, au ndiyo maana Raia alifanya mabadiliko kwenye wizara hii? Waziri na karibu wake wote wakatoka, yawezekana kuna makubwa zaidi aliyaona.

Sasa wizara ina Waziri mpya na katibu mpya, fanyeni kazi kutuondolea aibu hii. Na kama kuna uwezekano, mrudisheni Nsajigwa alisaidie taifa, hakuna aibu wala dhambi kumrudisha kazini, hiyo hutokea hata kwenye ndoa.

Watu hutalikiana na baadaye kurudiana na kusonga mbele. Ukigundua umekosea, patia kuanzia kuanzia hapo, kufanya kosa siyo kosa bali kurudia kosa. Kuanguka siyo dhambi, bali kuendelea kubaki chini.

Misemo yote hiyo inahalalisha kurekebisha makosa yaliyofanyika, kwa sababu kufanya makosa ndiyo ukamilifu wa ubinadamu.

Uwanja wa Mkapa ni tunu ya taifa, tuilinde. Tuwape dhamana ya kuuhudumia watu wenye uwezo, na tuwalinde, tusikubali kuwahukumu kwa majungu.

Columnist: Mwanaspoti