Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kule Qatar tunatoboa Waafrika?

Morocco Rrrrrr Kule Qatar tunatoboa Waafrika?

Thu, 1 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mwaka 1990, Cameroon ilikuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia. Ulikuwa ni mwanzo mzuri sana kwa Waafrika. Cameroon walikuwa na mwanzo mzuri baada ya kuanza michuano hiyo kwa kishindo. Unajua walianza kwa kumfunga nani? Walikuwa ni Argentina.

Moja kati ya wababe wa dunia kutoka Amerika Kusini. Argentina ilifungwa bao 1-0 na maisha ya Waafrika yakasonga mbele. Ilipita miaka 12 kupata timu nyigine kutoka Afrika kutinga robo fainali. Senegal 2002 walikuja kuliheshimisha Bara la Afrika. Walianza mbio zao kwa kuuchapa Ufaransa. Haikuwa kazi rahisi.

Sio jambo la kusahaulika hata kidogo. Walichofanya Senegal 2002 ni kama walichofanya Saudi Arabia kwa Argentina mwaka huu. Ufaransa ilikuwa ni bingwa mtetezi wa Kombe la Dunia. Ufaransa ilikuwa imesheheni mastaa kila kona. Senegal walikwenda mpaka robo fainali. Afrika ililazimika tena kusubiri kwa miaka minane kupata robo fainali nyingine. Ilikuwa ni Ghana pale nchini Afrika Kusini.

Walianza kwa kuichapa Serbia bao 1-0. Afrika ikapewa heshima kubwa. Ni kwa mara ya kwanza Afrika tulikuwa wenyeji wa michuano hiyo. Sasa ni miaka 12 tangu tulipotinga robo fainali kwa mara ya mwisho. Kuna dalili yoyote ya kwenda kuandikisha rekodi mpya mwaka huu Qatar?

Nilipotazama mechi ya kwanza ya Senegal dhidi ya Uholanzi nilisikitika sana. Dakika nane za mwisho Senegal ikapoteza kwa mabao 2-0! Ni makosa yaliyozoweleka Kwa Waafrika. Kuna kitu kwenye akili za Waafrika lazima kitoke.

Ni kweli wawakilishi wote watano wa Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia wana zaidi ya 85 ya wachezaji wanaocheza soka Ulaya, lakini bado wana tabia sawa kabisa na wachezaji wanaocheza Afrika. Sina nia ya kuwakosea heshima.

Sina nia ya kubeza mchango wao. ni kama kuna kuridhika na vitu vidogo. Kuna nanma moto unakata mapema. Kuna katabia ka kupoteza umakini kabla ya mechi haijaisha. Huu ndiyo ugonjwa wetu. Wachezaji wengi akilini wanamaliza mechi kabla ya dakika 90. Umakini unapungua dakika za mwisho tunaumia. Tunafungwa mabao rahisi. Ni-metazama me-chi ya kwa-nza ya Ghana na Ureno majanga ilikuwa ni matupu. Nafasi walizotengeneza Ghana Ureno wasingechomoka. Ureno wangekufa tu.

Kulikuwa na penalti ya mchongo aliyofunga Cristiano Ronaldo, lakini bado wasingetoka. Basi walau hata sare, lakini Ghana ikapoteza. Kuna wakati ni kama tumerogwa. Kuna muda ni kama tuna mapepo tunatembea nayo uwanjani. Sifa pekee kwa mzunguko wa kwanza ni sare walizopata Morocco na Tunisia. Hizi sare hazikupaswa kuwa jambo la kujivunia hata kidogo. Tulistahili matokeo mazuri zaidi ya hayo. Hongera sana kwa Morocco, Ghana na Senegal, mechi za pili mmeuwasha moto kwelikweli. Lakini Tunatoboa kweli Waafrika pale Qatar?

Hili ni Kombe la Dunia ambalo Saudi Arabia kamfunga Argentina. Hili ni Kombe la Dunia ambalo Iran kamfunga Wales. Hili ni Kombe la Dubai ambalo Ujerumani kafungwa na Japan! Sio aina ya matokeo ambayo watu wa mpira waliyatarajia. Sio aina ya matokeo ambayo wengi walidhani yatatokea. Lakini mbona sio kwa timu za Afrika? Sina jibu.

Hongera Tunisia na Morocco kwa kutofungwa mechi za kwanza. Hongera pia Cameroon, Senegal na Morocco, lakini hayo hayapaswi kuwa malengo ya Afrika. Tunahitaji kwenda nusu fainali. Tunahitaji kwenda fainali. Tunahitaji kutwaa ubingwa.

Tumekuwa wasindikizaji sana. Tumekuwa vibonde sana. Ufike wakati malengo yetu ni lazima yawe kutwaa ubingwa. Imetosha kuridhika na vitu vidogo. Inatosha kushangilia mataifa ya wenzetu.

Msimu huu tumekwenda Qatar watu wengi tukiamimia Senegal, Cameroon na Ghana watafanya makubwa, lakini hata waliotoa sare mzunguko wa kwanza ni Tunisia na Morocco. Ni nje ya matarajio. Ni tofauti na mipango. Mchezo wa mpira wa miguu haupaswi kuendeshwa kwa namna hii. Hatutakiwa kuwa watu wa kubahatisha.

Nilidhani kuwa mwaka huu tunaweza kupata timu mbili zinazoenda nusu Ffainali Kombe la Dunia. Kumbe bado tunatakiwa kupata timu mbili za kwenda robo fainali? Aisee. Kumbe bado kazi ipo. Huku siko ambako Waafrika tunapaswa kuwepo. Huku sio daraja letu. Afrika ni zaidi ya hapa.

Uwepo wa wachezaji wengi wanaocheza Ulaya kwenye timu zetu bado hawaleti utofauti mkubwa tunapocheza timu za Ulaya. Tuko kwenye dunia ambayo mpira umekua kila kona, lakini Afrika bado kuna mambo yaleyale. Tunatoboa kweli Qatar? Sina uhakika.

Nawatazama Morocco. Nawatazama Tunisia. Sina uhakika. Labda Cameroon. Labda Senegal. Sina uhakika. Nadhani kuwa na wachezaji tu wanaocheza Ulaya bado haitoshi. Kujitolea kwao na umakini uwanjani hasa wanapokuwa na jezi za timu za Taifa kuna muda hakulingani na uwezo wao mkubwa tunaowaona nao wakiwa na klabu zao za Ulaya. Haijakaa vizuri. Haiko sawa. Afrika bado ni presha tupu. Hatuna uhakika na timu yoyote mpaka sasa. Ni kweli Cameroon, Ghana na Morocco wako pazuri, lakini kuna hata mmoja wetu anayeona mwanga wetu hapo kesho? Usinipe jibu.

Columnist: Mwanaspoti