Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kukosea Majina sio kosa la mgombea kuwekewa pingamizi

101155 Uchaguzi+pic Kukosea Majina sio kosa la mgombea kuwekewa pingamizi

Wed, 10 Nov 2021 Chanzo: Habarileo

UCHAGUZI ni mchakato wa watu kumchagua mtu au watu watakaojaza nafasi kwenye ofisi ya umma ili kuwawakilisha katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Kwa mujibu wa Encyclopedia Britannica uchaguzi ni mfumo rasmi unaohusisha mchakato wa kumchagua mtu kwa ajili ya kushika nafasi kwenye ofisi ya umma au kukubali au kupinga pendekezo la kiutawala (political proposal) kwa kupiga kura.

Uchaguzi katika mfumo wa utawala unaweza kutumika kujaza nafasi kwenye bunge, serikali kuu, mikoa na serikali za mitaa.

Kwa muktadha wa Tanzania uchaguzi haswa wa kujaza nafasi kwenye utawala wa umma ngazi ya kata, jimbo na urais unaratibiwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na ushindani uliosawia, huru na wa haki, Tume inahakikisha kwamba mchakato wote kuanzia ngazi ya uteuzi wa wagombea, kampeni na hata siku ya kupiga kura unasimamiwa na kuratibiwa kikamilifu.

Hivi karibuni Tume imetangaza nafasi wazi ya ubunge katika Jimbo la Ngorongoro mkoani Arusha na kata sita za Tanzania Bara ambapo kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, wagombea wanachukua fomu kuanzia Novemba 9 (jana) hadi 15, mwaka huu.

Siku ya uteuzi itakuwa Novemba 15 mwaka huu na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Novemba 16 hadi Desemba 10 mwaka huu na siku ya uchaguzi itakuwa Desemba 11, mwaka huu.

Kata zilizotangazwa kufanya uchaguzi mdogo ni pamoja na Bomalang’ombe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Nyabulanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’wale na Ipwani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

Nyingine ni Likombe iliyopo Halmashauri Manispaa ya Mtwara, Handali katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Nalasi Mashariki iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na Naumbu iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Ikumbukwe kwamba katika ngazi ya uteuzi wa wagombea NEC kwenye tarehe iliyopangwa itafanya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi ambao wamependekezwa na vyama vyao na watatakiwa kuwasilisha fomu za uteuzi katika ofisi za Tume kabla ya muda uliopangwa siku hiyo ya uteuzi.

Ikumbukwe kwamba ili kuepuka makosa ambayo yanaweza kumnyima mgombea fursa ya kuteuliwa kwa kuwasilisha Tume fomu iliyokosewa au ambayo haijakizi vigezo vya kuteuliwa, mgombea anapewa fursa ya kupeleka fomu yake kwa msimamizi wa uchaguzi siku tatu kabla kwa ajili ya kukaguliwa na kuona kama fomu yake imekidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria.

Mada hii ni muhimu kufahamika vizuri haswa katika kipindi hiki ambapo Taifa linashuhudia chaguzi ndogo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za wabunge na madiwani kujiuzulu, kuhama vyama au kufariki.

Kwa kuwa chaguzi hizi ndogo zinahusisha wabunge na madiwani, makala hii inaangazia zaidi taratibu za kufuatwa katika teuzi za wagombea kwa nafasi hizo.

Kwa nafasi ya mgombea wa kiti cha ubunge, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo anao wajibu wa kumteua mgombea wa nafasi ya ubunge baada ya kujiridhisha kuwa fomu ya uteuzi namba 8B na fomu namba 10 ya kuheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi zimejazwa kikamilifu.

Fomu namba 8B inapaswa kujazwa kwa herufi kubwa lakini ni jina moja tu ndilo linapaswa kuandikwa kwa herufi kubwa kwenye karatasi ya kupiga kura kwa hiyo mgombea anapaswa kujaza mwanzoni jina analopendelea liandikwe kwa herufi kubwa kwenye karatasi ya kupigia kura likifuatiwa na majina mengine.

Ikumbukwe kwamba baadhi ya wagombea huwawekea wenzao pingamizi haswa wanapoona kwamba mgombea ameandika majina yake kwa kutofuata mtiririko, jambo hili kwa mujibu wa sheria si kosa na halimnyimi mgombea sifa za kuteuliwa.

Kwenye fomu hiyo majina ya wadhamini yanapaswa kujazwa kwenye jedwali na baada ya hapo fomu inapaswa kuwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi pamoja na picha nne za mgombea za rangi zenye ukubwa wa passport (Passport size).

Pia fomu hiyo inapaswa kuwasilishwa pamoja na fomu namba 10 ya tamko la mgombea la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi.

Ili fomu hiyo ikamilike kwa ajili ya uteuzi inapaswa pia kuambatanishwa na uthibitisho wa chama cha siasa wa kumpendekeza mgombea ubunge, tamko la wadhamini, tamko la kisheria la mgombea ubunge na baada ya hapo itakamilishwa kwa kupata uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi.

Utaratibu wa kukata rufaa kwa mgombea ubunge upo kwa mujibu wa sheria, Kifungu cha 40 (6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kinatoa fursa kwa mgombea ambaye hakuridhishwa na uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi kukata rufaa Tume.

Uamuzi wa Tume kuhusu rufani hiyo utakuwa wa mwisho na hautahojiwa katika mahakama yoyote.

Kifungu cha 40(6) kinatoa fursa kwa asiyeridhika na uamuzi wa Tume kufungua malalamiko ya uchaguzi mahakamani baada ya matokeo ya uchaguzi wa wabunge kutangazwa. Baada ya uteuzi wa mgombea upande ambao haujaridhika unaweza kukata rufaa kwa kujaza fomu namba 12.

Kwa upande wa mgombea wa udiwani, uteuzi kwa mujibu wa kanuni ya 25 (4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (madiwani) hufanywa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi baada ya kujiridhisha kuwa mgombea amejaza kikamilifu fomu namba 8C ya uteuzi na fomu namba 10 ya kuheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi.

Masharti na mtiririko wa ujazaji unafanana na ule wa mgombea ubunge isipokuwa mgombea ubunge anaweka dhamana ya Sh 50,000 na mgombea udiwani anaweka dhamana ya Sh 5,000.

Utaratibu wa pingamizi dhidi ya mgombea udiwani upo kwa mujibu wa Kifungu cha 44 (3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, pingamizi kwa mgombea udiwani huwekwa na mgombea mwingine wa nafasi ya udiwani au msajili wa vyama vya siasa au msimamizi wa uchaguzi kupitia fomu namba 9C. Pingamizi husikilizwa na kuamuliwa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata baada ya kupokea pingamizi na kufanya uamuzi anatakiwa amfahamishe msimamizi wa uchaguzi juu ya uamuzi huo ili aupitie na kuona kama umezingatia sheria ama la.

Msimamizi wa Uchaguzi ana mamlaka ya kubadili uamuzi huo kama itabainika kuwa haukuzingatia matakwa ya kisheria. Fomu namba 9C hutumika kuwekea pingamizi.

Kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kinaruhusu wagombea kukata rufaa NEC kupinga uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi kuhusu pingamizi dhidi ya mgombea.

Tume hupokea rufaa na kuzitolea uamuzi. Uamuzi wa NEC ni wa mwisho na hautahojiwa na mahakama. Kifungu cha 44(5) kinatoa fursa kwa asiyeridhika na uamuzi wa Tume kufungua malalamiko ya uchaguzi baada ya uchaguzi kumalizika na mshindi kutangazwa. Fomu namba 12 hutumika kuwasilisha rufani.

Columnist: Habarileo