Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kombe la Yanga linaendaje Msimbazi?

Msimbazi Pic Kombe la Yanga linaendaje Msimbazi?

Thu, 15 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hivi kwanini Yanga hawajaenda Chamazi inakotoka Azam FC au Turiani inakotoka Mtibwa Sugar na matokeo yake kila paredi za ubingwa lazima wapite Mtaa wa Msimbazi yalipo makao makuu ya Klabu ya Simba?

Nafahamu Simba na Yanga ni watani wa jadi, lakini hiki kinachofanyika kwangu sio utani. Wakiwa uwanjani, mchezaji haruhusiwi kwenda kushangilia goli sehemu walipo mashabiki wa timu pinzani.

Haruhusiwi kwenda kuwatia hasira mashabiki wa timu pinzani. Ukifanya hivyo kuna adhabu unapigwa. Ukifanya hivyo kuna namna unataka waamuzi wa mchezo husika wakutie adabu. Hongereni Yanga kwa paredi la heshima ambalo mmekuwa mkilifanya kwa msimu wa pili sasa, lakini ndani yake naona kama kuna kaushamba flani hivi

Najua fika kama Msimbazi ni mtaa ndani ya Kariakoo. Najua pale ndipo lilipo chimbuko rasmi la Klabu ya Simba. Kwenda mpaka kwenye jengo lao na kuinua kombe pale ni uchokozi usio na sababu yoyote ya msingi.

Kuna makusudi flani Yanga wanafanya ambayo kwa maoni yangu ule sio utani wa jadi. Unaweza kuleta vurugu zinazoweza kuepukika mapema. Paredi ya ubingwa kwa Yanga ni jambo jema sana, lakini sioni lazima ya kwenda Mtaa wa Msimbazi na kuwakoga watani. Sioni sababu ya kwenda kuamsha hasira za mashabiki wa Simba.

Paredi ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara ya Yanga pengine inazidi ile ya Al Ahly ambao ndiyo mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Pengine ndiyo paredi bora zaidi Afrika kwa sasa lakini sioni sababu ya kupita Msimbazi.

Inaweza kuboreshwa zaidi lakini isipite Msimbazi. Mpira wakati mwingine una Kichaa chake. Kwenda makao makuu ya Klabu ya Simba na kuinua kombe sio sawa. Kwenda makao makuu ya Simba na kuwapa viongozi waliowahi kufanya kazi Simba kunyanyua kombe na kuwakoga mashabiki wa Simba ni kutafuta vurugu.

Sina tatizo hata kidogo na utani wa jadi, lakini katika hili naona kuna siku linaweza kuleta shida kidogo. Ukianzisha mambo kama haya kuna siku Simba watashinda taji watataka kwenda kukesha pale Jangwani.

Kuna siku Simba wakishinda ubingwa wataenda pale Salamander Tower kugawana medali. Sioni kama imekaa vizuri. Tunaweza kucheka leo, kwa msingi wa utani wa jadi, lakini baadaye kuna siku itasumbua kwa kuwa watu wataweka hasira vifuani. Hongereni Yanga kwa paredi bora kabisa Afrika, lakini Msimbazi sio lazima muende. Ukiniuliza nitakwambia Yanga wana paredi la ubingwa kubwa kuliko lolote Afrika, lakini siungi mkono hoja hadi nitakapojiridhisha.

Nilichogundua Yanga inaona ili furaha ikamilike ni lazima tu imkwaruze mtani. Mimi napenda utani wa jadi udumu, lakini usiwe ule unaoweza kuleta vurugu. Usiwe utani unaoibua fikra tofauti.

Hivi ni kwanini Yanga hawajaenda Chamazi inakotoka Azam FC au Turiani inakotoka Mtibwa Sugar na matokeo yake kila paredi zao za ubingwa lazima wapite Mtaa wa Msimbazi yalipo makao makuu ya klabu ya Simba? Kama una majibu tafadhali niandikie ujumbe mfupi kwa namba yangu hapo juu.

Yanga wangeweza kupeleka kombe kwenye matawi yao yote hasa ya Dar es Salaam. Yanga wangeweza kupeleka kombe hadi mikoani. Ndiyo namna bora ya kujitambulisha vizuri nchini. Kiukweli wanalielimisha taifa, lakini kwenda kushangilia nje ya makao makuu ya Simba ule ni uhuni. Kupeleka kombe pale Msimbazi ni kutafuta vurugu zisizokuwa na faida yoyote.

Ubingwa wa 29 tayari umetua Jangwani, lakini watasumbua sana. Alisikika mlevi mmoja akizungumza. Muda si mrefu hii itakuwa ajenda Afrika kwenye kushangilia ubingwa.

Siungi mkono hoja ya kwenda Msimbazi kuwakoga watani. Naiona haijakaa vizuri. Kila barabara nchini kiasili ina mashabiki na wapenzi wa Yanga, shida ni ipi kwenye kushangilia?

Kuna siku Simba itatwaa ubingwa hapa na kufanya jambo gumu zaidi nchini kwenye kushangilia. Kuna siku Yanga wanaonewa ofisini. Hivi ni kwanini Yanga hawajaenda Chamazi inakotoka Azam FC au Turiani inakotoka Mtibwa Sugar na matokeo yake kila paredi zao za ubingwa lazima wapite Mtaa wa Msimbazi yalipo makao makuu ya Simba?

Kwa mara nyingine tena asanteni sana Yanga kwa kuendelea kuongeza thamani ya kombe na ligi. Kwa nilichokiona misimu miwili Yanga ndiyo timu inayopenda shughuli kuliko klabu yoyote Afrika. Ni watu wa shughuli. Wanakimbizana kirahisi tu. Ubingwa wa Manchester City hauwezi kuona wanaenda kushangilia Old Trafford. Haiwezi kutokea hata kwa dawa.

Liverpool hawawezi kutwaa ubingwa halafu mashabiki wakaenda makao makuu ya Klabu ya Everton. Huwezi kuona hii kitu. Haya mambo yanahusisha hisia kali kwa mashabiki. Ni vyema kuepuka mazingira yoyote yanayoweza kuamsha hizo hisia kali kwa mashabiki. Najua umesoma neno kwa neno hadi unamaliza. Niandikie maoni yako kupitia namba ya simu hapo juu. Hongereni Yanga kwa ubingwa.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: