Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kocha huyu Mbrazili amfundishe Kibu Denis?

Kibu Denis Usajili Kibu Denis

Mon, 9 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba imemtangaza rasmi kocha Mbrazili, Roberto Oliveira kama mkufunzi mkuu wa timu. Ni kocha mkubwa sana hapa Afrika Mashariki.

Mbali na kuifikisha Vipers kwenye hatua ya makundi ya CAF, amewahi pia kufanya makubwa na Rayon Sports ya pale Rwanda. Inafurahisha sana.

Ni wazi kuwa Simba ilikua inawaza kupata kocha wa kuwasaidia katika mechi za CAF kuanzia mwezi ujao. Hawakuwa na imani kubwa na Juma Mgunda. Ni jambo la kisaikolojia zaidi. Wanaamini katika makocha wa nje zaidi. Lakini swali ni je Mgunda alifanya vibaya? Inafikirisha sana.

Mgunda tangu apewe Simba amepoteza mechi moja tu ya mashindano. Alifungwa dhidi ya Azam FC kwenye Ligi Kuu Bara pale kwa Mkapa.

Tangu hapo hakuwahi kupoteza mchezo mwingine wowote wa mashindano ikiwemo dhidi ya Yanga ambao ulimalizika kwa sare.

Baada ya kupoteza kwa Azam, Mgunda amecheza mechi 13 za Ligi bila kupoteza. Ndio kipindi ambacho Simba imegawa dozi nzito ikiwemo dhidi ya Mtibwa Sugar, Geita Gold na Tanzania Prisons.

Labda watu watasema sare alizopata dhidi ya Singida Big Stars, Kagera Sugar na Mbeya City ndio zimempunguzia nguvu pale Simba. Lakini nani asiyejua kuwa michezo hiyo ya ugenini ni migumu?

Mfano pale Kaitaba, Simba iliizidi Kagera Sugar kila kitu. Walitengeneza nafasi za kutosha. Wakafanya majaribio kama yote. lakini golikipa Said Kipao alikua na siku nzuri mchezoni. Mechi ikaisha kwa sare.

Kwenye mechi za CAF, Mgunda ndio kocha pekee tangu kuanzishwa kwa Simba kushinda mechi zote za mtoano. Hakuna Mzungu wala Mjapani aliyeifundisha Simba amewahi kufanya hivyo.

Mgunda alikwenda pale Malawi akaichapa Nyassa Big Bullets kipigo cha Mbwa Koko. Tena akiwa na siku mbili tu na timu. Hakuna aliyeamini kama Guardiola huyo wa Tanga angeweza kufanya hivyo.

Akawafunga tena Nyassa pale kwa Mkapa. Akaenda Angola akawachapa De Agosto kipigo kizito. Ilikua ni mshangao mkubwa. Angola ni sehemu ngumu sana kucheza, lakini Mgunda aliifanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa.

Akawafunga tena Waangola hapo kwa Mkapa. Akawa ameshinda mechi zote za mtoano. Hakuna kocha mwingine katika historia ya Simba amewahi kufanya hivyo.

Kwanini Simba wamekwenda kutafuta kocha wa Kigeni wakati Mgunda ana rekodi hizi? Wanajua wenyewe. Labda pesa zinawawasha na wameona wazitumie. Ni kichekesho. Wakati Mgunda akiweka rekodi hizo lazima tukubali kuwa amefanya hayo katika mazingira magumu sana.

Ni kweli Simba ina kikosi bora kinachoanza. Yaani wale wachezaji 11 wanaoanza ni bora sana. Pengine ni bora kuliko wa timu nyingine nyingi. Vipi kuhusu wale walioko benchi? Ni kichekesho. Uwezo wao ni mdogo kama kiwango cha kufikiria cha watu wa Yanga.

Twende kwa mifano mizuri. Anaanza Augustine Okrah, Mbadala wake pale benchi ni Kibu Denis. Mchezaji anayetumia nguvu kuliko akili. Mshambuliaji anayesifika kwa kukaba zaidi.

Anaanza Moses Phiri wakati pale benchi mbadala wake ni Habibu Kyombo. Ni Mbingu na Ardhi. Phiri ni mchezaji wa daraja la juu sana wakati Kyombo ni mchezaji wa daraja la Jangwani. Inachekesha sana.

Chama ndio hana mbadala kabisa. Mzamiru mbadala wake ni nani? Vipi kuhusu Sadio Kanoute? Hakuna.

Hii ndio Simba ya Mgunda. Mechi ikiwa ngumu hakuna wa kumnyanyua pale benchi. Angalau sasa amekuja Saido Ntibazonkiza.

Hii ndio Simba ambayo wameleta kocha Mbrazili aje kufundisha. Kweli kocha Mbrazili aje kuwafundisha kina Kibu Denis, Nelson Okwa, Nasoro Kapama na Victor Akpan? Huku ni kumchosha Mbrazili wa watu.

Ni wazi kuwa Simba inahitaji kufanya usajili wa maana. Hili ndio tatizo lao kubwa. Hii ndio shida aliyokuwa anaipata Mgunda.

Kwa hawa kina Okwa na Kibu Simba hata ishushe kocha kutoka Sayari nyingine hawezi kuwa na maajabu.

Lazima Simba isajili straika mwingine wa kusaidiana na John Bocco na Phiri. Lazima Simba isajili winga na kiungo mwingine. Bila hivyo ni sawa na kujitekenya kisha wanacheka wenyewe

Ila yote kwa yote sina mashaka na uwezo wa huyu kocha aliyekuja. Muhimu ni kumwambia tu ukweli kuhusu baadhi ya wachezaji. Asiwe kocha wa mifumo na maelekezo mengi.

Mfano mchezaji kama Chama wala haitaji darasa kubwa kucheza. Chama anafahamu nini cha kufanya wakati wote. Kocha lazima afahamu kuwa huyu ndio Messi wa Simba. Asianze kumpa majukumu ya kukaba na kucheza kwa maelekezo mengi. Chama ndio ufunguo wa timu. Huyu ndiye anafanya wachezaji wote ndani ya timu wanachamgamka. Lazima kila kocha anayekuja ampe heshima yake.

Columnist: Mwanaspoti