Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Klabu zifikirie dili za kuuza wachezaji pia

Nionavyo Pic Klabu zifikirie dili za kuuza wachezaji pia

Sat, 5 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) lina sheria na taratibu za kuhakikisha ya kwamba kuna nidhamu ya mapato na matumizi miongoni mwa wanachama wake ikiwa ni pamoja na klabu.

Lengo la utaratibu huu siyo tu kuondoa ‘fedha chafu’ kwenye mchezo wa mpira wa miguu lakini pia kuhakikisha kuna utamaduni unaofanana katika matumizi ya fedha bila kujali klabu kubwa na ndogo.

Katika utaratibu huu wa Football Financial Fair Play (FFFP) kunatakiwa kuwepo uwiano mzuri kati ya mapato na matumizi ya klabu.

Klabu hazitakiwi kununua kuzidi kiasi, zinatakiwa kudhibiti matumizi au kulazimika kuuza sana ili kuweza kununua sana.

Hapa kwetu klabu hazijawekewa kiasi au namna ya matumizi ya fedha za klabu katika manunuzi ya wachezaji.

Hii yawezekana ni matokeo ya historia ambako klabu zilikuwa hazinunui wachezaji wote. Huko nyuma kulikuwa na wachezaji waliokulia kwenye klabu, waliomaliza mikataba kwingine na walionunuliwa na mashabiki au wanachama.

Kwa jinsi hii hakukuwa na haja ya kuwajibika kwenye matumizi na manunuzi ya wachezaji.

Baada ya shirikisho (TFF) kuruhusu klabu kusajili wachezaji mpaka 12 wa kigeni, unaweza kuona kuna klabu zina kiu hata ya kununua wachezaji 15 wa kigeni wakati kuna klabu za Ligi Kuu hazina hata uwezo wa kununua mchezaji mmoja kutoka nje ya nchi.

Kuna swali moja nimekuwa nikijiuliza nalo ni, je kuna klabu ngapi zimeuza wachezaji nje ya nchi? Au tuliweke hivi Je ni wachezaji wangapi wameweza kuuzwa nje ya nchi? Naamini kabisa majibu ya swali hilo hapo juu litakuonyesha kwamba klabu zetu zina hamu ya kununua kuliko ya kuuza wachezaji.

Klabu zina uwezo wa kwenda nje na kununua wachezaji lakini haziweki juhudi kwenye kutafuta soko la wachezaji wake kwa lengo la kupunguza matumizi, kuingiza kipato na kupata wachezaji walio bora zaidi.

Hata tukiachana na suala la kuuza wachezaji nje ya nchi, je ni klabu ngapi zinauziana wachezaji miongoni mwao? Jibu la swali hili litakushangaza.

Idadi kubwa ya wachezaji wanaosajiliwa kutoka klabu moja kwenda nyingine walio wengi ni wale waliomaliza mikataba (Free Agents), wakifuatiwa na wale walio kwenye mikopo (on loan) na mwisho ni wale ambao klabu imeuza mchezaji (sale transfer).

Maswali hayo hapo juu yananipeleka kwenye swali kubwa kwamba ni kwa muda gani klabu zinaweza kuendelea kuishi kwa kununua wachezaji huku wakiuza kidogo sana au kutouza kabisa? Hivi leo ziko klabu nyingi za madaraja yote ambazo ukiuliza msimu wa 2022/23 wameuza wachezaji wangapi, jibu utakalopewa ni sifuri au karibu na hapo.

Katika uzoefu wangu wa uongozi wa klabu, sikumbuki zaidi kusaini mikataba ya kununua wachezaji kutoka klabu za hapa nchini zaidi ya wachezaji kutoka Mtibwa Sugar FC.

Klabu ya Mtibwa Sugar sio kwamba tu ilikuza vipaji, pia ilikuwa na mikataba inayoeleweka kwa wachezaji wake kiasi kwamba klabu nyingine ikipiga hodi kutaka kununua mchezaji hawababaiki wanapokaa nayo mezani.

Mtibwa Sugar walikuwa tayari kuongea na kumpa ruhusa mchezaji kuongea maslahi binafsi (personal terms) na kisha biashara inaendelea.

Kwa namna hiyo, naamini mpaka leo Mtibwa Sugar watakuwa wanauza wachezaji kila msimu hivyo kupata kifuta jasho kutoka gharama walizotumia kumlea na kumtunza mchezaji.

Ni wakati sasa klabu za hapa nchini zinatakiwa kukuza na kuendeleza vipaji ili kuinua kiwango cha timu na kupunguza matumizi ya kununua wachezaji kutoka klabu nyingine.

Leo ukiuliza ni klabu ngapi katika kikosi kinachoanza (starting xi) zina wachezaji waliokulia pale bila shaka jibu litakushangaza.

Kwa uongozi wa klabu, hili linapaswa kuwashtua. Maana yake ni kwamba wachezaji ulio nao na ambao unawaonyesha sokoni kila timu iingiapo uwanjani, wakimaliza mkataba wa mwaka mmoja, miwili au zaidi wanaweza kuondoka na klabu isiambulie kitu.

Klabu kubwa kama Yanga, Simba na Azam zina uwezo na mvuto wa kuweza kuvutia vipaji na kwenda hatua mbele zaidi ya Mtibwa.

Kwenye michezo ya shule za msingi (Umitashumita) na ile ya sekondari (Umiseta) na hata mtaani kuna vipaji vingi wakiamua kuvitafuta.

Klabu hizi na nyingine zikiimarisha vikosi vyao vya vijana wanaweza kuvuna wachezaji wazuri wanaoufahamu utamaduni wa klabu lakini ambao pia wanaweza kupunguza uwiano wa wachezaji wanaonunuliwa na wanaouzwa.

Na zaidi kuna ‘mapato ya milele’ ikiwa mchezaji aliyekuzwa klabuni anafanikiwa kuuzwa hata na klabu ya 5 tangu aondoke klabuni.

Kama ulikuwa hujui, Mbagala Market (African Lyon?), Simba na TP Mazembe bado zinapata kipato kutokana na jasho la kijana wao Mbwana Samatta kiasi wanatamani auzwe kila siku na asitundike daruga.

Ni wakati sasa kwa kila klabu kujiuliza ni kwa nini kila msimu unakuwa ni wa kununua tu?

Ni wakati wa kuweka utaratibu na mikataba mizuri ambayo itawezesha klabu kuuza wachezaji ambao hawahitajiki badala ya kila mara kuwaacha huru huku zikilazimika kuwafidia. Ni wakati wa klabu kuangalia namna ya kushirikisha mifumo yake ya kutafuta vipaji na mifumo ya kuuza wachezaji.

Kwa wanaojua biashara ya michezo, ni hasara kubwa sana klabu inaposajili mchezaji ikamtumia na kisha akaondoka bila kuuzwa.

Hii ina maana kwamba uwekezaji wote tangu kumnunua mchezaji mpaka anaondoka unakuwa umekomea hapo. Sioni maendeleo endelevu kwa klabu ambayo imeamua kuishi maisha ya kununua wachezaji bila kuuza.Biashara ya mpira ni kununua na kuuza.

Columnist: Mwanaspoti