Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kipigo cha Yanga kimeteteresha afya

Simba Vs Yanga Chama Yulee.jpeg Kipigo cha Yanga kimeteteresha afya

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jumapili katika Uwanja wa Benjamini Mkapa kwenye mchezo wa Ligi Kuu, Yanga ilimdhalilisha mtani wake wa jadi, Simba mara baada ya kumpiga kipigo cha aibu cha mabao 5-1.

Kipigo hicho kisichokubalika kwa mashabiki kindakindani wa Simba kilisababisha mtetereko wa afya. Hii ni baada ya baadhi ya mashabiki kupata mshtuko na kupoteza fahamu wakiwa wanatazama mchezo.

Kama vile haitoshi kipigo hicho kilisababisha baadhi ya mashabiki na wachezaji wa Simba kupata mpasuko wa hisia ikiwamo nahodha wa klabu hiyo, Mohamed Hussein aliyemwaga machozi ya uchungu hadharani.

Naam huo ndio mpira, ni burudani lakini hubeba hisia za mamilioni ya mashabiki hasa wa Yanga na Simba. Katika hii ‘Kariakoo Derby’ inakuwa balaa zaidi kwani mechi inabeba msisimko wa kipekee nchini.

Kufungwa kwa yeyote huwa ni kawaida kupatwa na hali ya mtetereko wa afya hasa ya akili ikiwamo kupata hasira, ghadhabu, kujawa na hofu, wasiwasi, woga, shinikizo la akili na sonona.

Mtetereko wa kiafya ndio pia unaowafanya mashabiki kuanguka uwanjani na kuzimia kutokana na miili kupokea jambo la kufungwa kwa hisia hasi, hali inayoambatana na kuzalishwa kwa kichochezi cha Adrenaline.

Mtetereko wa kiafya huwa unatokea maeneo makuu manne ya klabu ikiwamo wachezaji, mashabiki, benchi la ufundi na uongozi. Kadri timu inavyofungwa mabao mengi ndivyo athari zake zinakuwa juu zaidi.

Tayari kuna baadhi ya wachezaji wa Simba wamenyooshewa vidole kuwa wamehujumu mechi hiyo. Hapa ni kawaida kwa wachezaji hao kupata mtetereko wa afya ya akili ikiwamo shinikizo la akili kutokana na kuwaza hatima zao.

Tayari Simba imewatupia virago makocha wawili Kocha Mkuu Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ pamoja na kocha wa viungo, Corneille Hategekimana ambaye ni raia wa Rwanda. Hali ya kipigo kama kile ni lazima kocha awe katika hali ya shinikizo la akili kutokana na kuwaza nini kitampata kufuatia matokeo mabaya.

Ndani ya uwanja wakati mchezo unachezwa wachezaji nao hukumbwa na hali ya mtetereko wa afya ya akili ikiwamo kupata mpasuko wa hisia, hali inayowafanya kucheza na hofu au wasiwasi.

Mchezaji akishaathirika kisaikolojia ndani ya uwanja tayari huwa ni faida kwa mpinzani kwani hali hiyo humfanya kucheza pasipo umakini. Haishangazi mara baada ya Simba kufungwa mabao mawili tayari hali hiyo ikaleta mtetereko wa afya ya akili kwa wachezaji ikiwamo kupatwa na hofu na hasira.

Hali hiyo ndio inayoathiri moja kwa moja muunganiko wa mchezaji mmoja baada ya mwingine kuweza kuratibu mambo mbalimbali ya uwanjani ikiwamo kukaba, umakini wa kutoa pasi na kushambulia.

Kama vile haitoshi mpaka kule bungeni tayari kumeibuliwa tuhuma kuwa huenda kipigo hicho kimetokana na rushwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachamwene ameomba Simba kama imebaini vitendo vya rushwa ni vizuri tuhuma zikapelekwa ofisi ya Takukuru, Wilaya ya Temeke ili hatua ziweze kuchukuliwa. Hii ndio mechi pekee hapa nchini ambayo inagusa kila mahali ikiwamo hisia za waheshimiwa wabunge na mawaziri.

Kama mnavyojua hata mchezo huu kuna janga lingine ambalo nalo linaweza kuteteresha afya ya akili hasa kwa wachezaji. Janga hilo ni hofu ya uchawi au ndumba.

Miaka yote ya mechi ya watani wajadi hugubikwa na vijimambo ambavyo kwa wengine kwao ni ishara ya uchawi au kurogwa ili wafungwe. Mfano wapo ambao wanaona kitendo cha Yanga kutotumia lango kuu badala yake wakatumia mlango maalumu wanaotumia waandishi wa habari ni kitu kisichokubalika.

Vilevile ipo video ambayo ilitumwa mitandaoni ikionyesha wachezaji wa Yanga wakimwaga vimiminika kwenye goli la Kaskazini na kwenye kibedera na kuvisigina kwa viatu vyao.

Hii ilileta gumzo, huenda ni maelekezo kutoka kwa wataalamu wa nje ya uwanja.

Vitendo vya ndumba katika soka navyo vinaweza kuwapa hofu wachezaji hatimaye kuteteresha afya ya akili na kuathirika kisaikolojia kwa wachezaji.

Pia, wapo mashabiki ambao kazi yao ni kucheza na saikolojia ya wachezaji na mashabiki, lengo ni kukata hamasa na ari. Hawa ndio wale mashabiki wakiwa na mavitu vitu mwilini vyenye mwonekano kama vile hirizi au vifaa vya kufanyia mambo ya kichawi.

Mchezaji au mwanasoka anapomwona mtu wa namna hii huweza kuingiwa na hofu ya kurogwa hatimaye kumtoa mchezoni.

Naam hizi ni mbinu au fitina ya soka, wadau wa soka la Bongo wanasema mchezo wa soka huwa unachezwa ndani na nje ya uwanja.

Nje ya uwanja ndiko kuna vibweka vya mambo ya kishirikina ambavyo vingine huwa vya utani tu lakini vina athari kwa wapinzani na kumfaidisha mwingine kupata ushindi. Katika mitandao ya kijamii nako hakupo nyuma tayari kuna baadhi ya watumiaji katika makundi ya Whatsapp baadhi ya mashabiki wa Simba wanakaa kimya isivyo kawaida bila kusema chochote.

Hii ni ishara ya uwepo wa majonzi au huzuni ambayo baadaye huweza kuleta sonona, kitabibu inaitwa depression ambalo ni tatizo la mtetereko wa afya ya akili.

Nako mtaani kejeli na maneno ya utani katika vijiwe ilifika hatua watu wanataka kupigana kutokana na kushindwa kuvumilia utani au kejeli. Hii inachangiwa na waliofungwa kuwa katika hali ya ghadhabu.

Chukua hii

Katika kutafuta mchawi nani aliyesababisha kufungwa inahitajika kufanya uamuzi kipindi ambacho akili haina mtetereko wowote wa kiafya. Kufanya uamuzi kwa hasira kunaweza kusiwe na tija. Muhimu wachezaji kupata mayatarisho ya kisaikolojia kutoka kwa wataalamu wa saikolojia kabla na baada ya mechi ili kuwaepusha na matatizo ya kiakili ikiwamo msongo wa mawazo na hofu.

Ndani ya uwanja ni jukumu la nahodha na msaidizi wake kuwatuliza wenzake hasa pale wanapoonyesha dalili za kutetereka kiakili baada ya kufungwa.

Columnist: Mwanaspoti