Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kina Drogba, Pacome wasingetazama nyuma

Pacome 1 Goal Pacome Zouzoua.

Sat, 20 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuona ni kuamini. Nilipewa nafasi ya pili kuijua nchi inayoitwa Ivory Coast. Nilikuja hapa mwaka 2012 sikuijua vyema. Nimekuja tena.

Naitazama michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) nikiwa katika mji unaoitwa San Pedro. Jina limekaa Kireno, lakini ni mji uliotawaliwa na Wafaransa.

Kabla ya hapo nilikuwa nimezurura Abidjan. Mji maarufu Ivory Coast. Kuona ni kuamini. Unakutana na umaskini uliotopea. Unakutana na vijana wanaohangaika.

Unakutana na kinamama wanaohangaika. Kutokea Abidjan kuja San Pedro nilitumia usafiri wa basi.

Nilipandia katika soko moja la Abidjan. Alfajiri.

Kabla jua halijachomoza nilikutana na kinamama wakiwa wamepanga bidhaa zao mbalimbali wakiuza kila kinachouzika. Eti alfajiri kabla jua halijachomoza.

Wanapambana na umaskini katika nyumba duni na maisha hafifu. Wameamka saa ngapi, wamefuata bidhaa saa ngapi na wamepanga saa ngapi wewe ulikuwa usingizini.

Mawazo yangu yalikwenda mbali. Yalikwenda kwa mastaa wa soka wa Ivory Coast ambao dunia inawafahamu na kuwakubali.

Kina Yaya Toure, Didier Zokora, Kolo Toure, Didier Drogba, Siaka Tienne na wengineo wengi.

Hawa ndio mama zao. Na hawa ndio sababu wakapambana kwa machozi, jasho na damu kufika walikofika.

Nilipokutana nao uso kwa uso nilikumbuka simulizi nyingi za mastaa wa Afrika Magharibi wakielezea kuhusu maisha yao ya utotoni. Mmoja angekwambia; “Mama yangu alishindwa hata kuninunulia viatu vya kuchezea soka. Nililazimika kucheza peku na vijana wenzangu katika uwanja wetu mtaani. Nimevaa viatu vya soka ukubwani.”

Kuna mwingine anakwambia; “Tulikuwa tunakula mlo tu nyumbani. Soka ndio kilikuwa kitu pekee ambacho ninaweza kufanya. Mama na baba walishindwa kunipa hata hela ya nauli ya kwenda mazoezini. Nililazimika kutembea kilomita tano kila siku kwenda mazoezini.” Umewahi kusikia mara ngapi simulizi kutoka kwa wanasoka wa Afrika Magharibi na Amerika Kusini?

Umaskini haujavaa nguo Ivory Coast. Haishangazi kuona ndiyo maana mastaa hawa walipambana kufika walikofika. Walipambana kuwaondoa mama zao na baba zao katika maisha haya. Labda ni tofauti na kule kwetu ambako kuna ujamaa mwingi na kwingine ambako kuna utajiri mwingi.

Ni tofauti na Afrika Kusini na Afrika Kaskazini ambako kuna utajiri unaoonekana kwa macho. Nimetembelea Afrika Kusini, Misri, Tunisia, Morocco na Algeria. Sawa kuna maeneo ambayo yana umaskini lakini walau wao wana utajiri. Ni utajiri ambao unawafanya wachezaji wengi wa ndani wasikimbie kwenda Ulaya. Mkate na chai ya maziwa vinapatikana.

Lakini umaskini huu ndio umeifanya Ivory Coast kuweza kuita wachezaji zaidi ya 40 kutoka Ulaya na maeneo mengine nje ya Ivory Coast kwa ajili ya kuchezea timu ya taifa. Ndio, watoto wao wakiondoka nyumbani huwa hawaangalii nyuma. Wanapambana kwa machozi, jasho na damu kuwaondoa mama zao katika unyonge.

Wale wa hizo nchi za kina Afrika Kusini huwa wanaridhika mapema. Mama zao hawapo katika umaskini uliotopea. Lakini hata wenyewe wakianza kupata pesa huwa wananunua magari ya kifahari na kuishi katika nyumba za kifahari. Klabu zao zinawalipa pesa nyingi na wanafanya vurugu nyingi katika mitaa ya Pretoria, Johannesburg, Cape Town na kwingineko.

Na hapo hapo nawawaza wakoloni wa Ivory Coast. Wafaransa. Walichofanya ni kuisambaza lugha yao kwa makoloni yao. Walichofanya ni kuwafanya kina Didier Drogba wajisikie kuwa Wafaransa. Baada ya hapo wanachuma mali na kupeleka Ufaransa.

Makoloni ya Wafaransa yote ni maskini. Kuanzia Ivory Coast, Benin, Guinea, Mali, Togo, Senegal na kwingineko.

Hapa Ivory Coast kinamama zao Drogba wanafanya shughuli za chini za kimaskini kwa sababu unaona kabisa nchi sio ya viwanda. Ni wazi kuna tatizo kubwa la ajira Ivory Coast.

Kwa nini hawakujenga viwanda Ivory Coast? Kwa nini hawakuwekeza moja kwa moja Ivory Coast? Hapana. Walichofanya wao ni kuchuma rasilimali na kupeleka Ufaransa ambako kuna viwanda na kila kitu. Na baada ya hapo wakafanya ulaghai kwa uraia.

Ukiwa Mfaransa maarufu unakuwa raia wa Ufaransa. Kuanzia kina Drogba hadi marais wake. Naambiwa marais wote wa nchi ambazo zinaongea Kifaransa ni raia wa Ufaransa. Hii inasababisha waendelee kutii. Lakini inasababisha kwa kiasi kikubwa wajione Wafaransa zaidi na wasijali sana kuhusu nchi zao.

Haishangazi kuona kuna wengine wameanza kushtuka. Na ndio maana kule Niger na kwingineko wameanza kung’oa marais wao wakiwa wanajua ni vibaraka wa Mfaransa.

Sijui kama itaendelea katika mataifa mengine lakini najiuliza kama wataweza kujinasua katika mikono ya Wafaransa licha ya kufanya mapinduzi haya. Naambiwa nchi zote zilizotawaliwa na Ufaransa hazina Benki Kuu. Uchumi wao unaendeshwa na Mfaransa.

Nimewawaza sana kina Pacome Zouzoua. Kina Yao Kouassi. Labda ndio maana wamejipambanua kuwa wachezaji tofauti. Labda ndio maana wako kwetu. Hata kama sio Ulaya, lakini wapo kwetu. Kuondokana na makucha ya umaskini wa kwao haikuwa kazi rahisi sana.

Lakini asikudanganye mtu. Wanapokatiza mitaa ya Sinza, Mwenge, Masaki na kwingineo basi wanakatiza katika mitaa ambayo wanapumua vyema na hawauoni umaskini mwingi kama kwao. Inawezekana Ivory Coast ikatajwa kuwa nchi iliyo juu ya Tanzania kwa utajiri lakini hauwezi kuona hayo yakiakisi kwa raia wa kawaida wa Ivory Coast.

Unapomwona Yao Kouassi anakazana namna ile kumbe ana siri kubwa ameiweka kifuani kwake. Labda anakumbuka alfajiri zinazomkumba mama yake. Labda anataka kumtoa katika zile alfajiri ambazo zilinikuta nikichukua basi kutoka Abidjan kuelekea San Pedro. Inawezekana. Labda.

Columnist: www.tanzaniaweb.live