Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kilimo cha kisasa, njia bora inayobadili maisha ya mkulima

761dedee86ae67fde26ff877ed3e57ee Kilimo cha kisasa, njia bora inayobadili maisha ya mkulima

Thu, 21 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KILIMO ni mojawapo ya shughuli za mwanadamu zinazomsaidia kupata mazao ya chakula na biashara yanayomuingizia kipato kwa ajili ya maisha yake na kukuza uchumi wa nchi.

Kilimo kina maana pana inayojumuisha mifumo ya uzalishaji mimea, ufugaji wa wanyama mbalimbali na uvuvi wa samaki. Mara nyingi kilimo cha mimea kinaenda sambamba na ufugaji.

Hata hivyo, kilimo ni kazi inayohitaji ustahimilivu, wakulima hustawisha mimea na kuitunza hadi mavuno hasa kwa uzalishaji wa chakula na lishe kwa binadamu na wanyama.

Aidha kilimo huzalisha malighafi zinazotumiwa kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile nguo, mafuta, nishati ya mimea.

Sekta ya kilimo ni kiinua uchumi kikubwa kwa mataifa mengi, Serikali zinatakiwa kuipa kipaumbele sekta ya kilimo ili kuepukana na janga la njaa na kushuka uchumi wa nchi husika.

Mojawapo ya mahitaji makuu ya mwanadamu ni chakula, Serikali zinatakiwa kuwafikishia wakulima zana za kilimo na pembejeo kuwarahisishia kuzalisha mazao ya biashara na chakula kwa wingi.

Swali muhimu katika sekta ya kilimo ni jinsi gani tutalisha watu bilioni 9.5 ifikapo mwaka 2050? Wakulima kutoka ulimwenguni pote walijadili suala hili na maswala mengine ya kilimo wakati wa Mazungumzo ya Wakulima Duniani yaliyofanyika wakati wa Tuzo ya Chakula Duniani ya mwaka 2016 Des Moines, Iowa.

Wakati unafurahia mlo wako au kuburudika na kikombe cha kahawa au kakao tumia walau dakika chache kumfikiria mkulima, tafakari taabu na karaha anazokumbana nazo mkulima wa zama za kale hadi sasa, waza mkulima akiyakinga macho yake kutokana na miale ya jua, anasimama mlangoni na kuvuta hewa yenye unyevunyevu, mvua tayari imelowanisha udongo uliokuwa umekauka kwa sababu ya jua.

Msimu wa kulima umefika anabeba mabegani jembe la mkono au anatumia jembe la kukokotwa na ng'ombe alilolitengeneza kwa mbao na kuelekea katika shamba lake, huyu ni mkulima wa karne ya kwanza! anakusanya ng'ombe wake na kuwafunga nira pamoja, kisha anawachomachoma kwa michokoo ili waanze kazi.

Ncha ya jembe hilo iliyotengenezwa kwa chuma inachimba udongo wenye mawe-mawe. Jembe hilo halipindui udongo bali linapasua udongo na kuchimba mtaro usiokuwa na kina kirefu na kutengeneza matuta. Akiyumba kushoto na kulia mkulima huyo wa kale anajitahidi kuhakikisha mtaro huo umenyooka, haangalii nyuma kamwe, la sivyo jembe litaenda mrama.

Baada ya kupanda miezi inapita, wakati wa kuvuna ni kipindi chenye shughuli nyingi kwa mkulima na familia yake, akichekecha nafaka ikiwemo kusaga na kukoboa nafaka hizo kwa kutumia jiwe, baadhi zinapelekwa gulioni na nyingine zinahifadhiwa kwa matumizi ya nyumbani.

Mkulima wa karne zilizofuata bado anakabiliwa na adha hiyo kivingine kama vile bei, pembejeo nk. “Baadhi ya watu wanaangalia matatizo ya wakulima kijuu juu, hawaelewi kwa nini wakulima huendelea kulima,” anasema Rodney mkulima wa kizazi cha tatu.

Hata hivyo, mamilioni ya watu ulimwenguni pote huendelea kulima kwa sababu kilimo ndicho kinachotoa ajira zaidi kwa mamilioni ya watu.

“Kuna wakulima wa aina mbili, wanaouza kahawa ambayo haijakomaa shambani na iliyokomaa katika vyama vya ushirika,” anasema Inyasi Kamakumbi mkulima wa kahawa kijiji cha Ihangiro pia Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Rulongo, wilayani Muleba akiongea na gazeti hili.

Mwenyekiti huyo anasema zao la kahawa lina tija, tatizo ni mashine ya kukoboa kwa vyama ambavyo havina mashine ya kuhimili wingi wa kahawa, anasema tatizo hilo husababisha gharama nyingine za kupeleka zao hilo ilipo mashine yenye uwezo wa kukoboa kahawa nyingi.

Kupunguza gharama inawalazimu baadhi ya wakulima kuuza kahawa hiyo kwa walanguzi baada ya kokobolewa kuliko kuingia gharama nyingine ya kupeleka kuuza kahawa hiyo kwenye chama cha ushirika.

Akizungumza na gazeti hili ofisa ughani (jina linahifadhiwa) kutoka wilayani Muleba anasema tatizo linalomkabili mkulima wilayani humo ni soko na pembejeo, ofisa huyo anasema kumkomboa mkulima ni kumpatia soko la uhakika na uhuru wa kuuza mazao yake bila kumpangia bei.

“Mkulima anapopata pembejeo kwa wakati”mazao yake yataongezeka kwa mfano mkulima akitumia mbolea ya kiwandani atavuna gunia 15 badala ya tatu au nne kwa eka moja.

“Wakulima wanashindwa kumudu bei ya pembejeo aidha wafanyabiashara walio wengi hawauzi pembejeo wakihofia hasara kwa sababu ni wakulima wachache wanaomudu bei”, anasema.

Ofisa huyo anatoa mwito kwa wakulima kulima mazao mengine kama vile vanila, karanga miti, nyanya na mengineyo. Itamsaidia mkulima wilayani humo kutotegemea zao la kahawa peke yake.

Anaiomba Serikali kuboresha soko na pembejeo kwa mkulima wilayani humo na kupeleka wataalamu wa nyanja mbalimbali vijijini kuboresha kilimo na maisha ya mkulima.

Anashauri vyama vya ushirika makubaliano na wakulima kwa kuwauzia pembejeo kwa makubaliano maalum, anasema ili vyama viweze kujiendesha ni lazima mkulima akatwe asilimia fulani, anasema hata hivyo makato hayo ni asilimia ndogo.

Mkulima Evodius Jeronimo wa Kijiji cha Rwagati, Tarafa ya Nshamba, anasema kutokana na jitihada za mkulima na elimu anayopata kutoka kwa ofisa ughani, kilimo kimeboresha maisha ya mkulima.

Anasema tatizo linalomkabili mkulima wa kahawa ni soko la uhakika, uchelewashaji wa malipo na bei ya pembejeo, anaomba Serikali isimamie upatikanaji wa pembejeo na bei ambayo mkulima ataimudu kulingana na uwezo wa mkulima mwenyewe.

“Kilimo cha migomba, kahawa, mahindi, maharage, kinapopata mbolea mazao yataongezeka,” anasema Jeronimo. Anashauri vyama vya Ushirika kuingia makubaliano na wakulima namna ya kuwakopesha pembejeo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini bado kuna uhaba wa maofisa ughani katika tarafa kadhaa wilayani humo, kwa mfano ofisa ughani mmoja anahudumia kata moja hadi mbili, kata moja ina vijiji saba hadi nane bila usafiri, tatizo la kutokupatiwa pikipiki maofisa hao linasababisha kutowafikia wakulima kwa wakati.

Tatizo la bei ya mazao na hali ya hewa isiyotabirika ni kizungumti duniani, bei ya pamba ikianguka kwa asilimia 10, maana yake mkulima wa pamba Afrika mathalani wa Mwanza na Geita anapungukiwa kwa asilimia 20. Matokeo yake anaachana na uzalishaji wa pamba na kutafuta ajira mijini.

Takribani mashamba ya pamba 900,000 Afrika Magharibi yaliathirika ilihali yakiajiri wakulima milioni saba hadi nane. Ukichanganya na familia zao ni jumla ya watu milioni 13 walioathirika kutokana na kuanguka kwa bei ya pamba.

Wakulima wakubwa 2,500 nchini Marekani wanagawana miongoni mwao zaidi ya dola billioni tatu kila mwaka, ambapo wakulima milioni 20 hadi 30 wa zao la Pamba barani Afrika wanaishi katika maisha ya tabu na kusikitisha kwasababu hawafaidiki na chochote kutokana na juhudi zao za ukulima wa pamba na mwisho hawawezi hata kukimu mahitaji yao ya chakula cha kila siku.

Eusebio anayeishi katika Milima ya Andes, analima mazao mbalimbali na kufuga ng’ombe 14 “Wote wana majina,” anasema anapenda kulima na kustawisha mboga.

Yeye mkewe na jirani zake husaidiana kulima na kuvuna, anasema hawana mashine za kilimo, “tunalima kwa plau zinazokokotwa na fahali, kwenye miteremko mikali tunalima kwa jembe la mkono”.

Anasema, “Wakati mifugo yetu yote ilipokufa kutokana na ugonjwa, baada ya janga hilo nilisomea namna ya kutibu wanyama, hakuna mnyama ambaye amekufa tangu wakati huo, ninaweza kuwasaidia majirani kutunza mifugo yao. Tunauza jibini sokoni kwa bei ya chini hata hivyo wakati wote tuna akiba ya chakula cha kuwalisha watoto wetu sita, anasema mkulima huyo mdogo.

Columnist: habarileo.co.tz