Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kilichojificha juu ya imani za kwenye misiba

Kifo Kifo Mauiaji.png Kilichojificha juu ya imani za kwenye misiba

Mon, 11 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Umewahi kusikia imani mbalimbali kuhusu misiba, zikiwemo potofu, kwamba alichokisema marehemu wakati wa uhai wake hakipaswi kupuuzwa hata kama familia yake haina uwezo wa kukitekeleza?

Mathalan, katika jamii, koo au makabila mbalimbali wengi wanaamini mtu anapofariki dunia lazima mwili wake upelekwe kwenye nyumba yake kwanza, ulale hapo kabla ya kuzikwa.

Wanaamini, bila kufanya hivyo tukio baya linaweza kutokea kwenye familia, ambalo kwa namna moja au nyingine litaathiri maziko.

“Iliwahi kutokea mvua kubwa ikanyesha wakati tunajiandaa kwenda kuzika, ni kwa sababu tulitoka na mwili Dar es Salaam kwenda Morogoro, tulipofika nyumbani maiti haikuingizwa ndani,” anasimulia Rahel Gamba.

Anasema jeneza lenye mwili wa baba yake lilifikishiwa nje ya nyumba yake na taratibu zote za kuaga zilifanyika hapo. Jeneza lilipobebwa kwenda makaburini, ilinyesha mvua kubwa, ndipo watani wakaanza kutoa maneno kwamba Mzee Gamba amekasirika hajaingizwa ndani ya nyumba yake.

“Kweli hakuna kilichoendelea, ilibidi jeneza lenye mwili liingizwe ndani kwanza kusubiri mvua ipite, ilipokata tukaenda kuzika, sijui kama ilikuwa ni kweli au ni imani tu,” anasema.

Hata hivyo, mmoja wa wazee wa kimila mkoani Mara, Mtayombwa Mafuru anasema hiyo ni imani tu ambayo imejengeka, baadhi ya koo au makabila yanaiendeleza kutoka kwa babu na bibi zao.

“Hata akilala nyumbani hawezi kufufuka, hakuna sababu ya msingi kwamba akilala nyumbani kwake kuna kitu kitatokea,” anasema.

“Hii ya marehemu lazima aingizwe ndani ni watu tu wa jamii fulani waliamua kuweka huo utaratibu kwa imani zao, tumezikuta na zinaendelezwa, mfano kuna watu wanasema ukimweka marehemu kichwa hivi, mtapata shida, lakini hakuna lolote litakutokea kama huna imani hizo,” anasema.

Anasema kuna familia zinaamini wakiwa wanazika na mvua ikanyesha wanasema marehemu alikuwa mkulima, hivyo mvua inamlilia.

“Wapo watu wanagombana wakiwa hai, wanaambiana ‘nikifa usije kwenye kaburi langu’, ikitokea mmoja ametangulia, yule aliyegombana naye anaogopa kweli kwenda.

“Hata baba yako, akikataa usimzike, ukilazimisha bila kuogopa, hakuna kinachotokea, ukiamini na kuogopa utapata tatizo kwa kuogopa kwako,” anasema Mafuru.

Jambo jingine, Rahel Gamba anasema ipo imani nyingine, kuhusu utaratibu wa kuliingiza kwenye gari jeneza lililobeba maiti.

“Sisi huwa tunaamini jeneza lenye mwili, upande wa kichwa lazima uangalie mbele. Mwaka jana alifariki dada yangu, tulimsafirisha kutoka Dar es Salaam kwenda Mafinga.

“Waliochukua jukumu la kusafirisha mwili wakawa wabishi, tuliwaambia jeneza halipaswi kuwekwa upande, wakatugomea, wakaliweka kwa upana, upande wa kichwa ukiangalia ubavuni mwa gari.

Hivyo, Rahel anasema walisafiri kwa taabu gari ilikuwa ikichemsha, lakini hataki kuamini kwamba huenda gari lilikuwa bovu.

“Baadaye tuliletewa gari nyingine, tulipohamisha mwili ukawekwa kwa kichwa kuangalia mbele, tulisafiri bila shida yoyote na ile gari nyingine ilitufuata nyuma bila tatizo,” anasema Rahel.

Ni masuala ya mila

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na imani hizo, Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo anasema matukio mengi ya aina hiyo yanachagizwa na masuala ya mila.

Akizungumzia kwa muktadha wa dini, Sheikh Kitogo anasema kwa Waislamu hata ile imani kwamba marehemu alisema akifa azikwe mahali fulani si sahihi.

Kadhi hiyo wa Dar es Salaam, anasema katika Quran, Mwenyezi Mungu anasema hakuna anayejua atafia wapi?

“Ikiwa utafia kwenu ni bahati yako, ukifia Ulaya, Marekani na popote itategemea na uwezo wa watu wako watakuletaje, vinginevyo pale utakapofia ndipo utakapozikwa.

“Ila tumeambiwa kama utafia karibu na eneo takatifu ambalo kwetu Waislamu ni Maka au Madina, unaweza kuihamisha maiti pale kufuata ule utakatifu, lakini sio kwa kusema uzikwe nyumbani alipolala baba au mama yako, unajuaje kama kalala?” anahoji.

Anasema, Uislamu pia haulazimishi na kuelekeza kuhamisha maiti, ila inatokea kwa sababu fulanifulani, ikiwamo kukua kwa mji na matukio ya kufukuliwa fukuliwa, ndugu wataona bora wazike eneo fulani.

“Kuna wale wanaacha wosia, kama upo nje ya utaratibu hauzingatiwi na walioachiwa hawatapa dhambi kuubadili,” anasema.

Sheikh Kitogo anakosoa pia imani kuwa marehemu anaweza kufanya mambo mbalimbali kama kujikunja, endapo alikuwa na ugomvi na mtu ambaye anakwenda kusimamia maziko yake.

“Nimewahi kusikia mara kadhaa, wanasema marehemu anafanya kinyongo hadi wengine huwa wanapinda hadi anaitwa mtu wa mila, ila kwenye dini haya hatuna.

Anasema, hata mwili kuingizwa ndani, katika dini hakuna kitu hicho, hata ile desturi ya mwili kuandaliwa ndani ya chumba cha marehemu, halina mizizi kwenye dini.

Anasema, Uislamu unataka maiti ikoshewe sehemu yenye stara, kwenye misikiti kuna mahala ‘spesho’ kwa kazi hiyo, japo wengi wanakataa wakiamini Uislamu unataka akoshewe chumbani kwake.

Kwa upande wake Mchungaji Daniel Mgogo anasema, Biblia inaamini wafu hawajui lolote, hivyo mtu anapofanya vitu kwa kufuatisha kauli za wafu au imani kwenye kitu kilichokufa si sawa.

Anasema, vyote vinafanyika kwa mila, lakini katika ulimwengu wa roho, hakuna marehemu anayesikia wala kufanya jambo.

"Mtu akishakufa, kinacholala pale ni mwili wake tu, hawezi kufanya lolote, kusema marehemu aliagiza hivi, au afanyiwe vile si sawa," anasema.

Simulizi za wasafirisha maiti

Wakati viongozi wa dini wakisema hayo, Mpale Said, dereva anayeendesha gari la kukodi ambalo mara kwa mara husafirisha maiti, anasimulia moja ya matukio ambayo aliwahi kutuhumiwa kuwa amepanga njama na familia ya marehemu.

Anasema, alikodishwa kubeba mwili kutoka Mwananyamala Hospitali, kwenda Moshi Kilimanjaro, wakiwa katikati ya safari gari lilikataa tu kuwaka.

Mpale ambaye amefanya kazi hiyo tangu mwaka 2000, anasema mara nyingi anaposafirisha maiti anakutana na matukio ya kiimani na kimila kwa wafiwa na wakati mwingine kupata maruweruwe.

“Mwanzoni nilikuwa naogopa, lakini sasa nimezoea na kuona ni kama changamoto za kazi, nakumbuka kuna siku nilikodiwa na mume wa marehemu kupeleka mwili Upareni.

“Ule msiba ulikuwa unagombaiwa, mume wa marehemu alitaka akazike Upareni na Wazigua, wazazi wa mke, walitaka wapewe ndugu yao wakamzike kwao Boma, walisema hawaendi Upareni, Wapare wakakataa,” anasema.

Anasema walipofika njiapanda ya kwenda Moshi na ile ya kuingia njia ya Boma, gari lilizima ghafla, kila alipojaribu kuliwasha ilishindikana.

"Niliambiwa nimepanga njama na ndugu wa marehemu, wakanigeuzia kibao mimi, nikasema basi mleteni dereva mwingine aendeshe gari, wakafanya hivyo gari halikuwaka.

"Tulikaa pale usiku kucha, kuanzia saa 2 usiku hadi asubuhi, ajabu ile gari nilipojaribu kuwasha na kuirudisha nyuma kufuata barabara ya alikozaliwa marehemu, iliwaka bila shida, lakini kupeleka mbele ili kuendelea na safari ya Upareni iligoma, hatukuvuka njia panda ile kwenda mbele.

"Alitokea ndugu mmoja akasema wazazi kule Upareni wapigiwe simu waelezwe kinachoendelea, walipoambiwa wakaruhusu apelekwe Boma, nikageuza gari ikawaka bila tatizo na tukafika salama," anasema akitaja matukio mengine kadhaa yenye kuhusisha imani za namna hiyo.

Kisaikolojia hiko hivi

Mwanasaikolojia wa kujitegemea, Deogratius Sukambi anasema kwa muktadha wa saikolojia, imani hizo ni mgogoro kati ya baiolojia, mila na desturi. Anasema, kuna misiba mingine pale mnapoanza kupakia mwili, gari nayo inaanza kusumbua bila sababu au jeneza halipiti.

Columnist: www.tanzaniaweb.live