Rafiki yangu Ibrahim Ajibu Migomba amekwenda katika timu yake ya tano Ligi Kuu Bara. Timu yake ya pili nje ya Jiji la Dar es salaam. Haikutazamiwa kuwa mapema hivi lakini ndio hali halisi. Ndani ya misimu mitano amecheza timu takribani tano.
Sasa Ajibu ametua Coastal Union. Ni ndoa ambayo inanishangaza kidogo. Kwanza kabisa utakubali Ajibu amekuwa hakosi timu kwa sababu ana kipaji kikubwa. Sahau kuhusu kama kipaji kimefikia malengo lakini ukweli atakutamanisha.
Ni kama msichana mrembo ambaye anakutamanisha. Unatamani awe na tabia nzuri ili awe msichana kamili. Unaamini unaweza kumrekebisha. Mwishowe unagundua unafanya miongoni mwa kazi ngumu kuwahi kufanywa duniani.
Sehemu ambayo Ajibu alitamaniwa na kutakiwa kubaki ilikuwa Yanga. Wakati ule anaondoka Yanga kurudi Simba ukweli ni kwamba Yanga walijaribu kupambana kumbakisha, lakini walikuwa na hali ngumu. GSM hawakuwepo na Yanga walikuwa wanaendeshwa kwa michango ya wanachama. Simba wakatoa Sh 80 milioni kumrudisha Ajibu Simba.
Kuanzia hapo maisha hayakwenda tena katika mkondo wa Ibra. Alipokuwa Simba hakujaribu kupambana kumwondoa Clatous Chama wala wengineo katika ufalme wao Simba. Akaamua tu kuwa mchezaji wa kawaida wa timu. Waingereza huwa wanasema ‘Squad player’. Kabla hata hajamaliza mkataba wake Simba wakairuhusu Azam imchukue.
Mfikirie Ajibu katika ubora wake. Au mfikirie tu kama akiamua kucheza soka katika kiwango cha juu. Ni timu gani inaweza kumruhusu aondoke kizembe kwenda kwa wapinzani? Kwamba Simba wala hawakuwa na hofu kuwa Ajibu atakwenda kuiimarisha Azam. Wakamuacha aende zake.
Azam waliamini wangeweza kumbadilisha Ajibu akatimiza kipaji chake kinachotumika kwa asilimia 30 tu ya uwezo wake kamili. Wakati mwingine unaweza kusadiki mawazo ya Azam labda Ajibu alishindwa kuhimili presha za mambo ya Simba. Waliamini wangeweza kumbadilisha Ajibu na kurudi kuwa yule ambaye alitamba na Yanga. Haikuwezekana.
Yoyote ambayo yalitokea kati yao na Ajibu yamebaki kuwa siri yao. Kitu kikubwa ni Azam haikuwa na mpango tena wa kumuongezea Ajibu mkataba wake pale ulipomalizika. Mkataba wenyewe ulikuwa wa mwaka tu. Kama ilivyokuwa kwa Simba basi ndivyo ilivyokuwa kwa Azam. Ajibu hakuwahi kuwa mchezaji wa First Eleven kikosini hapo.
Halafu ikaja zamu ya rafiki yangu Mwigulu Nchemba. Bosi wa Singida United. Huwa anaamini anaweza kuokoa vipaji vya wachezaji wakubwa walioshindikana Simba, Yanga na Azam. Wachezaji ambao huenda wameonekana wana matatizo ya nidhamu, umri au viwango vibovu.
Singida walijiaminisha wangeweza kukiokoa kipaji cha Ajibu. Kama ilivyo kwa wengine. Kuna kitu unahisi Ajibu anacho na unaweza kumtuliza halafu akakupa kitu kikubwa uwanjani. Rafiki yangu Mwigulu alijaribu kuwaona Simba na Azam kuwa wajinga. Akachukua silaha na kuingia vitani. Haikuwezekana.
Inasemekana katika barua ambayo Singida walimuandikia Ajibu katika mchakato wao wa kuachana naye walikariri maneno yake aliyowahi kuwaambia wachezaji wenzake wa Singida United kambini akiwaambia; “Hapa Singida hakuna mpira tumefuata vibunda tu. Mpira tumeuacha huko tulikotoka.”
Maneno haya yalikuwa mkuki ndani ya moyo kwa viongozi wa Singida United. Lengo lao la kumbadilisha Ajibu halikutimia. Ndio kwanza aliishia kuwadhihaki kwa juhudi zao walizokuwa wanafanya. Kama kilichowatokea Azam ndicho kilichowatokea Singida.
Binafsi nilijua ambacho kingefuata katika ndoa ya Ajibu na Singida. Ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza katika timu ya nje ya jiji la Dar es Salaam. Kwa vijana wa mjini waliokulia mjini kama yeye kisha wakazurura mitaa ya Ilala, Temeke na Kinondoni maisha yanakuwa magumu kwenda mikoani.
Zaidi ni pale kwamba mjini kwenyewe ulilelewa na Simba, kisha ukaletewa noti na Yanga, halafu ukarudishwa na noti za Simba halafu ukatembelewa na noti za Azam. Umekulia katika timu za mjini, noti unazo, halafu ghafla unajikuta unacheza katika timu ambayo inaishi kilomita chache kutoka Itigi au Manyoni. Maisha hayawezi kuwa rahisi.
Na sasa ametua Coastal ya Tanga. Hii ni timu nyingine ambayo inakiona kitu kile kile ambacho Azam na Singida walikiona. Kitu kile kile ambacho hata sisi tunakiona. Kwamba unaweza kumbadili Ajibu na akakupa kitu ambacho viungo wengi wa mbele hawawezi kukupa. Ambacho labda Coastal hawajui ni kwamba Azam, Singida na sisi wote tumetamani sana hali hiyo.
Swali linalobakia ni lile lile. Ajibu anaweza kutimiza kila ambacho tunakiona kutoka kwake? Kwa mfano, wakati akitoka Yanga kurudi Simba tuliamini kwamba alikuwa ana hasira ya kwenda kuwaonyesha kina Clatous Chama yeye ni nani. Kwamba baada ya kina Chama kusifiwa sana Simba kwa kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika yeye alikuwa na uwezo zaidi yao.
Azam walimchukua wakiamini kwamba alikuwa na hasira dhidi ya benchi alilopigwa Simba. Kwamba labda Simba ilikuwa na wachezaji wao waliokaririwa akina Chama na ikawa sababu ya yeye kunyimwa nafasi. Hata hivyo baadae Azam hawakuona hasira yoyote katika moyo wa Ajibu.
Rafiki zangu Singida nao walifikiria hivi hivi. Haikuwezekana. Na sasa ni zamu ya Coastal. Kuna vitu viwili ambavyo vinanichekesha katika ndoa ya Ajibu na Coastal. Kwanza kabisa ni ni kwamba wote ni viburi na wanajisikia hasa. Ajibu anajisikia. Anajua kwamba ana kipaji na hataki kubabaishwa.
Coastal nao wana tabia hii. Hawa ni Wajomba zangu. Wadigo, Wabondei na Wasambaa. Wana viburi vyao. Nimewahi kuwa msemaji wa Coastal Union. Najua tabia zao. Hawana muda wa kumdekeza mtu wala kuvumilia dharau za mtu. Lakini watake wasitake na wao wameingia katika mkumbo wa timu zilizowahi kufikiri zinaweza kumbadili Ajibu. Kila la kheri kwao.
Ambacho naelewa ni wakati wakifikiria kupambana hivi, hii itakuwa timu ya kwanza kwa Ajibu ambayo haitakuwa na huduma kubwa nzuri kama timu zote kubwa za Ligi Kuu ambacho amewahi kucheza. Ana hasira? Atajibu mapigo? Ni swali la kusubiri na kuona.