Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kila mtu naashinde mechi zake Ligi Kuu

102382 Pic+yanga Kila mtu naashinde mechi zake Ligi Kuu

Mon, 8 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JUMAMOSI ijayo, rasmi Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea na mechi zake zilizobaki kumalizika msimu wa 2019/20, baada ya kusimama tangu Machi 17, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19, unaosababishwa na virusi vya corona.

Ugonjwa huo uliosambaa duniani kote, ulisababisha ligi nyingi kuvunjwa na zingine kusimamishwa, huku Ujerumani ikiwa nchi ya kwanza duniani kurejesha ligi yake.

Hapa Tanzania, baada ya kazi kubwa ya udhibiti wa ugonjwa huo na wagonjwa kupungua, hatimaye serikali imerejesha tena michezo, ikiruhusu pia ichezwe nyumbani na ugenini kama ilivyokuwa awali, badala ya vituo kama ilivyotaka kufanyika.

Pia, Ligi hiyo itachezwa na mashabiki, badala ya kuchezwa uwanja mtupu kama ilivyopendekezwa mwanzo. Hata hivyo, mashabiki watakaoingia watatakiwa kufuata taratibu zote zinazotakiwa kiafya.

Tukirudi kwenye mitanange yenyewe ni kwamba timu zote zinakwenda kumalizia michezo yao zilizobakisha ili kujua hatima yao. Tayari Bodi ya Ligi imeshatoa ratiba na kila timu inakwenda kucheza mechi yake ambayo huenda ikatoa mwelekeo wa kule inakotarajiwa kuwa.

Hata hivyo, zitaanza mechi tano za viporo kwanza, kabla ya ligi hiyo kusonga mbele. Makocha wengi wameonyesha kutoridhika na hali ya utimamu wa miili ya wachezaji wao, hivyo wanapambana kurekebisha hali hiyo.

Hii ina maana mechi za mwanzo zinaweza kutoa matokeo yasiyotarajiwa na kila timu inatakiwa ipambane na hali yake iliyokuwa nayo na kila mtu akitaka kuwa kwenye na hali nzuri ni lazima ashinde mechi zake. Hizi ndizo mechi tano za viporo zitakazochezwa kuanzia Jumamosi na tathmini zake, kabla ya mechi zingine kuendelea kama kawaida.

1. Mwadui vs Yanga (Uwanja wa Kambarage)

Mechi hii ndiyo itakuwa ya ufunguzi baada ya corona na itachezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga Juni 13, ikiwa ni moja kati ya mechi mbili siku hiyo.

Ni mechi ya mzunguko wa kwanza, iliyopaswa ichezwe kwenye raundi ya 17, kwani Yanga haijacheza na Mwadui hata mechi moja. Inatarajiwa kuwa kali na ya kusisimua kwa sababu wenyeji huwa kama mbogo wanapokuwa kwao.

Yanga itaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa, ikikumbuka kuwa watani zao wa jadi kwenye uwanja huo huo walichakazwa bao 1-0, Oktoba 30, mwaka jana, ikiwa ni mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.

2. Coastal Union vs Namungo (Uwanja wa Mkwakwani)

Juni 13 kwenye Uwanja wa Mkwakwani kutakuwa na kipute kingine cha ufunguzi kati ya wenyeji Coastal Union dhidi ya Namungo FC kutoka Ruangwa mkoani Lindi.

Ni moja ya mechi za kusisimua ya kiporo cha raundi ya 29, pia ya kisasi. Ikiwa ugenini, Namungo itakuwa na kazi ya ziada kutaka kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1 nyumbani mechi ya mzunguko wa kwanza, Novemba 22, mwaka jana. Hata hivyo, timu zote haziko eneo salama kwenye msimamo wa ligi.

3. Simba vs Ruvu Shooting (Uwanja wa Taifa)

Mabingwa watetezi Simba kwa mara ya kwanza wataingia uwanjani Jumapili, Juni 14, wakiwa na mkakati wa kutaka kuchukua ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo dhidi ya Ruvu Shooting, ikiwa ni mechi ya raundi ya 29.

Haitokuwa mechi rahisi kwa Ruvu Shooting ambayo ina rekodi mbovu inapocheza na Simba, tena wakati mwingine ikipoteza kwa idadi kubwa ya mabao.

Hata, msimu huu zilipokutana kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza, Novemba 23, Simba iliitandika Ruvu Shooting mabao 3-0, hivyo itakuwa na kazi ngumu ya kubadilisha rekodi hiyo.

4. Azam FC vs Mbao FC (Uwanja wa Azam Complex)

Azam itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex kucheza dhidi ya Mbao FC kutoka mjini Mwanza mechi ya raundi ya 29. Utakuwa ni usiku mgumu kwa Mbao, ambayo inapigana kufa na kupona kuhakikisha inabaki Ligi Kuu.

Timu hiyo ambayo haiko kwenye nafasi nzuri, ikishikilia nafasi ya 19, itakabiliana na timu ambayo bado inasaka ubingwa, lakini ikijiweka sawa na Kombe la FA. Huenda bahati nzuri kwa Mbao ni Azam kutokuwa na baadhi ya wachezaji wake tegemeo ambao wamekwama nchini kwao kutokana na karantini ya virusi vya corona. Mechi ya kwanza iliyochezwa Novemba 23, Uwanja wa Mkwakwani, Azam ilishinda kwa bao 1-0.

5. JKT Tanzania vs Yanga (Uwanja wa Jamhuri)

Yanga itasafiri hadi Mji Mkuu Dodoma kucheza dhidi ya JKT Tanzania Uwanja wa Jamhuri kwenye mechi ya kiporo raundi ya 29. Ni moja kati ya mechi mbili za viporo za Yanga ilizokuwa nazo.

Rekodi inaturudisha nyuma kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza, Yanga ilipoichapa JKT Tanzania mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Novemba 22, mwaka jana.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha kuwa JKT Tanzania huwa haina ubavu inapocheza dhidi ya Yanga. Kinachoweza kuibeba JKT Tanzania, labda ni kucheza kwenye uwanja mgeni kwa Yanga wa Jamhuri, tofauti na miaka yote ambapo imekuwa ikicheza mechi zote Uwanja wa Taifa au Uhuru jijini Dar es Salaam na si vinginevyo.

Columnist: www.tanzaniaweb.live