Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kijiwe cha Salim Said Salim: Mrembo wa Guantanamera

Mrembo Guentamara Mrembo wa Guantanamera

Tue, 24 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Siku hizi mara nyingi watu wakiandamana kudai utawala wa kidemorasia, kulalamikia kupanda gharama za maisha wanaimba wimbo wa Guantanamera.

Wimbo huu sasa umechagiza kusikika katika harakati za kisiasa za kutaka mabadiliko katika baadhi ya nchi za Amerika ya Kusini, hasa Brazil na Peru.

Lakini hata katika nchi za Asia waandamanaji huutumia wimbo huu ambao pia husikika katika viwanja vya michezo mashabiki wanapofurahia ushindi.

Kama kipo kitu kilichoipa Cuba maarufu kwa kukisafirisha nje baada ya sukari ni Wimbo wa Guantanamera ambao ulisikika Qatar wakati wa fainali za Kombe la Dunia.

Wimbo huu unaojulikana kama ‘Guajira Guantanamera,’ ambao maana yake ni msichana wa kijiji cha Guantanamo inasifika kama moja ya wimbo bora kupendwa duniani katika miaka zaidi ya 80 sasa.

Guantanamo ni kijiji kilichopo Cuba kilichopata umaarufu kunzia miongo miwili iliopita baada ya Marekani ambayo kwa miaka mingi inakikalilia bila ya ridhaa ya Serikali ya Cuba kukifanya kituo cha kijeshi chenye kambi ya kuwashikilia watu inayodai ni magaidi.

Watu zaidi ya 400 wa nchi tafauti (ikiwemo Tanzania), walizuiliwa katika nyakati tafauti katika kambi hii iliofunguliwa mwaka 2002 na Rais mstaafu wa Marekani, George Bush.

Katika kisiwa hiki wapo waliohukumiwa vifungo vya maisha na wengine hawajafunguliwa mashitaka mpaka leo na zimekuwepo taarifa za wafungwaa kuteswa.

Kisiwa hiki chenye ukubwa wa kilomita 10 za mraba kilichopo Jimbo la Ghuba ya Guantanamo kina historia ya aina yake ya uzalendo katika kupambana na ukoloni kupitia muziki.

Baadhi ya nyimbo ambazo chimbuko lake lina uhusiano na kisiwa na kuimbwa kila pembe ya dunia kwa sababu ya muziki wake nyororo na maneno yenye kuvutia. Moja ya nyimbo hizo unazoweza kusema ni miongoni mwa vitambulisho vya Cuba, baada ya zao la sukari, ni Guantanamera.

Kila mwananchi wa Cuba, mkubwa na mdogo, anaujua wimbo huu mwanzo mwisho na hupigwa katika sherehe za kitaifa na za kijamii.

Wazee wengi wa Cuba inapoimbwa wimbo huu hububujikwa machozi au furaha kwa kutegemea kumbukumbu ambazo mtu anazo uu ya wimbo huu wa Guantanamera.

Mwana mapinduzi maarufu wa Cuba, Ernesto Che Gueveara alipofika Zanzibar 1965 kwa sherehe za mwaka mmoja za Mapinduzi alifurahi vijana waliosoma Cuba walipomuimbia Guantanamera na kumaliza kwa kusema ‘Venceramos’ (Tutashinda).

Wimbo huu unaweza kusema umekuwa kama wimbo wa taifa usio rasmi wa nchi hiyo na ni kawaida Cuba inapocheza kandanda na kufunga bao au mmoja wa wanariadha au mwana masumbi wake kushinda watazamaji huinuka na kuimba Guantanamera kufurahia.

Mashabki wa timu za Ulaya na hasa katika viwanja vya Uingereza nao huimba Guantanamera kuishangilia timu yao. Miongoni mwa mashabiki ambao wanaoupenda zaidi wimbo huu ni wa klabu ya Norwich.

Wimbo huu ulioibuka unazungumzia mahaba yaliomzunguka msichana mrembo wa shambani wa Kisiwa cha Guantanamo na hii leo imo katika maktaba ya nyimbo za karibu kila kituo cha radio na televisheni duniani.

Umaarufu wake ulipanda chati pale mwimbaji maarufu wa Cuba, Joseito Fernandez, alipouimba katika kipindi chake maarufu cha radio katika miaka ya 1930.

Vibwagizo vya mwanzo vya wimbo huu vilitungwa na mmoja wa mashujaa wa mapambano ya kupigania uhuru wa Cuba katika karne ya 19, Jose Marti. Miaka kama minane iliyopita Cuba ilizindua sanamu la shaba la Jose Marti waliopewa na Marekani kama kielelezo cha kujenga daraja la kurejesha urafiki na maelewano kati ya nchi hizi mbili. Sanamu hili linaonyesha sura ya Marti siku chache kabla ya kifo chake 1895 baada ya mapambano ya muda mrefu ya kutaka uhuru kutoka kwa Hispania.

Marti aliyekaa Marekani kwa miaka 15 kama mkimbizi wa kisiasa alitajwa na Baba wa Taifa la Cuba, Fidel Castro, kama msomi na mtunzi wa vitabu na mashairi aliyesaidia kufanikisha Mapinduzi ya Cuba ya 1959.

Masanamu yake mengi hivi sasa yapo katika sehemu mbalimbali za Cuba na maofisini. Majengo mengi pia yamepewa jina lake. Jose Julian Marti Perez, alizaliwa Havana, Cuba, Januari 28, 1853 na kufariki Mei 19, 1895 katika mapambano ya Dos Rios, Jimbo la Oriente, ya kupigania uhuru wa Cuba kutoka kwa wakoloni wa Hispania.

Sasa nielezee kilimo ndani ya hii wimbo huu wa msichana wa shamba ‘Guantanamera’ aliyekuwa mwingi wa haya na kuchoshwa na udangayifu na mateso aliyopata kutoka kwa mpenzi wake na kuamua kuachana naye. Kipande hiki kilitafsiriwa na wananchi wa Cuba kuelezea kuchoshwa na mapenzi ya udanganyifu ya Wahispana na ndio wakaamua kudai uhuru wao.

Katika wimbo huu huyu dada wa shamba analalama umefika wakati wa kutaka haki na wana mapinduzi wa Cuba nao wakakitumia kipande hicho kuonyesha na wao walichoshwa na wakoloni wa Hispania na hivyo kudai kuwa huru.

Hapo ndipo wimbo wa asili ulipofanyiwa marekebisho madogo, lakini kwa muziki, lahaja na mahadhi yaleyale kwa kuweka beti isemayo: Mimi ni mtu mkweli kutoka nchi hii ya minazi (Cuba ina minazi mingi).

Kabla sijaiaga dunia nataka niwe huru. Siku hizi wananchi wa Cuba huiimba katika harakati za kutaka Marekani iwarudishie Kisiwa cha Guantanamo kiwe huru kama alivyotaka yule dada wa shamba wa Guantanamo.

Wamarekani pia huutumia wimbo wa ‘Guantanamera’ katika maandamano ya kupinga vita na kutaka amani au migomo ya wafanyakazi na wanafunzi. Wanawake wanaopambana na udhalilishaji na ubakaji hutumia wimbo huu katika harakati zao.

Marti ambaye alisoma Marekani aliandika vitabu vingi na kutunga nyimbo nyingi za kulaani uonevu tokea akiwa na miaka 15 na kufungwa mara kadha Cuba na Hispania. Mwaka 1892 Marti alichaguliwa kiongozi wa Chama cha Mapinduzi cha Cuba cha Partido Revolucionario Cubano (Cuban Revolutionary Party), lakini alilazimisha kuitwa ndugu na sio Rais au Mwenyekiti. Alidhika sana pale alipoitwa mheshimiwa au bwana.

Wimbo huu unawapa furaha mamilioni ya watu wanaposhangilia ushindi, ukiwamo wa michezo.

Kwa upande wa Watanzania wimbo unaoweza kusema zinaufukuzia kwa mbali wimbo huu wa Guntanamera kwa vile hupigwa na kufurahiwa katika nchi nyindi dunia ni Malaika, Georgina na Nilikupenda sana. Lakini Guantanamera ni kiboko.

Columnist: Mwanaspoti