Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kijiwe cha Salim Said Salim: Hii ndio asili ya hat trick

Kijiwe Cha Salim Pic Hii ndio asili ya hat trick

Fri, 6 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika fainali za 22 za Kombe la Dunia zilizomalizika Qatar wachezaji wawili, Concalo Ramos wa Ureno na Kyllian Mbappe wa Ufaransa ndio walioibuka na kile ambacho kwa kimombo kinaitwa ‘hatrick’, yaani kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja.

Hawa wawili wameifanya idadi ya wachezaji kufunga hatrick kufikia 54 katika michezo zaidi ya 800 tokea mashindano kuanza 1930 kule Uruguay.

Kwa bahati mbaya sikumbuki katika miaka ya karibuni kusoma au kusikia maelezo ya kina ya nini hasa hat trick na historia yake ili kumwezesha shabiki wa kandanda kuelewa kwa undani suala hili. Kinachoandikwa au kuelezwa ni kwa mchezaji kupata hat- trick na sio zaidi.

Leo nitazungumzia chanzo cha hili neno hat trick. Nilipoanza kuandika habari za michezo miaka ya 1960 neno ‘hat- trick’ lilinikanganya kwa vile neno hat kwa Kiingereza ni kofia na hiyo trick ina maana ujanja au hadaa. Nlijiuliza upo uhusiano gani wa kofia na ujanja katika kufunga hayo mabao matatu?

Wakati ule zilitolewa tafsiri tofauti na mashirika ya soka ya kimaifa na wataalamu wa kandanda. Utata uliongezeka juu ya historia na asili ya neno hili hat-trick. Vyama vya michezo vingi hadi leo vipo katika mvutano wa kila mmoja kudai asili yake inatokana na mchezo wao.

Wachambuzi wa kandanda wengi hupenda kusema nchi zao ndio ziliobuni neno hili. Ninakumbuka utata uliozuka juu ya hat trick katika mkutano uliofanyika chumba cha habari cha Tanganyika Standard (sasa Daily News) katika Barabara ya Maktaba, jijini Dar es Salaam mwaka 1967.

Mhariri wetu, Ken Ridley (Muingerea) alituuliza nini maana ya hat trick. Tulikuwa watu zaidi ya 20 katika mkutano, thuluthi nusu yake wazungu kutoka Uingereza, Ireland, New Zealand na Australia.

Miongoni mwao tulikuwepo waandishi wa michezo kama watano. Pamoja na mimi ni Hadji Konde, mwandishi wa kujitegemea Chris Ndakaba na John Gardener (wote marehemu).

Kila mmoja alitoa tafsiri yake na hatimaye tulikubaliana hakuna aliyeelewa maana halisi ya neno hili na historia yake, isipokuwa tulilitumia tu kila alipotokea mchezaji kufunga mabao matatu.

Kila nilipokwenda kwenye michezo ya kimataifa nje ya nchi niliwauliza waandishi wa michezo waliobobea maana ya hat-trick. Kila mmoja alinipa maelezo tofauti, kama nilivyoona katika kile kikao cha ofisini.

Tokea mwanzoni wa karne hii nilijitahidi kumaliza kiu yangu ya kuelewa maana na historia ya neno hili, lakini bado sijapata jawabu iliyoniridhisha.

Nilichobaini kupitia niliyoelezewa kwa mdomo, niliosoma kwenye vitabu, niliyokuta katika mitandano na njia nyengine ni utata, hasa juu ya asili na tafsiri ya hat-trick.

Wapo wanaosema chanzo ni katika mpira wa magongo kwenye Uwanja wa barafu, lakini wapo wanaodai ilitokana na mchezo wa kriketi. Lipo kundi linalosema chanzo ni katika kandanda na wengine wanadai ni kutokana na mchezo wa mpira wa kikapu.

Kila upande unayo maelezo ya kuvutia yenye tarehe na maelezo mengi kutaka kuthibitisha msimamo wao.

Katika kitabu ch Cricketers Annual kilichoandikwa mwaka 1877 na James Lilly inaelezwa chanzo chake kilitokana na siku moja mchezaji kuchukuwa wiketi sita kwa kurusha mipira saba. Baada ya mafanikio hayo huyo mchezaji alivua kofia yake (heti) mara tatu na kuivaa. Lakini pia inaelezwa miaka 10 kabla ya hapo mchawi mmoja aliyekuwepo uwanjani katika mchezo wa kandanda alivua na kuivaa tena mara tatu kofia yake aliposhangilia hayo magoli matatu yaliyofungwa na mchezo mmoja.

Falsafa nyengine ni kuwa matumizi yake yalianza katika mchezo wa mpira wa magongo mwaka 1858 katika Uwanja wa Hude Park, Uingereza .

Kwa mujibu wa simulizi, mchezaji aitwaye Stephenson alipopewa zawadi ya kofia kwa kuwatoa wachezaji watatu, mmoja baada ya mwengine kwa kuwarushia mipira mitatu na kila mmoja kugonga vile vijiti vitatu.

Wengine wanadai lilitokana na mchezo wa mpira wa magongo kwenye barafu ilipokuwa kawaida (hailezwi wakati) kule Amerika ya Kaskazini kuona mashabiki wanavua kofia na kuzirusha uwanjani mchezaji alipofunga mabao matatu.

Vilevile yapo maelezo kuwa mfanya biashara wa duka la kuuza kofia katika Mji wa Toronto, Canada, alikuwa na kawaida katika miaka ya 1940 kumzawadia kofia mchezaji aliyefunga mabao matatu katika mchezo mmoja.

Hadithi nyengine ni ya klabu moja ya Canada ya kiwanda cha kutengenezea kofia iligawa kofia kwa mashabiki katika mwaka 1946 kila alipotokea mchezaji kufunga mabao matatu.

Kubwa zaidi ni kwamba upo utatanishi wa hat-trick. Wapo wanaosema mabao yote matatu katika soka au mpira wa magongo lazima yafungwe katika kipindi kimoja, cha kwanza au cha pili na sio mawili kipindi kimoja na kipindi chengine au katika muda wa nyongeza.

Katika kriketi wengine wanasema hat-trick hupatikana katika mzunguko mmoja wa kurusha mipira sita na wengine katika mchezo mzima, uwe wa muda wa siku moja au tatu.

Katika kandanda ndio upo mkorogo. Wapo wanaosema hat-trick hupatikana kwa mchezaji kufunga mabao matatu mfululizo bila ya wapinzani kupata bao wakati amefunga hayo mabao matatu.

Lakini wapo wanodai ni kwa muda wote wa mchezo, ikiwa pamoja na wakati wa nyongeza au panapokuwepo mpira wa adhabu. Hili goli la mpira wa adhabu lina utata kutokana na wapo wanaosema linahesabika na wengine wanaosisitiza kuwa halistahiki kuhesabiwa.

Huu mvutano katika kandanda unakwenda mbali zaidi. Lipo kundi linalosema hizi hat-trick zipo za dhahabu, fedha na shaba.

Hii ya shaba wanasema ni ya mabao matatu yaliofungwa kwa njia yoyote ile, iwe yote kwa mguu au kwa kichwa. Ile ya fedha ni mchezaji anapopata magoli mawili kwa mguu wa kulia au kushoto na moja kwa kichwa.

Hat trick ya dhahabu ni ya mchezaji kufunga bao moja kwa mguu wa kulia, moja mguu wa kushoto na jengine kwa kichwa.

Katika sakata hii ninakumbuka sokomoko aliozusha mwaka 1969 aliyekuwa kocha wa kikosi cha England kilichobeba Kombe la Dunia 1966, Alf Ramsey mwaka 1969.

Ramsey aliuliza: “Jee kama mchezaji atafunga bao moja kwa mguu, la pili kwa kichwa na la tatu kwa kifua itakuwa hat trick ya almasi?

Wapo waliouliza panapotokea mabao yote matatu kufungwa haraka haraka kama alivyofanya Alex Torr wa England katika Ligi ya Jumapili ya nchi hiyo kwa kutumia sekunde 70 itakuwa hat trick ya aina gani?

Torr alikuwa akiichezea Ross County ilipokutana na Narin County tarehe 28 Novemba, 1964.

Uholanzi iliwahi kusema inahesabu mchezaji kupata hat-trick kama amefunga mabao yote matatu katika nusu moja ya mchezo. Bao la tatu linalofungwa Ujerumani katika muda wa nyongeza huhesabiwa, tofauti na ilivyo katika nchi nyingi za Ulaya.

Ni kawaida katika nchi nyingi mchezaji anayefunga mabao matatu katika mchezo mmoja kukabidhiwa mpira uliotumika kuuchukua nyumbani kama kumbukumbu.

Katika miaka ya karibuni zimekuwepo hat- trick nyingi, lakini zipo ziliohesabika kuwa za kiufundi na kutolewa mfano kama uwezo mkubwa wa mchezaji.

Miongoni mwao ni ya Syndey Leourex wa timu ya wanawake ya Marekani wakati walipoifunga Mexico 7-0 mwezi Januari , mwaka 2013.

Dada huyu alifunga bao la kwanza kwa kichwa, la pili kwa mguu wa kulia na la tatu kwa mguu wa kushoto. Alifunga mabao yote matatu katika dakika 19 za kipindi cha kwanza.

Karibu na mpira kumalizika aliongeza bao la nne na kusema hakutaka liingie katika hesabu kwa vile alikuwa anafanya mazoezi.

Cristiano Ronaldo alipokuwa na Real Madrid alifunga hat trick yake ya 19 katika Ligi ya Hispania walipocheza na Getafe karibu miaka minne iliopita. Bao moja lilikuwa kwa mguu wa kulia, jingine kwa mguu wa kushoto na moja kwa kichwa.

Columnist: Mwanaspoti