Mikasa iliyomkumba kiungo Abdulswamad Kassim Ali baada ya kusaini Simba ndio iliyomfanya ayamalize kimya kimya, licha ya kuzungumziwa maneno mengi yaliyo nje na ukweli wa mambo.
Baada ya kimya kirefu, anafunguka kwa mara ya kwanza wakati anafanya mahojiano na Mwanaspoti, akiwa kwao Zanzibar akikipiga Mlandege ambapo anaeleza kitu gani kilimuondoa Simba na kwa nini hakudumu Ruvu Shooting ambako alisaini miezi sita. Anaanza kueleza mikasa aliyopitia huku akikiri kuona kila aina ya maneno yaliyokuwa yanaelekezwa kwake, baadhi ya mashabiki wakidhani kiwango chake kiliisha kutokana na kulewa sifa baada ya kusaini Simba.
Anakunja ndita, macho yake yamejawa machozi anaanza kwa kusema; "Kuna wakati mwingine unaacha upepo mbaya upite hata kama una uwezo wa kujibu kile kinachozungumzwa kuhusu wewe.
"Kifo cha Zacharia Hans Poppe, kwangu kilikuwa kikubwa mno ni kama kiliondoka na kiwango changu Simba, maana baada ya hapo kila kitu kiliharibika, nilikosa mwanga, nilipoteza matumaini ila nikamwachia Mungu maana kila jambo linakuwa na sababu nyuma yake," anasema.
Anafunguka mengi mazito na jinsi ambavyo mwaka jana ulivyokuwa mbaya kwake hata alipojaribu kusahau kifo cha Hans Poppe na kuanza maisha mapya Ruvu Shooting, mechi ya kwanza tu akala umeme, hajakaa sawa akapoteza mama yake.
POPE, MAGOLI WALIVYOMNASA KAGERA
“Nakumbuka tulicheza mechi ya mzunguko wa pili na Simba, Kagera tulifungwa mabao mawili lakini ukiniambia nikutajie mechi yangu bora tangu nimeanza kujihusisha na soka sitaacha kuitaja mechi hiyo,” anasema na kuongeza;
“Nilikuwa bora sana kwenye mchezo huo nilicheza vizuri mno sijisifu lakini kila mchezaji huwa anatambua siku akifanya vizuri au akikosea basi siku ya mchezo huo pamoja na kufunga nilikuwa bora sana eneo la kiungo.”
Anasema anakumbuka mabao kwenye mechi hiyo yalifungwa na Luis na Chris Mugalu lakini baada ya mechi wachezaji wa Simba walimfuata na kumpongeza.
“Haikuishia hapo tu viongozi pia walinitafuta alikuwa ni Marehemu Hanspope Mungu aendelee kumpumzisha mahala pema peponi na Magori (Crescentius) walinifuata na kunipongeza baada ya pongeze Pope aliomba namba yangu na kunihakikishia kuwa mimi ni mchezaji wa Simba na nitacheza,” anasema na kuongeza;
“Nakumbuka zilikuwa zimebaki mechi mbili kumaliza msimu niliumia mazoezini nikaaondoka kwenye timu na kuja Zanzibar nikiwa huku nilipigiwa simu na Pope kwa ajili ya kwenda kusaini nilifanikiwa kufanya hivyo baada ya ligi kumalizika Kagera Sugar walinitangaza kuachana na mimi, nilicheka sana kwa sababu tayari nilikuwa nimeshasaini Simba na nilikuwa bado sijatangazwa.”
ATELEKEZA MILIONI 60 SIMBA
Usajili wake ulifanywa kimyakimya Agosti 2, 2021, ndio alikamilisha dili lake na kuachwa kwake ilikuwa hivyohivyo mara baada ya kutangazwa kusaini miaka tatu na Simba kiungo huyo hakuonekana hata mechi moja akicheza mwenyewe anafunguka.
“Ni kweli sijapata nafasi ya kucheza tangu niliposajiliwa ndani ya timu hiyo nikitokea Kagera Sugar, nilipoteza kabisa mtu muhimu aliyenifanya nikasaini ndani ya timu hiyo na huo ndio ulikuwa mwisho wangu,” anasema na kuongeza;
“Baada ya Pope kufariki niliona ugumu wangu wa kuendelea kubaki ndani ya timu hiyo ambayo ilikuwa inaniweka benchi na baadaye walitaka kunitoa kwa mkopo ili wawe wananilipa nikiwa nje ya timu nilikataa na kuamua kuvunja mkataba ambao nakumbuka nililipwa mshahara wa miezi miwili kama sijakosea maana nilikasirika sana.”
Abduswamad anasema aliamua kuacha milioni 60 na kwenda kujaribu maisha sehemu nyingine ambapo alisaini Ruvu Shooting kwa miezi sita. Anasema akiwa katika maumivu makali ya kuachwa na timu ambayo aliamini angeweza kucheza na kutimiza malengo yake alipatwa na msiba mkubwa wa kuondokewa na mama yake.
“Nakumbuka sikumaliza msimu ambao niliusaini kwa miezi sita na kuamua kurudi Zanzibar kuanza upya kwani niliharibikiwa kwa matukio makubwa mawili kutokea ndani ya muda mfupi na ofa za nje ziliyeyuka kwani sikupigiwa simu hadi sasa.”
ZANZIBAR NI BRAZIL
“Zanzibar ni Brazil ni sehemu ambayo imebarikiwa vipaji kuna muda unakaa unaangalia vijana wanaochipukia unainamisha kichwa chini na kujikumbusha kuwa natakiwa kupambana bila hivyo nitaumbuka.
“Nasema ni Brazil kutokana na kubarikiwa vipaji ambavyo vinapenda kucheza mpira wa pasi na chini kama ilivyo kwa nchi hiyo kubwa niliyoitaja huwezi kukuta kiungo mbovu ni wachezaji waliokamilika vipaji kutoka kwa Mungu na siyo vya kufundishwa.”
Anasema kiungo huyo ambaye anatamba sasa Feisal Salum ‘Fei Toto’ wakitaka kuwapata basi wapo kama mia moja kwasababu anaamini kila siku wanazaliwa viungo ma hospitalini kwasababu ndio nafasi kubwa iliyo na vipaji Visiwani.
KUCHEZA NA FEI TOTO INAHITAJI AKILI
“Nimekutana na viungo wengi Bara na Visiwani lakini leo hii naomba kukiri kwamba Fei Toto ni moja ya mchezaji ambaye nikijua natarajia kukutana naye kwenye mechi yoyote najiandaa kikamilifu,” anasema na kuongeza;
“Nimecheza naye nikiwa Jang’ombe Boys na yeye akiwa JKU ilikuwa siku najua tuna mechi naye najiandaa wiki nikifanya mazoezi yangu binafsi hii ni kutokana na ubora wake ukienda kichwa kichwa anaweza kukutia mfukoni usionekane. Ukitaka kuonyeshana naye ufundi tumia akili na nguvu yupo vizuri utaumia wewe ukitaka ufundi basi uwe na akili ya mpira.”
MAPINDUZI BIASHARA KWA WACHEZAJI
“Mapinduzi kwa upande wetu wachezaji pamoja na kukosa medali na taji kutokana na miaka mingi kuchukuliwa na timu za bara wao wamekuwa wakonufaika kupata nafasi ya kuonekana na timu za bara,” anasema na kuongeza;
“Mimi nimeweza kucheza Bara kwenye timu ya ligi kuu baada ya kuonekana kwenye mashindano haya ya Mapinduzi nakumbuka nikiwa Malindi nilicheza mashindano hayo kwa ubora nikifunga mabao matatu nilionekana na kusajiliwa Kagera Sugar.”
RUVU vs MBEYA CITY
“Ni mechi ambayo imeingia kwenye kitabu changu cha kumbukumbu baada ya kucheza mechi yangu ya kwanza ya ligi nikiwa nimesajiliwa dirisha dogo mchezo wa kwanza tu nilipewa kadi nyekundu,” anasema na kuongeza;
“Kosa la kwanza halikuwa halali nilitakiwa kuonye tu lakini mwamuzi alinionyesha kadi ya kwanza ya njano nakumbuka siku hiyo mvua kubwa ilinyesha hivyo uwanja ulijaa utelezi nikiwa katika harakati za kuokoa nilimgusa mchezaji wa timu pinzani hapohapo mwamuzi alinipa kadi nyekundu nililia sana kwasababu haikuwa makusudi ni tukio ambalo lilisababishwa na utelezi.” anasema mchezaji huyo ambaye amewahi kupewa kadi tatu za njano katika maisha yake ya soka.
MWEMBENI CITY KAMA YANGA
“Nikiwa Mwembeni City ambayo ilikuwa inashiriki ligi daraja la pili kipindi hicho niliisaidia kwa kucheza mechi zote za ligi hiyo hadi tunapanda bila kufungwa, kwa upande wa Bara msimu ulioisha Yanga ndio walikuwa mabingwa na walicheza mechi zote za msimu bila kufungwa na kutwaa taji basi ndivyo ilivyokuwa kwa Mwembeni City."
ANDAMBWILE AHESHIMIWE SBS
“Ukiachana na Fei Toto ambaye nimekutana naye mara nyingi zaidi kwenye mechi za ushindani kuna kiungo mmoja fundi amekamilika sasa anakipiga Singida Big Stars, Azizi Andambwile jamaa anajua sana ukikutana naye akiwa fiti lazima ulale na viatu,” anasema na kuongeza;
“Jamaa hana kazi chafu, ni lugha yetu watu wa mpira anakaba na kushambulia kutokaba na kuwa na mashuti ambayo yanahama mstari mabeki wakiwa hovyo anatengeneza njia nzuri kwa washambuliaji kufunga,” anaeleza na kwamba anahitaji kupewa muda ndani ya SBS ili awe kama alivyokuwa Mbeya City.
SIMBA, YANGA ZINA UFALME WAKE
Wakati wadau wengi wakihoji vipaji vingi vinavyotoka timu ndogo vinapotea ama kufa vikifika Simba na Yanga lakini Abdul-Swamad anafunguka;
“Unajua kila timu ina mchezaji wake muhimu kikosini kuna wachezaji wamejijengea ufalme kabina ndani ya timu hasa Simba na Yanga huwezi ukatoka timu ya chini ukaingia moja kwa moja kikosini sio rahisi.
“Hivyo ni ngumu kwa mchezaji kuanza kuaminiwa na kupewa muda wa kucheza na ndio maana asilimia kubwa wamekuwa wakiishia kukaa benchi na baadae kuvunjiwa mkataba lakini sio kwamba walishindwa kuonyesha kwasababu ata ukipata nafasi ukicheza mechi moja ukakosea ndio basi hawakupi tena lakini hawajui kama mpira unaweza ukafanya kosa leo na kesho ukasawazisha na kuwa bora.”
MAUYA ALIPIGA BENCHI
“Msimu wangu wa kwanza natua Kagera Sigar nilimkuta Zawadi Mauya ndio panga pangua kikosi cha kwanza nilipambana kuhakikisha napata namba ya kucheza nilishindwa nikawa nasugua mbao tu,” anasema na kuongeza;
“Mungu mwema alisalijiwa Yanga ndio ilikuwa nafasi yangu ya kucheza ndani ya Kagera Sugar nafikiri na mimi nikajitengenezea ufalme wangu kikosi cha kwanza hadi naondoka ndani ya timu hiyo.” anasema Abdul ambaye anaamini kila kitu katika dua na si imani za kishirikisha zinazohusishwa na soka.
KIPIGO CHA 7-0
“Ulikuwa ni mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kati ya Simba na Ruvu Shooting ulichezwa Februari 16, 2022 tulifungwa mabao 7-0, ni siku ambayo kila mmoja alikuwa anainamisha kichwa chini, kocha aliumia sana.
“Ni kipigo ambacho sitakaa nikakisahau kwenye maisha yangu ya soka, sio kwamba tulizidiwa sana hapana tuliingia kwa kutokuwaheshimu wapinzani wetu na ukitaka kumiminiwa mvua ya mabao basi fanya makosa hayo kwa timu za Kariakoo.”