Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kifo cha Dwamena kuna kitu cha kujifunza

Raphael Dwamena Mchezaji wa kimataifa kutoka Ghana Raphael Dwamena (28) amefariki Uwanjani

Thu, 16 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Medani ya soka ilipata pigo Jumamosi iliyopita baada ya mwanasoka Raphael Dwamena, raia wa Ghana kuanguka ghafla uwanjani katika mchezo wa Ligi Kuu Albania kati ya klabu yake ya KF Egnatia na FK Partizani.

Tukio hilo lililotokea katika kipindi cha kwanza dakika ya 24 wakati timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1. Watoa huduma ya kwanza walifika uwanjani na kumpa huduma ya kwanza na haraka walimpeleka katika hospitali iliyopo karibu.

Baadaye ilibainika kuwa tayari ameshafariki dunia. Taarifa ya kifo chake ilitolewa na Shirikisho la Soka la Albania ikieleza kilitokana na kupata shambulizi la moyo kitabibu maarufu kama heart attack.

Mchezaji huyo aliyekuwa na umri wa miaka 28 alitua KF Egnatia, Januari 2023 akiwa mshambuliaji na aliongoza kwa ufungaji akiwa na mabao tisa katika michezo 11.

Video ya tukio hilo ilisambaa mitandaoni na kwa wadau wa soka lilionyenesha mshikamano thabiti wa timu zote kwani kila aliyekuwa uwanjani alijaribu kuwajibika kutoa na kuomba msaada zaidi.

Bahati mbaya siku yake Dwawena ilikuwa imefika. Pamoja na jitihada zote zilizofanyika ilishindikana kuokoa maisha yake. Lilikuwa ni tukio la kuhuzunisha Albania na kwa wadau wote wa soka duniani.

MAMBO YA KUJIFUNZA

Ukisoma maoni ya wadau wa soka mitandaoni kuhusiana na tukio hilo unapata picha kuwa kila mmoja anatambua umuhimu wa uchunguzi wa kina wa afya kwa wanasoka.

Wengi walisema ushauri wa wataalamu wa afya ungezingatiwa, lakini pasipo kufahamu kuwa kutokana na ukuaji wa teknolojia na maendeleo ya elimu ya tiba ni kawaida kukutana na maoni kinzani kwa madaktari.

Upimaji wa afya wa kina ndio uliobaini kuwa ana tatizo la kiafya ambalo lilibainika ni mapigo ya moyo kutokwenda sawa jambo lililosababishwa na hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo.

Pamoja ya kwamba hakuna binadamu ayeweza kuzuia kifo pale wakati unapofikia na wala marehemu halaumiwi kwa kile kilichotokea, kwani kifo ni fumbo ambalo hakuna anayeijua kesho yake. Kwa jicho la kitabibu tukitathimini tukio hilo linaweza kutupa funzo na hatimaye kuwa somo zuri kwa jamii na klabu zetu za soka ambazo zinapambana kufikia maendeleo makubwa ya soka.

Mtakumbuka katika makala za nyuma nimewahi kuandika kuhusu matatizo mbalimbali ambayo yanasababisha vifo vya ghafla kwa wanasoka wanapokuwa katika majukumu uwanjani.

Mojawapo wa matatizo ambalo linashika namba moja kusababisha vifo vya ghafla kwa wachezaji ni matatizo ya moyo.

Tatizo ambalo limesababisha kifo cha Dwawema linatajwa kuwa ni shambulizi la moyo na kusababisha moyo kusimama ghafla na kushindwa kutekeleza majukumu ya kusukuma damu.

Moyo ndio ogani kuu nyeti inayohusika katika kusukuma damu kwenda maeneo mbalimbali ikiwamo nyeti ya mwili kama vile ubongo, ini na figo.

HISTORIA YA UGONJWA

Mwaka 2019 mshambuliaji huyo alishauriwa na madaktari waliomfanyia tathimini ya kina ya afya kuachana na soka kutokana na matatizo ya afya ya moyo aliyobainika kuwa nayo.

Vilevile kuna historia nyingine ya kiafya 2017 wakati akijiandaa kutua Brighton ya England ambayo sasa inashiriki Ligi Kuu Englang na dili hilo lilivunjika.

Sababu iliyoelezwa ni kutokana na kushindwa kufuzu vipimo vya afya vilivyofanywa na jopo la wataalamu wa afya wa Brighton, hivyo klabu hiyo ikachomoa kumnunua.

Katika kupigania maisha 2020 alikubali kufanyiwa upasuaji na kupandikizwa kifaa maalumu kinachotoa umeme ili kusahihisha hitilafu ya mapigo ya moyo yanayodunda bila mpangilio.

Kifaa hicho kinajulikana kitabibu kama Automated Cardiovascular Defibrillator. Kifaa hicho kilimletea nafuu kiasi cha kuonekana kumudu kucheza bila shida.

Mwaka 2021 mshambuliaji huyo aliyekuwa na kiu ya kufika mbali alianguka uwanjani na kupoteza fahamu dakika kadhaa nchini Australia.

Alipewa huduma ya dharura na kupelekwa katika huduma za juu za afya na ilibainika kuwa chanzo cha kuanguka kwake ni uwepo wa tatizo katika moyo wake.

Hapa tunapata picha kuwa mchezaji huyo alifahamu kuwa ana tatizo la kiafya na alishauriwa kuacha soka, lakini inawezakana kwa kuwa soka la kulipwa ilikuwa chanzo cha kipato chake alishindwa kuacha.

Pia tunapata picha kuwa pengine alipewa ushauri mwingine kuwa aachane na soka la ligi ngumu na badala yake aende katika ligi nyepesi kama ile aliyocheza ya Albania.

Siyo mchezaji wa kwanza kushauriwa kuachana na soka kutokana na tatizo la moyo kuna Sergio Aguero ambaye 2021 akiichezea Barcelona alianguka uwanjani kwa tatizo la moyo.

Aliamua kukubaliana na ushauri wa madaktari wa kuachana na soka. Dwamena alikuwa na ndoto ambazo angependa kuona anazifikia hata kwa kujihatarisha akiwa na tatizo la moyo.

Kawaida matatizo ya moyo huwa ni yaliyojificha na yanayoweza kuja na kupotea. Na siyo yote ambayo yanaweza kupona kwa upasuaji au dawa na kumfanya mchezaji awe timamu na kurudi kucheza soka. Matatizo hayo ya moyo yanayowapata wachezaji ghafla na kuangua uwanjani ndio ambayo yalichangia Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kutoa mwongozo mpya wa upimaji wa kina wa afya ya moyo.

Ilihitajika mshauri nasaha nguli ambaye angeweza kumpa ushauri ambao ungeweza kuwa mbadala hatimaye kumuondoa Dwamena kucheza soka wakati ana tatizo.

Pengine badala ya kucheza angejifunza ukocha - kazi ambayo isingeupa mwili hekaheka za kutumia nguvu na kasi jambo ambalo lingekuwa rafiki kwa afya ya moyo.

CHUKUA HII

Upimaji wa afya kwa wachezaji wa soka unaanza kabla ya kujiunga na shule za soka za awali.

Ni muhimu kushikamana na miongozo ya upimaji iliyotolewa na Fifa.

Ushauri wa madaktari uzingatiwe ili kuepukana na vifo au madhara ambayo yanaweza kuepukika.

Epuka kucheza ukiwa na tatizo la moyo kwani hatari ya kupata shambulizi la moyo na kufa inakuwa kubwa.

Klabu zina wajibu wa kusimamia maelekezo yanayotolewa na wataaalamu wa afya hasa wakati wa upimaji wa afya kwa wachezaji wanaowanunua kabla ya kuwapa mikataba.

Jamii ikiwamo wachezaji wa soka wanapaswa kuwa na ujuzi na ufahamu wa kutoa huduma ya dharura kwa mtu aliyenguka ghafla.

Columnist: Mwanaspoti