Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kifaa cha utambuzi wa madini kimepunguza imani za kishirikina

2afb811a118b3df990cc13e42de41aac Kifaa cha utambuzi wa madini kimepunguza imani za kishirikina

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KWA muda mrefu, uchimbaji wa madini unaoendeshwa na wachimbaji wadogo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa umekuwa wa kubahatisha.

Ikitokea mtu anachimba shimo la choo na kubahatika kukutana na madini ya aina yoyote ile, basi baada ya wiki, hilo eneo linakuwa limevamiwa na mamia kama siyo maelfu ya wachimbaji wadogo.

Lakini, Yona Mapesa, mchimbaji mdogo wa Shinyanga, anasema, katika harakati za kugundua ni wapi kuna madini, imani za kishirikina zimekuwa zikitawala sana.

Anasema uchimbaji ni jambo zito na hivyo wamekuwa wakitumia fedha nyingi kutafuta madini na muda mwingi na ndio maana baadhi ya watu wamekuwa wakijielekeza kwenye imani za kishirikina wakiamini zitawasaidia kubashiri mahala wanakoweza kupata madini mengi kwa haraka.

Moja ya mbinu hizo za kishirikiana anasema imekuwa ni kwa kuchinja kuku wa kafara kutoka kwa mganga na damu itakaporukia basi ndipo mchimbaji anaamini kutakuwa na madini ya kutosha.

Anasema ikitokea mchimbaji akabahatisha madini basi anaamini mganga wake ndiye kafanikisha wakati sio kweli.

Mchimbaji huyo anasema baada ya kupatikana kwa kifaa cha utambuzi na elimu ya namna ya madini yanavyoonekana, uendaji kwa waganga umepungua sana.

Mkurugenzi wa kampuni inayojishughulisha na biashara ya madini Aboubakar Kihondo ambaye pia mtaalamu wa miamba anasema kupitia kifaa cha utambuzi wa madini (Scanner) kinachobaini yalipo madini, umbali yalipo kwa kina cha chini au mbele kimekuja kuwaokoa wachimbaji wadogo.

Kihondo anasema amekuwa akifanya kazi ya utambuzi wa madini kwa wachimbaji wadogo kwenye maduara wanayochimba katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kifaa hicho cha utambuzi kimekuwa kikibaini madini ya aina mbali mbali kwa umbali wa kilomita tatu na mita 100 kwenda chini.

Anataja baadhi ya madini ambayo mashine hiyo inagundua kuwa ni pamoja na almasi, dhahabu, maji, madini ya vito na miamba tofauti tofauti.

Anasema kimsingi kifaa hicho kimekuwa kikisaidia kubaini kama kuna mali ardhini ijulikane na kama hakuna inajulikana pia.

Anasema wachimbaji wadogo wamekuwa wakikodi kifaa hicho kwa ajili ya kubaini madini katika maeneo waliopo kwa makubaliano fulani kutegemeana na hali ya eneo na umbali lakini gharama ya kununua kifaa hicho anasema ni shilingi milioni 60.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara mkoa wa Shinyanga (TCCIA), Meshack Kulwa, anasema: “Kazi ya madini imepiga hatua kubwa kiteknolojia kwani hivi sasa tumeona kifaa cha utambuzi kama madini yapo mbali au karibu au hayapo kabisa na hivyo wachimbaji wadogo hawana sababu tena ya kwenda kutapeliwa na waganga wa jadi.”

Kulwa anasema maonesho ya biashara na teknolojia ya madini yamesaidia kutoa fursa ya kuona mchakato mzima unavyofanya kazi ya uchimbaji madini kisasa mpaka kufikia hatua ya kuwa sokoni.

“Zamani baadhi ya watu tuliamini kazi ya madini ni kwa ajili ya watu waliokosa ajira au ni sehemu ya kwenda kupotezea muda na kujificha wakati umefanya uhalifu. Lakini sasa kazi ya madini ni yenye faida kubwa,” anasema Kulwa.

Kulwa anasema maonesho ya madini yanatoa fursa ya kupata elimu na kuondoa dhana mbovu kwa baadhi ya wachimbaji wadogo ikiwemo ya kwenda kwa waganga wa jadi kuangaliziwa yalipo madini.

Yona Mapesa anakiri kwamba uendaji kwa waganga wa kienyeji umepungua sana baada ya watu kuanza kutumia teknolojia hii ya utambuzi.

“Yaani mtu ulikuwa unatumia fedha nyingi za kuchimba, kuwalipa watu kumi wa kukuchimbia. Unawalisha ndani ya miezi miwili, mitatu au zaidi lakini mwisho wa siku haupati kitu chochote, lakini chombo cha utambuzi ukikitumia unajua kama madini yapo na hivyo uwekeze pesa zako au hapana,” anasema Mapesa.

James Madale, mkazi wa Shinyanga anasema anashukuru kuona wachimbaji wanazidi kupata elimu kwamba wapi wanaweza kupata mali tofauti na ule uchimbaji wa kiholela au wa kubahatisha.

“Wachimbaji wakubwa wamekuwa wakitumia kifaa cha utambuzi ili kuweza kubaini wapi kuna madini na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa ndivyo wanavyotakiwa wachimbaji wadogo wawe. Kinachotakiwa ni kushirikiana kwa kuchangishana pesa au kupata mikopo ili wamiliki kifaa hicho cha utambuzi kiweze kuwasaidia,” anashauri Madale.

Ramadhani Juma, Mhandisi wa Kampuni ya madini ya Zem Development (T) Co. Ltd, anasema madini ya dhahabu hivi sasa ni rahisi kuyachimba kwa kutumia teknolojia rahisi ambayo ni kuchimba mtaro mrefu wenye mita 500 na kina cha mita moja chini kwenye mtaro huo.

Juma anasema kuwa wamekuwa wakichimba mitaro hiyo na kuchukua michanga na kuipeleka maabara kwa ajili ya vipimo.

Anasema kampuni yao hutumia mashine maalumu ya kutoboa miamba (drilling machine) inayowawezesha kwenda chini ya miamba na kupata sampuli.

“Hiyo scanner (mashine ya utambuzi) wanayotumia wachimbaji wadogo inasaidia kujua kama kuna madini ardhini lakini haiwezi kujua yapo kiasi gani. Kwa kujua tu kuna madini, unaweza kuwekeza lakini mwisho wa siku unakuta umetumia gharama kubwa lakini manufaa kidogo lakini angalau kifaa kunasaidia kujua uwepo wa madini,” anasema.

Anafafanua kwamba mashine ya kutoboa miamba ndiyo humpa mahusika hali halisi ya mwamba iliyopo ardhini baada ya sampuli kwenda kupimwa kwenye maabara.

Fred Makwebeta, Ofisa Usalama na Afya za wafanyakazi kutoka mgodi wa Stamigold wa Biharamulo, anasema wao wameweza kupanua wigo kwa kushirikiana na wananchi kuwasaidia kufahamu madini yanapatikanaje na tija iliyopo.

Makwebeta anasema elimu ambayo wamekuwa wakiwapatia wananchi kutoka kwao kama mgodi wa serikali ni kuhusiana na utafiti wa madini, uchimbaji, uchenjuaji na usalama wao mahala pa uchimbaji.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack anasema kuwa mkoa huu kuanzia mwezi Julai hadi wakati anafanya mazungumzo na mwandishi wa makala haya, kilo zilizokuwa zimepatikana za madini ni 752 zikiwa na thamani ya shilingi bilioni 42.5.

Anasema kiasi hicho ni kikubwa kulinganisha na siku za nyuma na kwamba anaamini uzalishaji umeongezeka kutokana na teknolojia kama za utambuzi kuwafikia wachimbaji wadogo huku uzalishaji wa madini ukizidi kuwa wa kisasa.

Rais wa shirikisho la wachimbaji wadogo wa madini nchini (FEMATA) John Bina, anawaomba wachimbaji wadogo wajikite kwenye elimu na kutafuta teknolojia zaidi ili kufanikiwa.

Anazitaka pia taasisi za kifedha kuwawapatia mikopo wachimbaji wadogo kwani kutokana na kutumia vifaa vya utambuzi, sasa wana uhakika wa kupata fedha na kulipia mikopo yao.

Columnist: habarileo.co.tz