Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kichekesho cha kufungiwa Aziz KI na Clatous Chama

Chama Aziz Chama na Aziz KI

Wed, 16 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hadi tunavyozungumza, Stephane Aziz Ki, shujaa wa pambano la Yanga dhidi ya Club Africain pale Tunisia yupo katika mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadougou akiwa amepumzika na familia yake. Kisa? Amefungiwa.

Yanga waliamua kumpa ruhusa kwenda kwao Burkina Faso kwa sababu hawakuona haja ya kurudi naye. Amefungiwa mechi tatu na wakubwa. Kisa? Alikwepa kupeana mkono na watu wa Simba pamoja na waamuzi kabla ya mechi ya Simba na Yanga kuanza.

Majuzi nilikuwa nawatazama Simba pale Singida. Walirudi katika uzamani wao wa msimu uliopita. Kasoro Moses Phiri wachezaji wengine wa safu ya mbele walikuwa wale wale kina Ousmane Sakho na Kibu Dennis. Walikosa akili ya Clatous Chama. Kwanini Chama amefungiwa? Sababu ni hii hii ya Aziz Ki.

Jumamosi jioni Simba walikuwa wanacheza na timu inayoburuta mkia, Ihefu kutoka Mbeya. Wakakumbana na tatizo lile lile ambalo walikumbana nalo Singida. Kukosa ubunifu katika eneo la mwisho. Kisa? Binafsi naamini Chama hakuwepo.

Mambo yote yale ambayo unayaona magumu basi huwa yanakuwa rahisi kama Chama akiwemo. Lakini anakosekana kwa sababu kama ilivyo kwa Aziz Ki na yeye alikwepa kupeana mikono na wachezaji wa Yanga kwa sababu anazozifahamu mwenyewe.

Inashangaza kidogo. Kule kwa wenzetu kupeana mikono kabla ya mechi kuanza ni desturi ya hiyari. Ni mchezo wa kiungwana ‘fair –play’. Hakuna ulazima lakini kwa sababu za kiungwana basi wachezaji wanapeana mikono kabla na baada ya kumalizika kwa mechi. Haijawekwa katika kanuni.

Huku kwetu imewekwa katika kanuni. Walioweka wanashangaza, lakini waliopitisha pia nao wanashangaza. Hata hivyo sishangai sana kwa sababu watu wanaishi kwa mazoea. Hata pale Bungeni kuna watu walipitisha tozo halafu hao hao wakarudi kupinga tozo. Ni wale watalaamu wa kuitikia ‘ndioooo’ bila ya kuelewa madhara yake.

Kwanza kabisa hii haikupaswa kuwa kanuni. Ni suala la hiyari na mtazamo. Wakati mwingine haulazimishwi kumpa mkono mtu usiyempenda au kama kuna mazingira ambayo haujayapenda. Kwa mfano niliwahi kuandika mahala kwamba Aishi Manula akimuona Prince Dube anajipakaa mafuta ya Nguruwe ataweza kumpa mkono Dube? Imani yake inamkataza.

Lakini kuna wachezaji wana chuki. Inawezekana ni chuki kuanzia ngazi ya familia au mtaani au uwanjani. Ni kama ilivyotokea wakati John Terry aliposhutumiwa kumbagua Antoni Ferdinand. Mechi zilizofuata Antoni pamoja na kaka yake, Rio waligoma kumpa mkono Terry. Hakuna hatua ambazo zilichukuliwa dhidi yao.

Ni Terry huyu huyu alijikuta katika wakati mgumu wakati aliponyimwa mkono na Wayne Bridge ambaye alimshutumu kwa kutembea na mpenzi wake. Hakuna hatua yoyote ambayo Wayne Bridge alichukuliwa. Ulikuwa ni uamuzi wake.

Baada ya hapo kuna maswali mengine ya kujiuliza. Kwanini katika matukio kama haya wachezaji hawaitwi kuja kujitetea. Inawezekana wana sababu zao za msingi za kutofanya hivyo. Hii tabia ya kamati kujigeuza kila kitu katika masuala ya haki huwa inashangaza kidogo.

Na baada ya hapo tujiulize ukubwa wa kosa lenyewe. Bernard Morrison alimkanyaga kwa makusudi Lusajo Mwaikenda wa Azam. Aliishia kufungiwa mechi tatu. Metacha Mnata alimpiga kiwiko kwa makusudi Charles Ilamfya. Akaishia kufungiwa mechi tatu.

Hawa wawili hawajasalimia nao wamepewa adhabu ile ile tu. Lipi kosa kubwa lipi kosa dogo? Hawa wawili Morrison na Metacha walihatarisha afya za wachezaji wenzao na bado wakafungiwa mechi tatu tu. Hawa wawili hawakufanya kosa la kuhatarisha afya za wenzao na bado walifungiwa mechi tatu.

Sikubaliani na suala la Fair –play kuwekwa katika kanuni lakini hata kama limepitishwa basi ukubwa wa adhabu unashangaza. Mechi tatu za Simba kumkosa Chama zinaweza kuwanyima ubingwa ambao unagharimu mamilioni ya pesa. Kwanini isingeishia katika faini tu?

Wenzetu huko nje wakisikia kwamba sisi Fair Play tunafanya kuwa lazima watatushangaa sana. Wakazi wa Burkina Faso wakigundua kwamba Aziz Ki amerudi kwao kupumzika kwa sababu amefungiwa mechi tatu watashangaa sana.

Mechi tatu ni takribani mwezi mzima. Kama Simba na Yanga zitacheza kila Jumamosi ina maana Chama na Aziz Ki wanaweza kuwa wamekaa nje mwezi mzima kwa kosa la Fair Play. Inachekesha na nadhani tunaishi katika dunia ya giza.

Mwisho wa siku inachekesha pale watu wanapong’ang’ania kwamba kanuni zilikuwepo kabla ya hapo. Ndio zilikuwepo na wengine hatukuzisoma. Hata hivyo, hatukuamini tulipoletewa mezani kwetu adhabu hii kwa sababu haikuingia akilini kwamba inaweza kutungwa na watu wenye akili timamu.

Nadhani kinachotokea ni kwamba kuna mtu mmoja aliamini kwamba huenda kuna siku wachezaji watagomea kumpa mkono kiongozi fulani kwa sababu ya tabia zake za ovyo. Kwa ajili ya kujikinga na aibu hii wakaamua itengenezwe kanuni ya kulazimisha kupeana mikono na hivyo wakawajumlisha na wachezaji.

Tukirudi ndani ya uwanja kuna jambo moja limenichekesha kidogo. Adhabu ilipotolewa watu wa Yanga walishangilia zaidi kuliko watu wa Simba. Au tunaweza kusema kwamba watu wa Simba walihuzunika zaidi kuliko watu wa Yanga.

Kuna maswali nilijiuliza, ina maana hisia zao zilikuwa zinaamua ubishi wa kijinga uliojitokeza mwanzo wa msimu kwamba nani ni bora kati ya Chama na Aziz Ki? Kwamba Simba inaingiwa na pengo zaidi anapokosekana Chama pengine kuliko Yanga inavyoingiwa na pengo anapokosekana Azizi KI?

Hapa kunaleta hisia kwamba Simba hawana mbadala au mtu ambaye anakaribiana kiuwezo na Chama. Kwamba Yanga wanaweza kumchezesha Fei Toto katika nafasi ya Aziz Ki na maisha yakasonga mbele kama kawaida. Lakini Simba haina uwezo huo.

Au kwamba kwa ujumla Yanga inajivunia ubora wa kikosi chao chote bila ya kujali sana mchezaji anayekosekana wakati Simba hawana ubora huo na hasa anapokosekana Chama. Inawezekana kuna ukweli ndani yake hasa unapoangalia namna ambavyo Yanga bado walikuwa bora uwanjani pale Tunisia hata kabla ya kuingia kwa Aziz Ki.

Columnist: Mwanaspoti