Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kibailo kutoka mtaani hadi Namungo

Kidailo Kibailo kutoka mtaani hadi Namungo

Fri, 31 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Unaikumbuka ile timu ya Taifa Tanzania upande wa watoto wa mtaani waliochukua kombe nchini Brazil mwaka 2014 basi mbegu zake zimeanza kuota kwenye Ligi Kuu Bara.

Beki Hassan Kibailo aliyezaliwa Julai 23, 2000 anayekipiga katika klabu ya Namungo akijiunga nayo kwenye dirisha dogo la usajili ni miongoni mwa wachezaji ambao wametokea kwenye timu hiyo ya watoto wa mtaani na sasa anaendelea kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu hapa nchini.

Mwanaspoti lilimtafuta na kuzungumza naye kwa kina safari yake nzima ya soka hadi leo akiwa kwenye kikosi cha Namungo.

WATOTO WA MTAANI WAMPELEKA PAMBA

Kibailo ni mtoto wa mtaani na soka lake amelianzia huko huko katika timu ya Pasias Boys ‘Juma Kampong’ ya jiji Mwanza na baada ya hapo alienda katika akademi ya TSC na ndipo safari yake ya soka ikaanza.

Beki huyo anasema walipata nafasi ya kushiriki kombe la Dunia kwa watoto wa mtaani na walichukua ubingwa wakiwa nchini Brazil na hapo ndio maisha yake ya soka yalipoanzia.

“Niliporudi nilicheza Pamba na timu ikaingia kwenye hatua ya Playoff ndipo Coastal Union waliniona na kuvutiwa na huduma yangu baada ya hapo basi nikasaini nao,”anasema Kibailo na kuongeza;

“Nilikuwa mtu wa mazoezi sana nikiwa na Coastal Union, nilipata nafasi ya kucheza nikaonyesha nilichokuwa nacho na timu zingine zikaniona hivyo mkataba wangu ulivyoisha nikaamua kuondoka kwenda kutafuta changamoto nyingine.”

ATUA MTIBWA MAJERAHA YAMTIBULIA

Kibailo anasema baada ya kuondoka Coastal alipokea ofa ya Mtibwa Sugra lakini akiwa na timu hiyo alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kup[ata majeraha ya goti yaliyomuweka nje ya uwanja muda mrefu.

“Baada ya kusajiliwa Mtibwa sikuweza kudumu kwa muda sababu nilipofika sikua na msimu mzuri nilipata majeraha ya kuniweka nje kwa muda mrefu, mkataba wangu ulipoisha niliaachana nao na kurudi Mwanza kujiweka vizuri kwa sababu mtaji wa kweli kwetu sisi wachezaji ni Afya,”

anasema Kibailo na kuongeza;

“Kuna vitu vingine vilitokea lakini havina afya kuvizungumzia, kikubwa nilipona baada ya kujitibia na nikawa nafanya mazoezi mwenyewe mdogo mdogo hadi nikakaa sawa kabisa.”

TIMU ZAMTAFUTA AKIWA MGONJWA

Kibailo anasema baada ya kuumia akiwa na Mtibwa Sugar aliamua kupumzika lakini akiwa nje ya uwanja alijikuta akipigiwa simu nyingi na baadhi ya viongozi wakihitaji huduma yake.

Beki huyo anasema lakini maamuzi ya mwisho aliamua kusaini Namunggo kutokana na ukaribu na baadhi ya viongozi ambao walikuwa nae kwenye ukaribu mkubwa wa kujua hali yake wakati anaumwa.

“Nashukuru Mungu simu zilikuwa zinaita nilikua natafutwa kwa kile ambacho nilichokua nimekionyesha katika Ligi kwa muda nilocheza kuna klabu bado zilikua zinanitafuta kuulizia kama nimeshapona kuhitaji huduma yangu, “ anasema na kuongeza;

“Dili ya Namungo ilikuja nilitafutwa na uongozi tukakubaliana nao kwavile nishapona na nipo vizuri nikaamua kufanya nao kazi na nashukuru Mungu napata nafasi ya kuipambania ili tuwe sehemu nzuri.”

HUMWAMBII KITU KWA ALVES

Kibailo anasema kwa sababu yeye anacheza beki wa kulia basi beki ambaye anamvutia kwa Ulaya ni Dany Alves ambaye aliwahi kutamba katika klabu ya Barcelona na timu ya Taifa ya Brazil.

Beki huyo anasema anavutiwa na Alves kutokana na uwezo wake mkubwa kwenye ukabaji sambamba na kupeleka mashambulizi hali ambayo inawapa tabu wapinzani.

“Nje bhana yule Dan Alves anavyocheza anakaba na kushambulia na burudani anakupa kwahiyo navutiwa nae sana, napenda anavyocheza na kuna namuangalia na kuchukua baadhi ya vitu ili niwe kama yeye au zaidi,”anasema Kibailo.

AIWAZA TIMU YA TAIFA

Kibailo baada ya kucheza timu ya Taifa kwa watoto wa mtaani sasa anasema akili yake ameigeuzia kupata nafasi ya kucheza katika timu kubwa ya Taifa.

Beki huyo anasema yeye kama mchezaji ataendelea kufanya mazoezi na kujituma sambamba na kumtanguliza Mungu kisha watu wataona uwezo wake na anaamini atapata nafasi.

“Siri yangu ya mafanikio ni kujituma na mpira ni mchezo wa wazi na watu wataona, kikubwa kazi kamwe usimuache Mungu kwa sababu yeye ndio mpaji,”anasema na kuongeza;

“Muda wowote na wakati wowote nitakuwa kwenye timu ya Taifa kwa sababu ni ndoto ambayo inaninyima usingizi sana, kwenye soka nilichojifunza ni kutakiwa kuthamini muda.”

Columnist: Mwanaspoti