Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kibadeni na mambo yaliyobadilika Kariakoo Derby

Inonga Simba Yanga Kibadeni na mambo yaliyobadilika Kariakoo Derby

Wed, 19 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Juzi kulikuwa na mechi ya watani pale Temeke. Simba na Yanga. Hadi wakati naandika makala haya sifahamu matokeo yalikuaje, lakini nafumba macho na kuvuta picha nzito ya pambano hili tangu nikiwa kijana mdogo.

Nyakati zimekwenda wapi? Kuna mambo yamebadilika na kuna mambo hayajabadilika. Tuanze na jambo moja ambalo halijabadilika.

Labda libadilike jana kama Jean Baleke au Fiston Mayele mmoja wapo angefanikiwa kukabidhiwa mpira na dada Jonesia Rukyaa baada ya pambano kumalizika.Namaanisha kama mmoja wao akiondoka na hat trick. Vinginevyo kama hilo halikutokea jana basi hat trick pekee ya pambano hili inabakia kuwa ile ile ya King Abdalah Kibaden Mputa.

Mwaka huu hat trick yake imefikisha miaka 45. Ni kitu kinachoshangaza kidogo. Hii inaweza kuwa miongoni mwa rekodi ndefu katika soka.

Miaka yote hii wale wanaoitwa washambuliaji hatari walikuwa wapi kuvunja rekodi ya Kibadeni? Sijui. Kuna washambuliaji wamesifiwa hasa katika timu hizi lakini hadi sasa kuna Kibadeni mmoja tu. Kuna pambano ambalo Yanga ilichapwa 5-0 pale Uwanja wa Taifa. Ilikuwa Mei 6, 2012 katika mechi ya kufungia msimu, ambapo Simba ilikuwa tayari imeshabeba ubingwa wa Ligi Kuu mapemaa.

Katika miaka ya karibuni nusura, Emmanuel Okwi aondoke na mpira. Alishafunga mabao mawili halafu ikatokea penalti. Akaamua kumpa mpira kipa wake, Juma Kaseja aliyetupia.

Kama Okwi angekuwa mchoyo, au kama kuna mtu angemnong’oneza Okwi kwamba kuna rekodi ya miaka mingi inapaswa kuvunjwa, labda Okwi angekuwa mbinafsi.

Lakini, Fiston Mayele ile siku aliyofunga mabao mawili nusura pia aifikie rekodi ya Kibadeni. Kuna mpira ambao Aziz Ki alimpitisha tobo Mohamed Hussein 'Tshabalala' akampasia Mayele aliyekuwa anatazamana na nyavu, lakini kinara huyo wa mabao wa Ligi Kuu kwa sasa, akakosa.

Tutakaa na rekodi hii hadi lini? Vimepita vizazi vingi sasa na umefika wakati mchezaji mmoja akaifikia rekodi hii. Katika zama hizi pale barani Ulaya wachezaji wengi wamevunja rekodi mbalimbali zilizowekwa na kina Pele, Diego Maradona, Bobby Charlton na wengineo. Vipi kuhusu hii ya Kibadeni?

Tukiacha na jambo hilo la rekodi ambayo haibadiliki kuna mambo mengi yamebadilika kuelekea pambano la Simba na Yanga. Mbona siku hizi hawatoki kwenda kujificha mahala kuelekea siku ya pambano lenyewe? Zamani kama timu ingebakia hapa hapa Dar es Salaam basi ilikuwa inahalalisha kufungwa. Simba wangeenda Zanzibar halafu Yanga wangeenda Bagamoyo. Bila ya kujifungia ilikuwa inaondoa imani kwa mashabiki kwamba timu yao inaweza kushinda.

Ulikuwa ni usumbufu ambao haukuwa na maana yoyote ile. Ilikuwa ni tamaduni ya ajabu. Kwanza kabisa unawachosha wachezaji bila ya sababu za msingi. Unasafiri vipi kwenda mbali kujichosha wakati ungeweza kutulia tu.

Shukrani kwa Simba. Walikuwa timu ya kwanza katika miaka ya karibuni kuvunja utaratibu huu. Kuna pambano moja dhidi ya mtani waliamua kujichimbia katika kambi yao hapa hapa Dar es Salaam huku Yanga wakisafiri kwenda Zanzibar. Pambano lenyewe lilimalizika kwa sare.

Kuanzia hapo Yanga nao wakaiga. Kama Simba wangefungwa katika mechi ile si ajabu mechi ambayo ingefuata wangetoka jijini wakihofia kwamba maandalizi yao hayakuwa mazuri. Na si ajabu Yanga nao waliamua kuiga baada ya kuona Simba hawakudhurika na kitu chochote kubakia Dar es Salaam.

Kitu kingine ambacho kimebadilika kwa kiasi kikubwa kuelekea katika pambano hili ni suala la ushirikina na ishara zake. Wiki nzima hii watu wamekuwa wakijadili ubora wa Mayele na Baleke au ubora wa vikosi vyao. Zamani hali ilikuwa tofauti kidogo. Watu walikuwa wanajadili matokeo kwa hofu za kishirikina. Kuna mtu ambaye aliamini kabisa kwamba timu yake imefungwa kabla ya mechi kuanza, kisa? Mganga amesema.

“Nasikia mechi ngumu sana hii. Fundi ndio anajaribu kubadili matokeo.” Watu wangesemezana jambo hili. Nadhani kuna kupungua kwa imani hizi kadri kizazi kipya kinavyojitumbukiza katika soka. Enzi zetu tuliamini matokeo ya nje ya uwanja na sio ya uwanjani. Hamis Gaga aliwahi kukosa penalti katika pambano la watani akiwa na jezi ya Simba mwaka 1990 ikasemwa kwamba kama angefunga angekufa.

Leo hatusikii tena mambo hayo. Tunasikia vijana wakijadili zaidi ubora wa wachezaji wao. Kumbe tulikuwa hatuwatendei haki mastaa wetu wa zamani.

Badala ya kujadili ubora wao utakavyoamua mechi sisi tulikuwa tunajadili ubora wa waganga. Ni katika hili hili pia kuna watu walikuwa wanapoteza muda kwenda katika ofisi za FAT kulinda mpira ambao ungetumika katika pambano la Simba na Yanga.

Makomandoo walikuwa na kazi kubwa katika mipira. Leo naona hatulindi tena mpira kwa sababu kwanza mipira inayotumika ni mingi hivyo hatujui tuurogee upi.

Kitu pekee ambacho hakijabadilika ni kulinda vyumba vya kubadilishia nguo. Hilo sidhani kama litakuja kubadilika hasa katika nyakati hizi ambazo inadaiwa kwamba kuna timu zimekuwa zikipulizia dawa katika vyumba vya timu pinzani kwa ajili ya kumlegeza adui.

Kitu kingine ambacho kimebadilika ni presha kwenda kwa wachezaji. Kwa sasa hakuna presha kubwa kwenda kwa wachezaji kabla ya mechi. Hadi jana wakati pambano likitarajiwa kuanza hatukusikia habari ya kwamba Mayele amechukua hela au Aishi Manula amechukua hela. Wachezaji wanaishi kwa amani kidogo kambini.

Nilitazama wachezaji wa Yanga wakicheza michezo ya ajabu kambini huku wakicheka. Zamani hali ya hewa inakuwa ngumu kuelekea katika pambano hili.

Sio tu kwa wachezaji, hata kwa mwamuzi hali yake inakuwa ngumu kuelekea katika pambano hili. Presha inakuwa kubwa kwake, lakini zaidi ni kwa kuambiwa kwamba amepewa kitu chochote kwa ajili ya kuisaidia timu fulani kushinda mechi.

Lakini subiri kwanza. Kitu kingine kikubwa kilichobadilika ni kwamba zamani tulikuwa tunategemea maoni ya Charles Hillary au Ahmed Jongo kwa ajili ya kutueleza kinachotokea katika mechi. Hata kama mpira uko mbali wangeweza kutudanganya kwamba kulikuwa na hatari langoni.

Zaidi ya kila kitu wao ndio waliokuwa wameshikilia maoni kuhusu pambano zima hata kama hali haikuwa hivyo. Siku hizi kila mtu ana maoni yake. kila mtu anatazama katika televisheni na kutoa maoni yake.

Tunaweza kujua nani alitawala mechi hata kama tumezima sauti ya Baraka Mpenja. Hivi ndivyo maisha yalivyoenda kasi kuelekea katika pambano la jana. Kesho Mungu akinipa pumzi nitakueleza kilichotokea jana.

Columnist: Mwanaspoti