Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kibabe sana! Nigeria hawapo lakini ni kama wapo tu Qatar

Musiala Jamal Jamal Musiala

Sat, 3 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Nigeria kama taifa, imeshindwa kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia 2022 zinazoingia kwenye hatua ya 16 bora huko Qatar.

Kwenye mechi ya mchujo ya kufuzu ushiriki wa fainali hizo, Super Eagles ilikwama mbele ya Ghana kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya 0-0 katika mechi iliyofanyika uwanjani Baba Yara Sports mjini Kumasi, kabla ya ile ya marudiano iliyofanyika Abuja, iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, hivyo Black Stars ikakamatia tiketi ya Qatar kwa faida ya bao la ugenini.

Nigeria ikashindwa kwenda Qatar kama nchi, lakini hilo wala halina shida, kwani kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia 2022 kuna mastaa wao kibao wanapiga kazi ya maana kabisa kusaka ubingwa.

Shida ni kwamba wakali wake hao wapo Qatar wakiwa na vikosi vya mataifa mengine na hakika mambo yao ya uwanjani ni matamu balaa.

Baada ya vikosi kutajwa kwa timu zilizokwenda kukipiga kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia 2022, ambalo kimsingi ni tamasha kubwa kabisa la mchezo wa soka duniani, Nigeria haijafuzu, lakini kuna mataifa mengine kadhaa yameteua wachezaji wenye asili ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwenda kukipiga Qatar.

Fainali hizo za Kombe la Dunia 2022 zilianza Novemba 20 na zitafika tamati Desemba 18.

Wakati hatua ya makundi ya fainali hizo ikikamilika leo Ijumaa na kushuhudia mataifa kibao yakitupwa nje na kubaki 16 yakayoanza mchakato wa kutoana katika kuelekea ubingwa, Nigeria ikiwa zake nyumbani, ilikuwa na wakali wake saba kwenye fainali hizo.

Bukayo Saka -England

Kinda huyo wa Arsenal ameibukia kibabe kwenye soka misimu miwili iliyopita na hakika amekuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho cha Emirates chini ya Mikel Arteta kinachosaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Saka alizaliwa London na wazazi wa Kinigeria, alikuwa na ruhusa ya kuitumikia Nigeria kwenye soka la kimataifa, lakini badala yake aliamua kuchagua kuitumikia England na sasa yupo huko Qatar na ameshafunga mabao mawili.

Tangu aanze kuitumikia Three Lions mwaka 2020, Saka amecheza mechi zaidi ya 20 na uwepo wake umekuwa muhimu kwenye kikosi hicho cha kocha Gareth Southgate katika kusaka ubingwa wa dunia.

Manuel Akanji - Uswisi

Huyu ni staa mwingine wa Ligi Kuu England mwenye asili ya Nigeria anayekipiga kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar akiwa na uzi wa taifa jingine kabisa. Beki Manuel Akanji anayekipiga kwenye kikosi cha Manchester City, yupo zake Qatar akiwa mchezaji wa Uswisi, ambapo leo Ijumaa watafahamu hatima yao kwenye mchakamchaka wa kutinga hatua ya 16 bora kutokea kwenye Kundi G. Akanji baba yake ni Mnigeria na mama yake ni Mswisi.

Kutokana na hilo, beki huyo aliamua kuitumikia Uswisi kwenye soka la kimataifa, lakini bado alikuwa na uwezekano wa kuwa staa wa Super Eagles kupitia baba yake. Akanji alianza kuichezea timu ya wakubwa ya Uswisi mwaka 2017.

Noah Okafor - Uswisi

Ukimweka kando Akanji, kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uswisi iliyopo Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 kuna staa mwingine mwenye asili ya Nigeria anayeitumikia timu hiyo. Noah Okafor ni kama ilivyo kwa beki Akanji, ambapo na yeye wazazi wake waliomzaa, baba ni Mnigeria na mama ni raia wa Mswisi.

Mshambuliaji huyo, Okafor alizaliwa Binningen na aliichezea Uswisi katika ngazi zote za timu za vijana, kabla ya kuanza kuitumikia timu ya taifa ya wakubwa mwaka 2019. Amekuwa mchezaji muhimu wa taifa hilo kwenye fainali za Qatar, ambapo bao lake ndilo lililowapa tiketi ya kufuzu michuano hiyo.

Jamal Musiala -Ujerumani

Kama kuna kitu kilichokuwa kikivutia kuitazama Ujerumani ikicheza mechi zake kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, basi ni kumtazama mshambuliaji Jamal Musiala akiwa na mpira kwenye miguu yake. Lakini, kitu usichokifahamu ni kwamba Musiala ana asili ya Nigeria, hivyo alipaswa kuwa kwenye kikosi cha Super Eagles. Kinda huyo wa Bayern Munich ni fundi kwelikweli wa mpira na amekuwa na faida kubwa kwenye kikosi cha Ujerumani.

Akitokea kwenye akademia ya Chelsea, Musiala alizaliwa na baba mwenye asili ya Nigeria na England na mama yake ni Mjerumani. Alizaliwa Stuggart na alihamia England alipokuwa na umri wa miaka saba, kabla ya kuichezea England kwenye kikosi cha U-17. Lakini, baadaye aliamua kuachana na England na Nigeria na kwenda kuitumikia timu ya upande wa mama yake, Ujerumani. Mwaka 2022, Nigeria walijaribu kumshawishi achezee Super Eagles, akachomoa.

Karim Adeyemi -Ujerumani

Kama ilivyo kwa Musiala, timu ya Ujerumani iliyokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar ilimweka kwenye orodha kinda wa miaka 20, Karim Adeyemi na kwenda kukipiga kwenye fainali hizo akiwa na kikosi cha Ujerumani. Adeyemi alizaliwa na baba wa Kinigeria na mama Mromania huko Munich, Ujerumani.

Baba yake anaripotiwa kuhamia Ujerumani kwenye miaka ya 1990 na kuanza kucheza soka. Karim alianza kuchezea timu za vijana za Nigeria kabla ya kuhamia kwenye kikosi cha wakubwa katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Armenia, Septemba 5, 2021. Staa huyo, ambaye ni mshambuliaji wa Borussia Dortmund alijiunga na kikosi cha wakubwa cha Ujerumani, Mei 2022. Tangu aanze kuitumikia Ujerumani, amecheza mechi nne na alikuwa mmoja wa wakali wa huko Qatar 2022.

Ike Ugbo - Canada

Tukihamia Amerika Kaskazini, kuna wachezaji wawili wenye asili ya Nigeria wanakipiga kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Canada. Kwenye orodha ya mastaa wa Canada waliokuwa wakiunda kikosi cha timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 kulikuwa na jina la Ike Ugbo, anayechezea klabu ya Ligue 1 ya Troyes.

Staa huyo alizaliwa London na wazazi wa Kinigeria, lakini familia yake ilihamia Canada kipindi hicho akiwa na umri wa miaka mitano. Staa huyo alikuwa na uwezekano wa kuwakilisha mataifa matatu kwenye soka la kimataifa na aliitumikia England kwenye soka la vijana. Septemba mwaka jana, Ugbo alikubali kuichezea Nigeria, lakini miezi miwili baadaye alibalidi mawazo na kuanza kuitumikia Canada kwenye soka la kimataifa. Kinda huyo wa zamani wa Chelsea, mechi yake ya kwanza huko Canada alicheza ile ya kufuzu Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Costa Rica.

Samuel Adekugbe -Canada

Jina jingine kwenye kikosi cha Canada lenye asili ya Nigeria ni Samuel Adekugbe, ambaye alizaliwa England na wazazi wa Kinigeria. Familia ya Adekugbe ilihamia Canada na staa huyo anayechezea klabu ya Hatayspor ya Uturuki, alipewa uraia wa nchi hiyo na hivyo kuwamo kwenye kikosi kilichokwenda Qatar. Amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Canada, ambacho hata hivyo mambo yao hayakuwa mazuri huko Qatar baada ya kusukumwa nje ya michuano kwenye hatua ya makundi.

Columnist: Mwanaspoti