Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kesi ya kusisimua kwa Ramsdale na David Raya

David Raya David Raya

Sun, 8 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Manchester United wakiwa hawajui silaha ya ncha kali inayowapiga usoni, ghafla kuna kesi ya kuvutia inaendelea pale Emirates. Kesi ambayo imekuja ghafla kidogo. Hatukuiona inakuja vema.

United walimuondoa David de Gea katika lango na kumuweka Andre Onana. Nilizungumza hapa wiki iliyopita, aliyeondoka alikuwa hodari katika mikono na aliyekuja ni hodari katika miguu. Inaonekana kama vile ni uhamisho uliowapalia. Wameshaanza kumkumbuka De Gea.

Pale Emirates kuna kesi inayovutia kutoka kwa Mikel Arteta. Amemchukua kipa wa Brentford, David Raya. Kwa wasiomfahamu Raya walidhani kwamba amekuja kuwa kipa msaidizi wa Aaron Ramsidale. Kwa tunaomfahamu Raya tuliguna sana. Ilianzia kule kule Ulaya ambako wachambuzi na wachezaji wa zamani walihoji akili aliyotumia Arteta kuwaweka makipa wawili hodari ndani ya timu moja.

Raya ndiye aliyesababisha De Gea aachwe na kocha wa timu ya taifa ya Hispania katika michuano ya Kombe la Dunia pale Qatar mwaka jana. Sababu ni ile ile ya matumizi mazuri ya miguu. Lakini Raya pia yuko vizuri kwa matumizi ya mikono. Ilishangaza kumuona Arteta akiwaweka pamoja yeye na Ramsdale.

Wakati huo huo, ikumbukwe kwamba Arteta alimuondoa langoni Bernd Leno na kumpatia nafasi Ramsdale akiamini kwamba Muingereza huyu alikuwa tayari kwa kuwa katika lango la Arsenal ndani ya kikosi kipya cha mapinduzi cha mpira wa kisasa pale Emirates. Na kweli Ramsdale alionekana kuwa imara katika lango kuliko Leno.

Lakini sasa Arteta ameonekana kukorofisha mambo zaidi. Langoni amesimama Raya ambaye amewabadilisha akili mashabiki wa Arsenal. Mzuri zaidi katika miguu kuliko Leno lakini pia anadaka kwa ufasaha. Tukifika mwisho wa msimu mchomo mmoja alioucheza dhidi ya Tottenham unaweza kuwa mchomo (save) bora zaidi msimu huu.

Mashabiki pia wamejua kwanini Wahispania walimuacha De Gea na kwenda na Raya. Mashabiki pia walikuwa wakihojiwa nje ya Uwanja wa Emirates na kukiri kwamba Raya ni bora kuliko Ramsdale. Ni kitu kinachowaumiza Waingereza lakini wakati huu Raya akiwa hafanyi makosa wamebakja kimya kidogo.

Waingereza wanapenda wachezaji wa Kiingereza wawepo katika vikosi vinavyowania ubingwa. Namna wanavyompenda Jack Grealish na Man City yake. Namna wanavyompenda Phil Foden na Man City yake. Ni hivyo wanavyopenda wachezaji wao kama Bukayo Saka, Ramsdale, Ben White, Eddie Nkettiah watambe Arsenal. Leo ghafla hawamuoni Ramsdale katika lango la Arsenal.

Wanasubiri Raya akosee ili walipuke. Tayari wameanza kumuhusisha na klabu mbalimbali kubwa. Ni stori za kutengeneza kwa sasa kwa sababu wanaamini Ramsdale anaweza kucheza timu kubwa. Ni kweli wanachokiamini lakini mpaka sasa Raya amethibitisha kwamba anastahili kusimama katika lango mbele ya Raya.

Inawezekana Arteta amefanya hivi kwa sababu Ramsdale alifanya makosa ya kitoto kidogo kuelekea mwisho wa msimu. Au Inawezekana amefanya hivi kwa sababu anajua kuwa ubora wa Raya ambaye ni Mhispaniola mwenzake huku pia alikuwa anapatikana kwa bei rahisi.

Nini kinafuata? Nadhani Ramsdale ataondoka Arsenal. Tatizo kubwa la nafasi yake ni kwamba huwa hawabadilishani. Kipa wa kwanza anakuwa kipa wa kwanza. Kipa wa pili anapewa pambano la Carabao kama alivyopangwa katika pambano dhidi ya Brentford.

Wazungu wana msemo wao usemao “what goes around comes around.” Kwa waswahili msemo huu unamaanisha kwamba ‘Muosha huoshwa’. Kama ambavyo yeye alimfanyia Leno basi ndicho na yeye anachofanyiwa na Raya. Kipa wa kwanza anabakia kuwa kipa wa kwanza. Ni tofauti na nafasi nyingine uwanjani.

Leo Tomiyasu anaweza kucheza kama beki wa kulia au kushoto. Marcus Rashford anaweza kucheza katika wingi zote au mshambuliaji wa kati. Declan Rice anaweza kucheza kama kiungo wa chini au wa juu. Lakini kipa anaweza kucheza langoni tu. Na daima hakuna mzunguko (rotation) kwa makipa.

Kipa bora anaweza kukubali kukaa benchi basi ni yule mwenye miaka 18 anayesubiri nafasi yake, au yule mwenye miaka 34 ambaye anasubiri kustaafu. Kipa mwenye umri wa miaka 25 kama Ramsdale hawezi kukubali kukaa benchi. Yupo katikati ya ubora wake wa soka. Lakini zaidi ni kwamba anasaka nafasi ya kwanza katika kikosi cha England.

Kama Jordan Pickford ataendelea kusimama katika lango la Everton kila wikiendi huku Ramsdale akiendelea kusugua benchi basi ni wazi kwamba shughuli ya Ramsdale kuitaka nafasi ya Pickford itakuwa imeishia hapo. Hawezi kukubali. Simuoni akikubali. Lakini Arteta pia hana ubavu wa kumuweka kikosini mchezaji ambaye hana furaha.

Makipa wawili walio bora na ambao wamesogeleana kwa umri hawawezi kuwa timu moja. Labda iwe katika kikosi cha timu ya taifa. Allison Becker na Ederson unaweza kuwaweka katika kikosi kimoja cha timu ya taifa, lakini hauwezi kuwaweka pamoja Manchester City. Hii ndio asili ya nafasi yao.

Kinachochekesha na ambacho hakiwezi kufikirika ni pale Manchester United watakapoweka dau mezani kumtaka Ramsdale katika dirisha la Januari. Nawaza kijinga lakini ni jambo linalowezekana kabisa. Sidhani kama rafiki yangu Onana ana maisha marefu pale Old Trafford. Nawaza ujinga tu lakini Waingereza wataupenda uhamisho huu. Nawaza ujinga tu kwamba hautaweza kutokea kwa sababu Arteta atakuwa anaiimarisha United ambayo mpaka sasa inaelekea kujifia. Itakuwa hadithi ya Arsene Wenger kumuuza Robin Van Persie kwenda Manchester United akawapa ubingwa wa England.

Itakuwa hadithi ya namna alivyowauza Samir Nasri, Emmanuel Adebayor, Gael Clichy, Bacary Sagna kwenda Manchester City akawaimarisha wapinzani. Wadadisi wengi wa mambo ya soka hawajawahi kumuelewa Wenger mpaka leo. Kwanini uchukue uamuzi ambao unamuimarisha mpinzani? Ramsdale atakuwa mtego.

Kesi ya Ramsdale na Raya inavutia. Tusubiri na kuona kinachoendelea. Sioni kama Ramsdale ataendelea kuwa na Arsenal msimu ujao. Sidhani kama ana maisha marefu sana pale Emirates Stadium. Ndivyo maisha ya soka yalivyo. Hii sio mara ya kwanza kutokea na wala haitakuwa mara ya mwisho.

Columnist: Mwanaspoti