Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Katika kila Arteta mmoja kuna Graham Potter wanne

Arteta With Potter Katika kila Arteta mmoja kuna Graham Potter wanne

Sun, 9 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Stamford Bridge, Mtaa wa Fulham, katika jiji la London anuani namba London SW6 1HS, kuna mtu amefukuzwa kazi. Graham Potter. Inasikitisha kidogo. Na sasa anarudi uswahilini kuendelea na maisha yake mengine. Anaweza kupata kazi haraka iwezekanavyo, lakini imenikumbusha kitu.

Kila unaposoma stori ya kusisimua ya mtu mmoja aliyefanikiwa, tena kwa njia ngumu, basi kumbuka kuna watu wengine wengi walifeli katika njia hizo hizo licha ya kujitahidi kwao kama huyo aliyefanikiwa. Tatizo huwa hatuambiwi ukweli kuhusu waliofeli. Huwa tunasimuliwa zaidi kuhusu waliofaulu.

Imenikumbusha kwamba katika kila Mikel Arteta mmoja kuna Graham Potter wanne. Katika kila Pep Guardiola mmoja kuna Graham Potter sita. Maisha sio rahisi kama tunavyodhani. Tazama namna ambavyo Potter alichukuliwa Chelsea halafu tazama namna alivyochukuliwa na Chelsea halafu tazama mwanzo wa Arteta na Pep.

Kuna wakati inatokea ghafla unakuwa kocha mpya katika soka na watu wanakuamini wanakupa jukumu zito. Kwa Pep ilianzia alipokuwa katika timu ya vijana ya Barcelona. Inaonekana alikuwa anafanya vitu vizuri vya kustaajabisha. Wakampa timu ya wakubwa ambayo awali ilikuwa katika mikono ya Frank Rijkaard. Akafanya vema.

Tena Pep alitushangaza kwa maamuzi yake magumu ya awali. Amefika tu akawaondoa Ronaldinho, Deco na kisha Samuel Etoo. Tulidhani alikuwa mwendawazimu. Baadaye kilichotokea kimetuachia kumbukumbu ya kupendeza katika historia ya soka. Alitutengenezea Barcelona ya kustaajabisha chini ya Andres Iniesta, Xavi Hernandez na zaidi ya kila mtu, Lionel Messi.

Hadi leo Pep ni kocha wa maana. Hajawahi kufukuzwa popote pale. Ni mmoja kati ya makocha bora kuwahi kutokea katika uso wa ulimwengu. Ukijaribu kufikiria kwamba alitokea timu ya vijana ya Barcelona kabla ya kwenda kwa wakubwa, bila ya kutokea timu yoyote kubwa hapo awali, inakupa picha inayopendeza.

Mgeukie Mikel Arteta. Amekuwa kocha wa maana katika timu kubwa kama Arsenal na anaelekea kuipa ubingwa wa kwanza Arsenal baada ya miaka 19. Ni kama Mungu atamjalia. Inachekesha kidogo kwa sababu Arsenal walimuamini kumpa timu huku wasifu wake ukionyesha kwamba alikuwa kocha msaidizi wa Pep Guardiola pale Etihad.

Aliyefukuzwa Emirates alikuwa kocha mwenye wasifu mkubwa kuliko yeye. Unai Emery. Mwanzoni Arteta alionekana kuyumba, huku akijitafuta. Baadaye akachukua maamuzi magumu kama yale yale ambayo Pep aliwahi kuchukua pale Barcelona. Arteta aliwaondosha Mesut Ozil na kisha baadae Pierre-Emerick Aubameyang. Tulishangaa lakini kuanzia hapo Arsenal wamecheza soka la juu zaidi kuliko walipokuwepo.

Niliamini Graham Potter alikuwa anakwenda kufuata mkondo wa kina Pep. Sawa, hakutokea timu ya vijana, wala hakuwa msaidizi wa mtu mahala. Chelsea ilimtoa Brighton and Hove. Haikuwa bahati mbaya. Walikuwa wanacheza soka maridadi chini yake. Kwa tulioijua Brighton tuliamini kwamba Chelsea walikuwa wamefanya maamuzi sahihi.

Sawa sokoni kulikuwa na makocha wengi wenye wasifu mkubwa ambao hawakuwa na kazi. Kina Zinedine Zidane na wengineo wengi. Lakini hata wakati Barcelona na Arsenal walipoamua kuwachukua Pep na Arteta sokoni kulikuwa na makocha wengi ambao walikuwa na wasifu mkubwa kuliko wao. Hivyo hayakuwa maamuzi mabovu kutoka kwa Chelsea.

Na nadhani Potter aliingia Chelsea akiwa na wasifu mzuri kidogo kuliko Pep na Arteta walivyoingia katika vikosi vya Barcelona na Arsenal. Fikiria Brighton ile ya kina Leandro Trossard, Sol March, Yves Mesuma na wengineo ilivyokuwa inaupiga mwingi. Kama Potter angepeleka kitu kile kile Chelsea basi ingekuwa ya moto. Chelsea ina pesa nyingi na mastaa wakubwa kuliko Brighton.

Hata hivyo Potter ameshindwa vita. Unajaribu kutafuta sababu za msingi unazikosa na mwishowe unaishia kumuonea huruma tu. Binafsi naamini alikuwa kocha sahihi kwa Chelsea. Labda alihitaji muda zaidi na mamlaka timilifu kuweza kufanya kile ambacho alikifanya Brighton.

Unapokuwa na timu kama Brighton unakuwa na mamlaka kamili na unaweza kutimiza unachokitaka. Unapokuwa Chelsea presha ni kubwa, wachezaji wakubwa, kila kitu kikubwa. Hauwezi kupata mamlaka kamili kwa haraka. Inabidi uwe na bahati kupata mafanikio ya haraka ili uweze kupata mamlaka ya haraka. Potter hakuwahi kupata.

Arteta ana bahati ya kuvumiliwa. Kuna nyakati tulikuwa tunamuona akiwa anaenda ukingoni. Tukasikia mashabiki wengi wa Arsenal wakisema 'Arteta OUT'. Hadi leo hatujui kwanini alipona katika mawimbi. Labda kama Potter angepata bahati kama ya Arteta si ajabu angeweza kufanya mambo mazuri bahati.

Inaonekana ni mambo yanayohitaji muda. Pep alikuwa miongoni mwa watu ambao waliisihi Arsenal isiachane na Arteta akiamini kwamba alikuwa mtu sahihi kuibadilisha Arsenal licha ya mawimbi makali ambayo walikuwa wanapitia. Na arteta alikuwa miongoni mwa watu ambao walimkingia kifua Potter asifukuzwe akiamini kwamba angebadilisha upepo.

Hata hivyo, matokeo yaliendelea kuwa mabovu zaidi na zaidi. Binafsi licha ya kuamini kwamba Potter alikuwa kocha mahiri na angeweza kubadili mambo siku za usoni kwa Chelsea lakini napata wakati mgumu kuwalaumu Chelsea. Matokeo yaliendelea kuwa ovyo. Na hapo hapo unakumbuka kwamba kila kwenye Arteta wanne kuna Potter mmoja. Kwamba haikuwa lazima pia Potter kufanikiwa Stamford Bridge.

David Moyes aliifanya Everton kuwa moto. Alipoteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Manchester United baada ya kuondoka kwa Sir Alex Ferguson watu wengi tuliamini kwamba yalikuwa maamuzi sahihi kwa sababu kama angehamishia kile kile ambacho alikuwa anafanya Everton kwenda kwa Manchester United ambayo ina pesa nyingi basi angefanikiwa. Hata hivyo, haikuwezekana.

Kuna wakati unajikumbusha stori za mafanikio za makocha vijana walioaminika mahala na kisha wakafanya vema, lakini kuna wakati pia unajikumbusha stori za makocha vijana waliochemka mahala. Hapo mabosi na mashabiki wanashindwa kumuamini kocha aliyepo madarakani. Inasemwa kwamba hata tajiri wa Chelsea alikuwa anamuamini Potter kwa kiasi kikubwa na ndio maana amechelewa kumtimua lakini presha imekuwa kubwa kutoka kwa mashabiki.

Wakati unapokumbuka stori za kina Arteta na Pep, hapo hapo unajikumbusha stori za kina Moyes, Frank Lampard, Steven Gerrard, Patrick Vieira, Andrea Pirlo na wengineo ambao wanaonekana kama wamefeli licha ya kutazamiwa kufanya makubwa katika kazi hii.

Bahati nzuri kwa Potter ni kwamba anatakiwa na Leicester City. Nadhani watu wa Leicester wanaamini kwamba Potter atawafanyia kile ambacho aliwafanyia Brighton. Kwa sababu wao sio watu wenye presha kama Chelsea basi wanaweza kumpa muda kufanya anachotaka. Na kama timu yao itafanya kama kile ambacho Brighton walifanya chini ya Potter basi watajihisi salama tu. Hawana shida.

Kitu ambacho hatujawahi kukiona mara nyingi ni pale mtu wa aina ya Potter anapofukuzwa kazi halafu akarudi timu ndogo, halafu akafanya mambo makubwa na kuaminiwa kurudi tena katika timu kubwa. Mara nyingi makocha wa aina yake wakizama huwa wanazama kabisa.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: