Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Kasi ya Rais Samia itawasaidia wenye mashaka’

9f1774d550af006fc9b966772f3099cb ‘Kasi ya Rais Samia itawasaidia wenye mashaka’

Mon, 29 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATAALAMU wa saikolojia na madaktari wamesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itafanya kazi kwa ari na kasi ya Rais John Magufuli itakuwa tiba ya kisaikolojia kwa Watanzania waliopata mashaka baada ya kifo cha kiongozi huyo.

Rais Magufuli alikuwa Rais wa Tano wa Tanzania tangu mwaka 2015. Alifariki dunia Machi 17 mwaka huu kwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.

Msaikolojia Tiba wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania (MEHATA), Dk Isaac Lema, alisema ni kawaida kwa binadamu wanapofiwa na mpendwa wao kuwa na mabadiliko ya kihisia ikiwemo huzuni, kutoamini kilichotokea, kuwa na hasira na kujiuliza maswali.

Alisema hisia hizo huwafanya watu kuwa katika hali ya wasiwasi, hofu, taharuki, sononeko, msongo wa mawazo na mfadhaiko.

“Sasa hisia na hali hizi kumtokea mtu ni kawaida, na kwa kuwa haya yote ni ya kawaida, sayansi inasema kwamba inatuhitaji wiki mbili na kuendelea kwa mtu kurudi katika hali yake ya kawaida hasa baada ya mwili kuzikwa,”alisema Dk Lema.

Naye Mtaalamu wa Saikolojia ambaye pia ni Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), John Ambrose, alisema wananchi wengi hasa wa kawaida waliumzwa na kifo cha Rais Magufuli kwa sababu wanaona uhuru na tumaini lao limepotea.

Ambrose alisema kutokana na hali hiyo, kuna mambo ambayo Serikali ya Rais Samia inapaswa kuyafanya ili kuleta tiba ya kisaikolojia kwa Watanzania na kuwarejeshea matumaini.

Alisema mambo hayo ni pamoja na hatua ya kijasiri aliyoichukua Rais Samia ya kuungana na Watanzania kwa kumzungumzia Magufuli kwa mazuri aliyoyafanya, kumwelezea kama mwalimu wake na alijifunza mengi kwake hali inayorejesha matumaini kwa wananchi na kumuona kuwa ni mwenzao na atashirikiana nao.

“Ni vyema Rais Samia, makamu wa rais atakayekuja na waziri mkuu, wakaendelea kuyazungumzia kila wakati mambo aliyoyafanya Magufuli, pia kipindi cha miaka minne ijayo chini ya Rais Samia kusiwe na mfumo mpya, bali kiende katika mfumo ule ule wa uongozi wa Magufuli katika kutekeleza mambo ya msingi hasa yanayogusa maslahi ya wanyonge,” alisema Ambrose.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Tiba Asili ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), Bonaventura Mwalongo, alisema ni kawaida na ni hulka ya binadamu kutaharuki linapotokea jambo kubwa lisilotarajiwa.

Mwalongo alisema kitendo cha Watanzania kushtuka, kulia, kuomboleza na kujiuliza mengi kuhusu kifo cha Rais Magufuli ni jambo la kawaida kwa sababu Magufuli aligusa maisha ya watu wa chini, wanyonge na maskini.

Alisema pia ni jambo la kawaida taharuki kuwakumba watu waliopo kwenye mamlaka waliokuwa wakitekeleza majukumu mbalimbali kutokana na kuwepo kwa Rais Magufuli.

“Namna gani watu hawa wanaweza kupata tiba kisaikolojia, ni kufarijiwa kwa kujengewa uhakika wa yale ambayo Rais Magufuli alikuwa akiyasimamia, kuyatetea, aliyotamani yawe, hivyo kila kiongozi aliyepo aone kuwa ana jukumu la kuendeleza kazi nzuri ambazo Hayati Rais Magufuli alizisimamia,” alisema Mwalongo.

Akaongeza: “Pia Serikali ya Rais Samia iweke mwelekeo kamili ili kuwafanya wananchi kuwa watulivu, wafanye kazi kwa juhudi, kujituma, kuenzi mazuri na kazi nzuri alizofanya Rais Magufuli na kuziendeleza, kuibua miradi mipya mikubwa, kuimarisha taasisi za umma, wananchi kupata huduma za jamii kwa gharama nafuu na kulinda rasilimali za nchi yetu.”

Columnist: www.habarileo.co.tz