Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Kashfa za ufisadi zinavyowatesa Marais duniani

Ufisadi.jpeg Kashfa za ufisadi zinavyowatesa marais duniani

Thu, 7 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Wakati wananchi wa mataifa mbalimbali duniani wakitaabika kwa dhiki na umasikini, viongozi wao na familia zao wamekuwa wakiogelea kwenye utajiri mkubwa uliohifadhiwa nje ya nchi.

Kama utajiri huo ungekuwa unahifadhiwa au kutumika katika nchi zao ungechochea ukuaji wa uchumi, ajira na viwanda lakini hawawekezi katika nchi wanazoziongoza wakihofia hasira za wananchi, kukwepa kodi na sheria mbalimbali zinazowabana.

Baadhi ya viongozi hudiriki kufanya safari mbalimbali za kwenda kukutana na wawekezaji ili wakawekeze kwenye mataifa yao ilhali wenyewe wana uwezo wa kufanya hivyo kutokana na utajiri wa siri walionao.

Ripoti mpya ya ufisadi na ukwepaji kodi duniani, inaiweka Tanzania na viongozi wake nje ya mstatili wa kashfa. Hata hivyo, inaendelea kuzungukwa na mataifa ambayo wanasiasa wake na watumishi wa umma wametajwa kwenye orodha.

Taasisi ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi (ICIJ), yenye maskani yake Washington DC, Marekani, Septemba 3, mwaka huu, ilitoa ripoti yenye kuwaonesha wanasiasa 336 duniani, wenye kampuni zinazofanya kazi kwa kukwepa kodi, vilevile wanaojipatia fedha kifisadi, hata hivyo baadhi ya waliotajwa wamekana

Ripoti hiyo iliyopewa jina la “Pandora Papers” , inafuatia ile ya Mei 10, 2016, iliyotolewa na ICIJ na kupewa jina “Panama Papers”. Ndani ya ripoti zote hizo, Tanzania haijaguswa, isipokuwa majirani zake.

Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Msumbiji, Rwanda na Malawi, ni nchi zinazopakana na Tanzania, ambazo kwa namna moja au nyingine, wanasiasa wake na watumishi wengine wa umma, wameorodheshwa.

Kabla ya mwaka 2015, kwa hoja nyingi zilizokuwa zikijengwa kuhusu ufisadi Tanzania, usingedhani ICIJ, wangechapisha matoleo mawili ya orodha ya viongozi wenye utajiri wa siri duniani pasipo hata jina moja la Mtanzania.

Mwaka 2007, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Willibrod Slaa, wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Chadema na mbunge wa Karatu, alitoa orodha aliyoiita ya mafisadi (list of shame). Akiwa Mwembeyanga, Temeke, alitaja majina 11 ya vigogo aliodai walikuwa wakiifilisi nchi.

Orodha hiyo ya mafisadi, ilifuata baada ya kashfa kubwa kubwa wa uchotwaji fedha, Benki Kuu Tanzania, kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA). Sh133 bilioni zilichotwa. Rais aliyekuwa madarakani, Jakaya Kikwete, akamfuta kazi aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, marehemu Daudi Balali.

Mwaka 2008, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, alijiuzulu. Ni baada ya Taasisi ya Makosa ya Ufisadi UK (SFO), kuonesha kuwa Chenge alikuwa na fedha dola 1.5 milioni, kwenye kisiwa cha Jersey, Uingereza. Fedha hizo zilihusishwa na mgao wa kifisadi katika ununuzi wa Rada kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza.

Ongeza kashfa nyingine kama Richmond, iliyohusisha mkataba mbovu wa mradi wa ufuaji umeme wa dharura kati ya Kampuni ya Richmond LLC na Tanesco. Halafu kuna ‘skendo’ nyingine ya uchotaji fedha Benki Kuu kwenye akauti ya Tegeta Escrow.

Isisahaulike, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliwahi kutamba na orodha ya vigogo walioficha mabilioni ya fedha Uswisi. Hivyo, hadi kufikia mwaka 2015, Tanzania ya kwenye majukwaa ya kisiasa na vyombo vya habari, iliogofya kwa ufisadi. Ajabu, si Panama Papers wala Pandora Papers, iliyoitaja Tanzania.

Columnist: mwananchidigital